Pages

Pages

Monday, February 02, 2015

TFF yamlilia bosi wa IRFA, John Ambwene wa mkoani Iringa

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA), John Ambwene Mwakalobo uliotokea jana (Februari 1 mwaka huu) mkoani Iringa baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura, ilisema kuwa msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Mwakalobo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa IRFA, kabla ya 2012 kushinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Alizaliwa Februari 4, 1954 na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Azania, Dar es Salaam na baadaye mafunzo ya ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Mpwapwa mkoani Dodoma. Alianzia kazi ya ualimu Newala mkoani Mtwara kabla ya kuhamia mkoani Iringa mwaka 1981. Alistaafu mwaka 2013.

TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho (Februari 3 mwaka huu) kwao Kyela mkoani Mbeya. Ameacha mke, watoto wanne na mjukuu mmoja. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

No comments:

Post a Comment