Pages

Pages

Monday, March 23, 2015

SIWEZI KUVUMILIA:Mgambo ingecheza hivi mechi zote ingetwaa ubingwa

Na Kambi Mbwaana, Dar es Salaam
NAJUA kuifunga Simba au Yanga ni ujiko mkubwa. Kila mtu anafahamu hivyo, ndio maana timu ndogo zinapigwa kila mechi wanapokutana wenyewe, ila inapoingia uwanjani kucheza na Simba au Yanga, wanajikaza.

Wanajikaza kiasi kwamba mara kadhaa hushinda au wakishindwa wanalazimishwa sare na timu hizo kongwe na vigogo Tanzania Bara. Hii siwezi kuvumilia. 

Ukiacha matokeo ya mechi ya Yanga na Mgambo iliyochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Mkwakwani, jijni Tanga, Wagosi wa Kaya hao wanaotokea Kabuku, wilayani Handeni, walikuwa na pointi 24 na kushika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi ya Tanzania Bara.

Katika mechi yao na Simba, Mgambo waliweza kucheza soka safi na la kuvutia kiasi ambacho kiliwapatia ushind wa mabao 2-0. Matokeo hayo yalikuwa machungu kwa mashabiki wa Simba. Hii ni kwa sababu yaliwaweka katika nafasi mbaya kuelekea kutwaa ubingwa wa Bara.

Kama hivi ndivyo, naumiza kichwa kwanini Mgambo isiwe inacheza soka safi la kuvutia hata inapokutana na timu ndogo? Kwanini timu zote zisiwe zinacheza soka lao safi ili ligi izidi kuwa na msisimko?

Sio kama nimeumia kuona Mgambo wameshinda mbele ya Simba, ila ni kuchukizwa na mfumo wa soka letu kuona timu zinajikaza pale wanapokutana na timu kubwa za Simba na Yanga.

Timu kubwa au kongwe ni Simba na Yanga.Ni sawa na pointi 12 kama timu hiyo itashinda nyumbani na ugenini kwa mechi zote watakazokutana na wakongwe hao kwa msimu mmoja wa Ligi.

Hii ni kuonyesha kwamba matokeo hayo hayawezi kuipa ubingwa timu husika kwa kushinda mbele ya Simba na Yanga tu. Ni wazi timu hizi zinapaswa kupata mafunzo mazuri kutoka kwa makocha wao. Waonyeshe soka safi kwa timu zote ili  walau zikuze kiwango chao kama si kutwaa ubingwa wa Bara.

Lakini kufungwa ovyo na mwisho kujifariji na pointi tatu za Simba au Yanga ni kujiharibia tu, maana inaweza kuwa dalili mbaya za kudumaa au hata kushuka daraja. Huu ni ushauri tu. 

Ieleweke kuwa napenda maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania, huku nikiwa siamini kuwa kucheza mechi za wakongwe tu na kwingine kusua sua ni kujilemeza.

Huo ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia, maana ndio timu ndogo zifanye vizuri, lakini si kwa mechi za wakongwe tu. Kuna faida gani kumfunga Simba au Yanga na baadae timu inashuka daraja?

Au ndio kufungwa tunafungwa japo chenga twawala?
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949



No comments:

Post a Comment