Pages

Pages

Monday, July 06, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Hatuwezi kuendelea bila soka la vijana lenye dira

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), kwa kupitia Rais wake Jamal Malinzi, limesema halina makosa katika ufanyaji vibaya wa timu yake ya Taifa, akiaminisha kwamba wachezaji ndio wa kulaumiwa.

Malinzi aliyasema hayo siku alipotangaza kusitisha ajira kocha wake Mart Nooij, ambaye sasa nafasi yake imechukuliwa na kocha mzawa, Charles Boniface Mkwassa. Hata hivyo katika kuangalia mwenendo wa soka la Tanzania, ni wazi TFF inaweza kuingia kwenye makosa, maana bado haliweki mkazo katika soka la vijana, hususan maeneo ya mikoani.Huko kuna vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka. Hakuna juhudi za kuwaibua na kuwaendeleza. Tumeendelea kusubiri mashindano ya Diwani Cup ambayo mara kadhaa hufanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu. Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Hii ni kwa sababu tusipokuwa na mipango ya dhati, hatuwezi kusonga mbele. Kama TFF itawabana viongozi wa vyama vya soka vya mikoani na wilaya ili kuona namna bora ya kuwa na mashindano makubwa yenye tija, walau tutasonga mbele.

Lakini kuendelea kusubiria wachezaji kutoka Simba na Yanga ni kujisumbua, kwa sababu bado si wote wanaweza kupata nafasi katika timu hizo kongwe za Tanzania. Lazima tukubali kuwa mfumo wetu wa soka la Tanzania una tatizo kubwa, kwakuwa hakuna mbinu za kuibua vijana wazuri kwa maendeleo ya mpira wa miguu wa Tanzania.  Hatuwezi kupiga hatua. Tutaendelea kulalama kila siku, huku muda mwingi ukipotea na pengine kushuka chini zaidi na zaidi. Mkwassa si suluhisho la soka la Tanzania. Mwarobaini wa soka la Tanzania ni kuona wachezaji wengi vijana wanapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Kinyume cha hapo hakuna kitu. Tutatimua makocha kila siku. Matokeo yake hata wadau wanaosaidia soka, kama vile makampuni au hata mashabiki watachoka, kwakuwa huwezi kushabikia kitu kisichokupa furaha. Huo ndio ukweli wa mambo. Tunapaswa kuweka mipango na mikakati yenye tija kwa mustakabali wa soka la Tanzania. Kinyume cha hapo hakuna kitu.Tuonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949




No comments:

Post a Comment