Pages

Pages

Monday, February 16, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: NSSF safi, sasa tutasonga mbele

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKA la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), limejitokeza katika sekta nyeti ya michezo kwa kushirikiana na Klabu ya Real Madrid kuanzisha kituo cha michezo nchini Tanzania. 
Meneja Kiongozi na Uhusiano wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume, pichani.
Katika kituo hicho cha michezo, NSSF shirika kubwa Tanzania lenye uwezo mkubwa na kushirikiana na jamii yake, litashirikiana pia na klabu ya Real Madrid ya Uhispania, huku mradi huo ukigharimu Sh bilioni 16.

Ujenzi huo utajumuisha viwanja vitano vya mpira wa miguu, mabweni ya wachezaji na wageni, maduka na huduma nyingine muhimu, ambapo pia watajenga uwanja wa gofu wenye mashimo 18 utakaoambatana na ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo la ekari 400 lililopo katika mji uliopangwa kuwa wa kisasa wa Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Hongera sana NSSF, ila wengine wapo wapi? Shirika hilo limefanya kitu ambacho kitakuwa na mguso na uwezo wa kuibua vipaji vya vijana wetu. Hii ni kwa sababu kwa miaka mingi Tanzania imeshindwa kufanya vizuri katika michezo, hususan mpira wa miguu.

Kushindwa huko kunatokana na kukosa mipango yenye tija. Tunakuwa na wachezaji ambao umri wao ni mkubwa. Nguvu zao nyingi zinaishia kwenye ligi za mchangani na wanapoingia Ligi Kuu wamechuja.

Na ndio  maana mara kadhaa wamekuwa na ndoto ya kuona kunakuwa na vituo vingi vya michezo, bila kusahau ligi za vijana nchini kote. Kila mmoja kwa nafasi yake akitimiza wajibu wake vizuri, maendeleo yatapatikana.

Na hilo la wadau kushindwa kubuni na kusimamia miradi mikubwa na midogo inayohusisha soka la michezo ya kuanzia umri mdogo ndio unaonifanya nishindwe kuvumilia. Hakika siwezi kuvumilia. Angalau sasa tunaweza kupata cha kujivunia, tukiamini kuwa mambo mengi yanayoanzishwa na NSSF Tanzania huwa na uhakika.

Ni jukumu la wadau wa michezo sasa kuona namna ya kuwaunga mkono NSSF juu ya program yao hiyo, huku mchakato wa upatikanaji wa watoto ukianza rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita, katika viwanja vya Karume, jijini Dar es Salaam.

Ni vyema sasa tukaweka mipango na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunavuna watoto wengi wanaoweza kufaidika kutokana na vipaji vyao vya michezo kwa kuwanoa kuanzia chini hadi juu, maana ndio njia nzuri ya kuwakwamua.

Kinyume cha hapo tutaendelea kuwa mashabiki wa wachezaji wa Kimataifa wanaowika duniani kote, hali ya kuwa tunao uwezo wa kuzalisha idadi kubwa ya vijana kutoka nchini Tanzania, kama tutakuwa na mipango kama waliyokuwa nayo NSSF.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949

No comments:

Post a Comment