Pages

Pages

Monday, April 06, 2015

SIWEZI KVUMILIA:Uchaguzi huo, walau watapa jezi na mipira

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIFANYA utafiti kidogo tu namna vijana wanaojihusisha na mambo ya kimichezo wanavyoangaliwa, utabaini kuwa leo hii wameanza kuonekana umuhimu wao. Baadhi yao katika maeneo mbalimbali wameanza kupokea vijizawadi vya jezi au mipira.

Hata hivyo, vijana hao wameanza kupata zawadi hizo kwa sababu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Wanaotoa zawadi hizo wanasukumwa na dhamira zao za kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, iwe ni ubunge au udiwani.

Haya ni matatizo makubwa. Ni matatizo kwa sababu umuhimu wa vijana hao unaonekana kila mwaka wa uchaguzi. Ingawa tunatambua umuhimu wa michezo, lakini wadau wamekuwa kimya wakisubiria mwaka wa uchaguzi tu ndio wajitolee.

Hakika Siwezi kuvumilia kuona siasa zinapewa nafasi kila wakati hata kwa mambo yasiyostahili kutokana na umuhimu wake. Na wakati mwingine natamani kuwaambia vijana hao wasisumbuke na watu hao wanaojikosha katika mwaka wa uchaguzi.

Bali wajiweke mikakati ya kuona vipaji vyao vinawika hata kama asipotoa mpira mmoja au jezi mwanasiasa asiyekuwa na dhamira ya kukomboa vijana wanaokufa njaa licha ya kusheheni vipaji vya kucheza soka katika mikoa mbalimbali.

Hii inakera na kustaajabisha mno. Tanzania imebarikiwa kuwa na vijana wenye vipaji vya kila aina kama vile ngumi, riadha, mpira wa miguu na mingineyo. Hata hivyo hatuna mipango ya kuwaendeleza wenye vipaji hivyo. Tumeendelea kuwa wanasiasa.

Mtu anajiwekeza visenti vyake akijua fika anapotoa jezi seti mbili au tatu basi ataungwa mkono na makundi ya vijana. Hii haikubaliki. Na lazima wadau hao, wakiwamo hao wanasiasa kutafuta nafuu ya maisha kwa wanamichezo wao. Waweke mikakati endelevu kabla ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi ili faida zao zionekane dhahiri.

Tuacheni kufanya siasa hata pasipotakiwa. Lazima tufahamu michezo ni ajira. Makundi ya watu wasiokuwa na ajira wanaweza kuishi vyema kama wataibuliwa na kuendelezwa kutokana na vipaji vyao vya michezo, iwe ni riadha au mpira wa miguu.

Huo ndio ukweli. Ni wakati huu makundi hayo yakawa makini kupokea wanasiasa hao wanaoanza kuwaona leo kwa kuwapa jezi za bei rahisi ili wawachague na bada ya hapo huwakimbia kwa kipindi cha miaka mitano, huku wakiishi bila kujua kesho yao.

Badala yake watumie nguvu zao na maarifa yao kufanya mazoezi kwa bidii, pamoja na kutumia fursa zozote wazipatazo, ikiwamo kutafuta timu zenye dira ili waonyeshe vipaji vyao kwa ajili ya kuwakomboa kimaisha na kiuchumi.

Kinyume cha hapo, vijizawadi vya jezi au mpira vitaendelea kuwapatia maisha duni, maana licha ya kuwachagua watu hao, lakini wanashindwa walau kuanzisha ligi yenye thamani ya Sh 10 tu kwa mwaka ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na Ligi yenye nguvu na ushindani kwa ajili ya kuwapatia mwangaza makundi ya vijana wanaoamini soka au michezo ndio ajira zao.
Tuone wiki ijayo.

0712053949

No comments:

Post a Comment