Pages

Pages

Wednesday, August 12, 2015

Kura za maoni jimbo la Handeni zazidi kuwaka moto

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HALI imezidi kuwa tete katika Uchaguzi wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea Ubunge, Jimbo la Handeni, wilayani Handeni, mkoani Tanga, baada ya kubainika mapendekezo yaliyofikiwa na Kamati ya Siasa na Maadili hayajafikishwa kwenye Kamati Kuu, kwa sababu ya kuwabeba baadhi ya wagombea waliokuwa kwenye mchakato huo.
Wagombea wa Ubunge CCM jimbo la Handeni, Dr Seif Mhina, John Salu, Chifu Msopa, Mboni Mhita, Ahmed Bwanguzo, Ramadhan Mahiza na Kambi Mbwana mwenye koti, walipokuwa kwenye kampeni hizo Handeni.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Handeni, Salehe Kikweo, yalionyesha kuwa mgombea John Salu, aliongoza, lakini alikiri kuwa hayo si matokeo halisi kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni pamoja na wagombea watano kupita njia za panya, vikiwamo vitendo vya rushwa kwenye mchakato huo wa Ubunge Handeni.

Akizungumza kwa hisia kali, mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Ramadhan Mahiza, aliuambia mtandao huu kuwa ofisi ya CCM Handeni, imeidanganya Kamati Kuu, chini ya mwenyekiti wake wa CCM Taifa, Mh Jakaya Mrisho Kikwete, kutokana na ripoti na mapendekezo ya vikao halali kutofika mezani kwa ajili ya kujadiliana juu ya kumpata mtu anayekubalika kwa wananchi wote.

Alisema katika mchakato huo wa ubunge Handeni, wapo wagombea walioguswa moja kwa moja kutoa rushwa na kugawa madera ambayo waliokamatwa walikiri, hivyo suala hilo kumalizwa kwa kutoa mapendekezo ya kuwaengua wagombea watano wa nafasi hiyo ya ubunge Handeni.
“Katibu Kikweo alitueleza kwamba hakuna haja ya kuweka mgomo wowote, kwa sababu mshindi halali atajulikana baada ya vikao vya Kamati ya siasa na maadili kukaa, kamati ambazo kwa maslahi makubwa ya kulinda hadhi ya chama ilipendekeza watu hao waunguliwe,” alisema Mahiza na kushangazwa na matokeo ya kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa majimbo matano ambayo ni Ukonga, Busega, Kilolo, Makete na Rufiji, huku Handeni ikiwekwa kando.

Naye Ahmed Bwanguzo, alisema kwamba kimsingi uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki, huku ikishangaza kwanini Katibu wa CCM wa wilaya Handeni, ametumia nguvu kubwa kuwabeba baadhi ya wagombea mchana kweupe pamoja kushindwa kutumia haki ya msingi ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Huwezi kuwapeleka washindi ambao hawana uwezo wa kujenga hoja jukwaani, wakiwamo wale waliotumia nguvu kubwa ya kifedha ili washinde katika uchaguzi huo, hivyo sisi kama miongoni mwa wagombea hao hatukubaliani na matokeo hayo na kila aliyeguswa na tuhuma haki itendeke,” alisema Mtemi.

Mgombea mwingine Kambi Mbwana, aliyesema kuwa haoni kwanini uchaguzi huo umesiginwa kwa makusudi, hali inayoweza kukiangusha chama tawala katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

“Kimsingi hakuna mgombea anayejua amepata kura ngapi na wapi amekosa, maana hata huyo Salu anayedaiwa ameshinda amepewa ushindi wa jumla na hakuna anayejua namna gani mchakato huo umefanyika, ndio maana ofisi ya CCM wilaya iliamua kufanya siri, huku kila mgombea akiambiwa jambo la kumpa moyo,” alisema Mbwana.

Naye Chifu Msopa alisema kwamba hawawezi kukubali mtu mmofa afanye mambo kwa maslahi yake, hivyo wagombea wote wa ubunge watasusia mchakato wa kampeni katika jimbo la Handeni, kama hali ya kubebana itaendelea dhidi ya Katibu na washindi wake aonao wanafaa kuliko wengine.

“Hatutaki kuendelea kuwa waoga huku wachache wakiendelea kuiharibu CCM yetu, uchaguzi huu urudiwe au kufuata maagizo ya Kamati ya Siasa ya wilaya na ile ya Maadili ambayo kwa bila kujua kwanini, Katibu aliyaweka kando mapendekezo hayo na kufanya anavyotaka mwenyewe,” alisema Msopa.

Kwa kipindi cha wiki moja sasa jimbo la Handeni limekuwa kwenye mgogoro mkubwa kati ya viongozi wa CCM wilaya ya Handeni na wagombea ubunge ambao kwa kiasi kikubwa wameonyesha kuchukizwa na mwenendo mbovu wa katibu wa CCM handeni, ambaye ameendelea kuwabeba wagombea, wakiwamo wale waliotajwa kwenye kashfa za rushwa.

No comments:

Post a Comment