Pages

Pages

Wednesday, May 20, 2015

MGODI UNAOTEMBEA: Joto la wataka urais CCM, linadhihirisha nguvu ya chama tawala


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAHITAJI akili ya kiuwendawazimu kuaminishwa na kuamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza mvuto. Kwamba vinavyokubalika ni Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, NLD, TLP na vinginevyo, ambavyo kwa udhaifu wao, wameona waungane baada ya kukosa dawa ya kukiangusha chama tawala.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ni mmoja wa makada wa CCM, wanaotajwa kuwa na ndoto za kuwania Urais, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nchini Tanzania.

Si kweli, maana vipo viashiria vingi vinavyoonyesha kuwa chama hicho kikongwe Tanzania, kipo imara na kinaungwa mkono na watu wengi, wakiwamo watoto, wazee, vijana na wake kwa waume. Bado wapo watu wanaoamini kuwa mtu mtu anayepitishwa kugombea katika nafasi yoyote ndani ya CCM, basi huyo ndiye mshindi. Na yapo maeneo mengi ambayo watu wake hawajui chochote kuhusu vyama vya upinzani, isipokuwa CCM.

Kuelekea katika Uchaguzi Mkuu, kumekuwa na kauli za hapa na pale zinazoshiria kuwa baadhi ya Watanzania wenzetu, hususan wanaotoka katika Chama Tawala wamedhamiria kuchukua fomu za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Ingawa wapo wengine wenye nia hiyo ya kutaka urais, ila ndani ya CCM hali hiyo imezidi. Ndani ya CCM kuna joto na mchuano mkali. Takribani miaka mitatu sasa tumeshuhudia mivutano ya kila aina.

Wataka urais huo wamekuwa na vikao na safari za kutunisha makundi yao, bila kusahau kasi ya kuongeza ushawishi kwa vijana wao wanaoshindana katika mitandao ya kijamii kwa kujiita majina ya kila aina, kuashiria wapo kwenye msafara huo. Haya yote yanadhihirisha nguvu ya chama tawala. Kila mtu anaangalia nani ana mvuto zaidi ya mwenzake ndani ya CCM. Kila jina linalotajwa zaidi mtaani, basi linatokana CCM.

Wapo wanaomtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwamba anayo haiba na uwezo wa juu ya kurithi kiti cha urais, kitakachoachwa na Rais, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete, baadaye mwaka huu. Wanaoamini Membe anafaa wanafanya kila wawezalo ili jamii iwaelewe, bila kusahau wanaojiita wapo kwenye safari ya matumaini, nao wakichagiza Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli arithi mikoba ya JK.

Si Lowassa au Membe tu, bali wapo wana CCM wengine kede kede walionyesha nia ya kutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiamini uwezo na vigezo wanavyo.
Vipi kuhusu January Makamba, Samuel Sitta, William Ngeleja, Emmanuel Nchimbi, Profesa Sospeter Muhongo, Dkt Asha Rose Migiro, Augustino Ramadhan, Stephen Wassira na majina lukuki yanayotajwa katika ndoto hizo za urais.

Ingawa wenyewe hawajatangaza nia hiyo hadharani, lakini mwenendo wao, harakati zao na pengine matamshi kadha wa kadha yanaonyesha kiu hiyo ya kutakaa kuongoza taasisi nyeti na kubwa nchini Tanzania, kwa kofia ya urais. Kuwa na ndoto ya urais ni jambo moja na kuwa rais ni jambo jingine. Hii ni kwa sababu kunahitaji mipango na ridhaa ya kuaminiwa na Watanzania wote kwa kupitia sanduku la kura. 

Kura zitakazochanganya wagombea kutoka CCM na wale wa upinzani, huku kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za Tanzania, ikidaiwa kuwa vyama vine vya siasa vitasimamisha mgombea mmoja kwa mgongo uitwao UKAWA. UKAWA ni msamiati ulioasisiwa katika Bunge la Katiba, ambapo vyama vine vya vya Chadema, CUF, NCCR MAGEUZI NA NLD, viliamua kuungana, muungano ulioendelezwa pia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji Desemba mwaka jana, wakisisitiza pia utaratibu huo utaendelea kwa madiwani, wabunge na urais.

Pamoja na kuungana kwa vyama hivyo vine, bado hawakaribii nguvu inayotoka CCM. Wagombea wawili, Dk Willbroad Slaa kutoka Chadema na Profesa Ibrahimu Lipumba kutoka CUF ndio wenye kudaiwa wanao uwezo wa kusimama kwa upande wa Bara. Upande wa Visiwani Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ndiye atakayesimama kwa upande wa CUF ama UKAWA, kwa madai chama hicho ndicho chenye nguvu na ushawishi wa kuaminiwa na watu wa Zanzibar. Sawa, lakini vipi wanao uwezo wa kuitingisha CCM? Lipumba aliyegombea urais zaidi ya vipindi viwili Tanzania Bara na akaonekana kachokwa, anaweza kuitikisa CCM?

