Pages

Pages

Tuesday, June 02, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Kwa ubabaishaji wetu, hakuna kocha mzuri ndani ya Simba na Yanga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WENYEWE wanaziita Kulwa na Dotto. Eti Yanga ni Kulwa na Simba ni Dotto. Kama majina haya hayaendani nao, basi yanakaribia kabisa na tafsiri ya majina yao haya.


Wanafanana mizengwe na ubabaishaji. Hata migogoro pia hurithishana, ukitoka Simba, utahamia Yanga. Klabu mbili hizi ambazo ni kongwe, hazijawahi kukaa miaka mitatu mfululizo bila migogoro.  Na kwa miaka ya karibuni, wamezidi.


Mbali na migogoro hiyo, klabu hizi zimekuwa na kawaida ya kubadilisha makocha kama nguo za ndani. Labda wanatafuta kocha mwenye mafanikio zaidi ya Sir Alex Ferguson, aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Manchester United ya nchini Uingereza.


Kama huo ndio mtazamo wao, basi wanajidanganya. Wanajipotezea muda,  maana ndani ya timu hizi kongwe hakuna kocha mzuri. Hata akiwa mzuri, ataharibiwa na mizengwe yao.
Hadi leo hawaheshimu makocha wao.  Mwenyekiti au kiongozi wa klabu anaingilia upangaji wa timu bila kuona athari zinazoweza kujitokeza kwenye klabu yao.


Na ikitokea timu inafungwa, wanajaribu kuwasumbua wataalamu hao ambao wengi wao wamekuwa wakiishi kwa kubangaiza wasiojua kesho yao itakuwaje.


Hakika siwezi kuvumilia. Ni wazi klabu hizi kongwe zinazoitwa dira ya soka la Tanzania kwa ngazi ya klabu kuwa makini katika utendaji kazi wao na namna ya kusaka mafanikio.

Huu ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo klabu hizi zitaendelea kusua sua kwa sababu hawatakuja kuheshimu utaalamu wa makocha wao, ambao ni watu wenye kupaswa kuheshimiwa na kusikilizwa maoni yao kwa maendeleo ya timu zao.


Tanzania imeshindwa kupiga hatua katika nyanja ya mpira wa miguu kwa sababu mbinu zinazotumika ni duni, huku zikichagizwa na ubabaishaji mkubwa wa viongozi wa timu zetu, hususan Simba na Yanga, zinazoitwa Kulwa na Dotto.


Tunataka ushindi. Tunataka mafanikio. Mafanikio yanayoweza kuja kwa kujipanga kuanzia utawala na ufundi, kwa kupitia makocha wetu wanaopaswa kulipwa vizuri na kusikilizwa pia namna wanavyotaka kuziendesha timu zetu.
Tunaonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949

No comments:

Post a Comment