Pages

Pages

Monday, June 29, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Mashabiki wamekosea, ila Stars imekosea zaidi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI miongoni mwa wadau wa michezo hususan mpira wa miguu waliohudhunishwa na kitendo cha hivi karibuni cha baadhi ya mashabiki wa soka walioamua kuwazomea wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars), hali iliyoibua utata baina yao. Ingawa nilihudhunishwa na suala hilo, lakini pia nilihudhunika zaidi kwa kitendo cha wachezaji kushuka na kufanya fujo kwa mashabiki wao, ambao kimsingi wameguswa na matokeo mabovu ya timu yao ya Taifa, licha ya kuwa na mapenzi nayo. Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwa sababu inaonyesha wachezaji hawana nidhamu. Na hawajui kuwa kiasi gani matokeo yao mabaya hupelekea wengine kuugua au kujisikia vibaya.

Hii haiwezi kukubalika na haivumiliki pia. Ni wakati sasa wachezaji wa Stars kujua wana deni kubwa. Wanapoingia uwanjani wahakikishe kuwa wanafanya kila wawezalo kupata ushindi. Na inapotokea wanapata matokeo mabaya, lazima wajue pia watawafanya mashabiki wao wahisi presha. Ni kutokana na presha hizo, baadhi ya wadau na mashabiki wanaona hakuna njia nyingine ya kufikisha ujumbe kwa wachezaji wao zaidi ya kuzomea.

Ingawa hii si tabia nzuri dhidi ya mashabiki hao, lakini kwa wachezaji kushuka chini na kufanya vurugu ni kubaya zaidi. Ingekuwaje kama mashabiki hao walipoanza kuzomea gari lingeondoka, mashabiki hao wangelikimbilia hadi linapoishia? Ni wazi wangeliacha ili waendelee na zao. Ni wakati wetu sasa kila mtu kuwa na mapenzi dhidi ya mwenzake. Wachezaji wawe na nidhamu mbele ya mashabiki wao hali kazalka mashabiki nao wawe na nidhamu kwa wachezaji wao.

Kucheza mpira si jambo dogo. Kunahitaji nguvu na akili kubwa katika kusaka ushindi uwanjani, hivyo kuna kila sababu ya kuona namna gani ushindi unapatikana. Huu ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo tutaendelea kuona mwenendo mbaya dhidi ya timu yetu, huku wachezaji wetu wakiongeza ukali kwa mashabiki wao. Je, watawatoa roho? Huu ndio ukweli wa mambo. Mashabiki kuwafanyia vurugu wachezaji wao ni kibaya, ila wachezaji nao kushuka chini kufanya fujo ni kubaya zaidi. Ingekuwaje kama wachezaji wangeumizwa kwenye vurugu hizo?

Tubadilike kama kweli tunahitaji maendeleo ya mpira wa miguu.
Tuonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949

No comments:

Post a Comment