Hata kama akiitikisa, UKAWA watamuanini na kumpa nafasi hiyo, huku akiwapo Dk Slaa, aliyeshika nafasi ya pili nyuma ya Rais Kikwete, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010?
Hili na mengine mengi yanawafanya hata wale wasioamini CCM, nao wanaingia kwenye wimbo wa nani bora kutoka chama tawala. Wanaamini huko ndiko kwenye mvutano mkubwa zaidi. Na mvutano huo unatokana na nguvu ya chama hiki kikongwe. Chama kitakachotoa rais mwingine baada ya Kikwete aliyeingia Ikulu huku akiungwa mkono na makundi mengi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Ni dhahiri wanaotaka kujua nguvu ya CCM waiangalie namna inavyoweza kumpata pia mgombea wake wa Urais. Ni jambo nyeti linalowekwa katika utaratibu mzuri na wa kueleweka. Hii inaonyesha ukomavu wa juu wa chama hiki. Hawa wote wanaotajwa kutaka urais, wameibuliwa na kukomazwa na chama hiki kikongwe. Waliaminiwa katika nafasi mbalimbali. Na pengine kila mmoja ana uwezo huo wa kusimama kama mgombea urais, huku akishinda kwa kishindo. Uzuri ni kwamba hadi mtu anapoweza kusimamishwa kama mgombea urais kwa tiketi ya CCM, anakuwa amepita katika vikaango lukuki kwa ajili ya kujiridhisha naye. Kwamba ni mtu safi? Ana nguvu na ushawishi mbele ya hadhira?

Anaweza kuaminiwa na Watanzania wote, ukiacha hawa wanaopiga kelele kwenye mitandao ya kijamii, ambao ni dhahiri baadhi yao wanafadhiliwa na majina hayo? Je, anauzika, hana kashfa? Sifa hizi na nyingine kadha wa kadha zitaondoa wasiwasi na uwezekano wa kuungwa mkono na makundi yote nchini Tanzania. Na hapo ndipo panapojibu maswali ya wale wanaoamini mtu anayetoka CCM ndio kiongozi wao.

Huu ndio ukweli wa mambo. Ukweli huu wanaujua pia hata wale walioibukia kwenye siasa za upinzani. Ndio hao hao wanaoanza kupiga porojo kwamba kuna uwezekano mtu anayetoswa ndani ya CCM, atahamia upinzani. Kama hiyo ni kweli, ndio kusema kwamba wagombea na wanaoapaswa kugombea nafasi hiyo ya urais wapo CCM. Na itaingia kwenye kumbukumbu mgombea wa CCM aliyetoswa kwenye urais, amekimbilia upinzani. Ataonyesha uroho wake wa madaraka.

Ataonyesha hafai kuungwa mkono na Watanzania. Ikumbukwe kuwa urais ni nafasi moja inayotokea kwa Mtanzania mmoja kila baada ya miaka mitano au 10 kwa vipindi viwili.
Hii inaonyesha kuwa Watanzania wote hatuwezi kuwa rais wa nchi hii. Hivyo ili iendelee, lazima tuache tamaa zetu. Wote hatuwezi kuwa rais kwa kipindi cha miaka mitano au 10.
Tuvumiliane, tuheshimiane na pengine tuwe na uzalendo halisi wa  chi yetu Tanzania. Uzalendo uliochochewa kwa kiasi kikubwa na uwapo wa chama tawala CCM. Chama chenye nguvu na ushawishi kwa Watanzania wote. 

Ni nani anayeweza kusimama na kuthubutu kukisema chama hiki kuwa hakina mvuto, hali ya kuwa ndicho kinachosikilizwa kimtaje mtu wa kusimama kama mgombea urais?
Chama kilichokufa kitatoaje rais kila msimu wa uchaguzi? Hata wale wanaosema hayo, nao hukaa chini na kusema fulani anafaa, yule akisimama atasumbua na maneno nk. La kushangaza, wote wanaotajwa kwa mazuri au kwa mabaya wanatoka CCM?

Hii ni dalili ya wazi wazi kuwa mwenye uwezo wa kugombea urais wa Tanzania Bara na akaungwa mkono na Watanzania wote atatoka CCM na atakuwa rais wa Watanzania wote.
Kama hivi ndivyo, basi ni jukumu la CCM wenyewe kuhakikisha kwamba mtu anayeweza kupewa nafasi hiyo ya kugombea urais ni sahihi na pengine asilazimike kusafishwa na dodoki ili aonekane msafi kwa Watanzania wote.
Mungu ibariki Tanzania.
+255712053949

No comments:

Post a Comment