Pages

Pages

Monday, May 18, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Timu tatu, Mkoa wa Tanga utakuwa na cha kujivunia?



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LIGI ya Tanzania Bara itakayoanza baadaye mwaka huu, itakuwa na raha za aina yake, baada ya mkoa wa Tanga, kupata timu tatu zitakazoshiriki Ligi hiyo.
Timu hizo ni Coastal Union, Mgambo Shooting ya wilayani Handeni na ile African Sports, iliyopanda daraja msimu huu, ikijikatia tiketi ya kushiriki ligi hiyo kubwa nchini Tanzania.

Kushiriki kwa timu hizo, mkoa wa Tanga utakuwa unashika nafasi ya pili nyuma ya jiji la Dar es Salaam, ambalo lenyewe lina timu ya Yanga, Simba na Azam FC. Hata hivyo, mkoa wa Tanga unapaswa kujipanga ili kushiriki kwa timu hizo tatu kuwe na cha kujivunia. Namaanisha kupata ushindani wa aina yake. Kusiwe na timu ya kufungwa kila mechi. Itakuwa ni aibu kubwa.

Katika kuangalia mfumo uliopo, ni wazi mkoa wa Tanga utakuwa umepanda kiasi fulani katika sekta ya mpira wa miguu, jambo linalohitaji ushirikiano pia kutoka kwa wadau wa michezo, wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia. Hii ni kwa sababu kusipokuwa na mipango, timu hizo zitaendelea kusua sua. Ni Mungu tu, ila ni wazi Mgambo ilibaki kidogo ishuke daraja. 

Kwa sababu imenusurika, kila mdau wa michezo wa mkoa wa Tanga ahakikishe anafanya bidii kuliweka soka lao katika kilele cha mafanikio. Kushiriki kwa Ligi ya Tanzania Bara, ni wazi Mkoa wa Tanga utakuwa na sehemu ya kujitangaza. Pia unaweza kuwa na nafasi nzuri kibiashara kutokana na wageni watakaoingia na kutoka kufuata timu zao kutoka katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Dar es Salaam kunapopatikana timu kubwa na kongwe, kama vile Yanga, Simba na Azam.

Kwa timu kama African Sports na Mgambo Shooting zenyewe zinapaswa kufanya bidii ili kuhakikisha kwamba zinaonyesha soka la uhakika, ili zisiwe katika hatari ya kushuka daraja. Mkoa kuwa na timu tatu zinazocheza Ligi Kuu si jambo dogo. Hata hivyo kunaweza kusiwe na tija kama hakutakuwa na juhudi, mipango na kujituma kusaka ushindi utakaowaweka juu kisoka na kibiashara pia. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia, maana hakutakuwa na jipya licha ya kuwa na timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu katika Mkoa mmoja wa Tanga.
Tuonane wiki ijayo.
+255 7120539

No comments:

Post a Comment