Pages

Pages

Monday, June 15, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Sakata la Singano na hadithi ya fisi akiwa hakimu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAHITAJI akili za kiuwendawazimu kukubali mwenendo mbovu wa soka la Tanzania, linaloendeshwa kwa mizengwe mizengwe. Leo mtu anaweza kuharibu mkataba wa kisheria kwa makusudi na bado asiburuzwe katika vyombo vya sheria.

Ndio, maana tumeshuhudia Shirikisho la Soka nchini (TFF) kulimaliza sakata la mchezaji wa Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’, kitu ambacho wengi walikitarajia. Hii ni aibu kubwa, maana TFF waliamua kulifunika funika.

Mwenyewe Singano anasema anamuachia Mungu. Pengine aliyasema haya kwa sababu alijua kwamba hawezi kuipata haki aliyokusudia. Kama hivi ndivyo, nakumbuka msemo mmoja wa Kiswahili usemao ‘Fisi akiwa hakimu, mbuzi sheria hana’. Ndio, TFF wao wanamtaka Singano na klabu yake warekebishe mapungufu kwenye mkataba wao.

Kurekebishwa kunaashiria kuwa kuna tatizo kubwa. Lipi hilo? Kwanini tatizo hilo lisiwekwe hadharani ili kila mmoja alijuwe? Hii inaonyesha kwamba kuna dalili za kulindana. Ni wazi kati ya Simba au Messi, kuna mmoja anatatizo.

Ila kulifumba fumba si njia ya kusuluhisha mzozo huo. Hata kama leo hili likiisha, vizazi vinavyo vitaendelea kuwa na kasumba hii. Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kuona soka letu linaendelea kuendeshwa kienyeji na kiubabaishaji.

Hatuwezi kuendelea kamwe. Tunahitaji kutunga sheria na kanuni na kuziishi. Hii kuziba ziba na kulindana kutaliweka soka letu kwenye mashaka makubwa. TFF inapoamuru kurekebisha mapungufu kwenye mkataba wa Singano, kunamaanisha kubariki uozo wowote uliokuwapo kwenye pande hizo.

Kwanini tusizidi kubaki kama tulivyo? Bado tutalalamika kwamba soka letu haliendelei? Hatuwezi kupiga hatua kamwe. Singano analalamika mkataba wake umechezewa. Badala ya kuangalia umechezewaje, tunakuwa bubu kwa sababu tunazojua wenyewe.

Kesho mkataba huo utachezewa tena na tena. Kama Singano amedanganya, tunapaswa kuchunguza kwanini amedanganya ili apewe adhabu. Haya sasa, siku moja baada ya uamuzi huo kutoka, Simba hao hao wanaibuka tena na kusema hawawezi kufanya lolote likiwamo kuangalia marekebisho hayo kwa sababu wana mkataba halali na Singano.

Huu ni ujinga wa karne. Nathubutu kusema kuna dalili za wazi za kuharibu kipaji cha kijana huyu ambaye Taifa linamtegemea kutokana na kipaji chake. Kama TFF ingekuwa makini, siku ile ile ya kikao chao cha kuangalia suala hilo, wangebaini tatizo na kulitatua.

Ipi kazi ya TFF? Au ndio fisi akiwa hakimu, mbuzi hana sheria? Hatuwezi kuendelea kwa ubabaishaji huu katika nyanya ya mpira wa miguu kwenye nchi yetu na siwezi kuvumilia.
Tuonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949

No comments:

Post a Comment