Pages

Pages

Tuesday, February 17, 2015

Radio za Jamii zapewa somo

DSC_0219
Mshehereshaji kwenye madhimisho ya siku ya redio duniani, Bi. Usia Nkhoma Ledama akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.(Picha zote na Zainul Mzige.

Na Mwandishi wetu, Arusha
Vyombo vya habari hususan redio za jamii zimetakiwa kutanguliza uzalendo na kutetea maslahi ya taifa ili kuliepusha taifa katika migogoro na mitafaruku inayoweza kusababisha machafuko nchini hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha Nyerembe Munasa wakati wa kuadhimisha Siku ya Redio duniani iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na watangazaji wa redio za jamii na wadau mbalimbali wa habari nchini katika ufunguzi wa maadhimisho hayo Munasa alisema redio ina nguvu kubwa kuchambua na kutengeneza mustakabali wa taifa na hasa vijana iwapo itatumika vizuri badala ya kuwa chanzo cha matatizo na uchochezi mambo ambayo yanaweza kulisambaratisha taifa.

Amewataka waandishi na watangazaji wa redio jamii kuzingatia maadili ya kazi zao kwa lengo la kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania na kujenga taifa endelevu .
DSC_0255
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Nyerembe Munasa akizungumza katika ufunguzi wa kuadhimisha siku ya redio duniani iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.

“Mnatakiwa kutafiti, kutathmini na kupeleka taarifa zenye tija na kuhamasisha vijana kujituma kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa wimbi la umaskini kwa wananchi na hasa vijana, mkitekeleza wajibu wenu kwa kujua nini mnachofanya mtachochea mabadiliko kwa haraka katika jamii”.

Akizungumzia fursa zilizopo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru ametoa wito pia kwa vyombo vya habari hususani radio za jamii kuwawezesha vijana wa Kitanzania kutambua na kutumia fursa zilizopo za uchumi wa gesi na mafuta ili kujiondoa katika umaskini unaolalamikiwa kusababishwa na ukosefu wa kazi.

“Pamoja na utengenezaji wa vipindi vyenye kuelimisha jamii redio jamii lazima ziwajibike kibinafsi na kijamii hadi ngazi ya taifa kwa kuwapa vijana taarifa zilizosheheni fursa zilizopo na namna ya kuzifanyia kazi, ili vijana waondokane katika migogoro na maandamano yasiyokuwa na tija kwa sababu watakuwa wanajua nini cha kufanya ndani ya sheria na utengamano wa amani”.
DSC_0242
Amesema vyombo vya habari jamii iwapo vitatumia vyema Katika kuwashirikisha vijana vina uwezo na nguvu kubwa kubadilisha fikra za wananchi kwa kutengeneza vipindi ambavyo vitachochea mawazo endelevu kwa kuzingatia mila na utamaduni wa taifa la Mtanzania kuwakomboa vijana kuepukana na utamaduni tegemezi unaosababisha kulemaa kwa vijana kutafuta njia za mkato na kutopenda kufanya kazi jambo ambalo linasababisha mwendelezo wa umaskini nchini.
Akizungumza kwa wakilishi wa redio za jamii, waandishi na wadau wengine wa habari mjini hapa, Munasa alisema majukumu matatu ya utangazaji wa redio, yamekuwa hayafikiwi inavyotakiwa kutokana na wengi wa wahusika kutofahamu vyema majukumu yao au kutowajibika kikamilifu.
“Utakuta mwandishi wa habari hasa watangazaji anaingia studio hajajiandaa kwa kufanya utafiti wa somo linalozungumziwa, hana mwongozo wa kipindi (script), hana mpango kazi wa kipindi (programme matrix) na wala mlolongo wa uendeshaji wa kipindi kinapoanzia na kuishia, hili ni tatizo sio utangazaji!”
DSC_0223
Baadhi ya washiriki kutoka redio mbalimbali za jamii nchini wakimsikiliza mgeni rasmi wakati akifungua rasmi sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani.
Pamoja na kuwakumbusha watangazaji umuhimu wa kutangaza katika vyombo vya habari hususan redio mkuu huyo wa wilaya aliwataka washiriki kubadili mtazamo wa muziki kwa kupiga muziki wa asili kwa lengo la kupeleka ujumbe mzito na wenye manufaa kwa taifa badala ya muziki uliojaa mahadhi ya mapenzi na matusi.

“Muziki una nguvu kubwa katika maisha ya binadamu watangazaji lazima mfahamu na mjue namna ya kuupangilia kutokana na vipindi mnavyovitayarisha na muda wa aina ya muziki husika. Sio wakati wote ni wakati wa kusikiliza muziki wa mapenzi, kwa sababu redio husikilizwa na watu mbalimbali kwa sababu mbalimbali pia.”

Suala la mpangilio wa muziki, kuuelewa na thamani yake katika redio na umma lilielezwa kwa undani zaidi na nguli wa masuala ya muziki katika vyombo vya habari Masoud Masoud ambaye alisema kuwa watangazaji wa kisasa wamekuwa hawaelewi maana ya muziki na faida zake Katika kuendeleza taifa kitamaduni na kimaendeleo.
DSC_0012
“Vijana wengi wamekuwa wakitayarisha muziki wanaoupenda wao na sio unaopendwa na kufufaisha umma, wakati umefika kwa kutafuta mbinu au jitihada zozote za kuwafundisha muziki ni nini, unachezwa wakati gani na kwa manufaa ya nani.”

Sherehe hizo ambazo huandaliwa kila mwaka tarehe 13 Februari, ziliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na ujumbe wa mwaka huu ni “Nguvu ya Redio na Ushiriki wa Vijana katika Maendeleo”.

Ujumbe kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova katika kuadhimisha siku hiyo na kusomwa kwa niaba yake na mwakilishi wa UNESCO nchini Bokosha Spencer umesisitiza nguvu ya radio katika kujihusisha na masuala ya kijamii kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani .
DSC_0258
Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akifurahi jambo na baadhi ya washiriki kutoka redio mbalimbali za jamii wakati Mkuu wa Wilaya ya Arumeru akibariki ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya redio duniani yaliyofanyika jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
“Vijana wanawake na wanaume hawashirikishwi vema katika vyombo vya habari - hutengwa mara nyingi kunakoashiria kusahaulika kwa mapana yake katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kidemokrasia. Redio kama chombo cha mshikamano, kinachokuza elimu na utamaduni ushirikishwaji wa vijana ni muhimu”.
Bokova aliitaka jamii kuwasaidia vijana kwa kuwapa sauti kubwa zaidi na kujenga hisia ya jamii kwa njia ya usambazaji wa habari kwa kutayarisha na kusikiliza vipindi vya redio.
DSC_0007
Bw. Spencer Bokosha akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya redio duniani kwa niaba ya Mkuu wa ofisi ya Shirika la UNESCO, Tanzania Zulmira Rodriguez.
DSC_0061
Mwenyekiti wa mkutano wa sherehe maadhimisho ya siku ya redio duniani ambaye pia ni Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Allan Lawa akiendesha akitoa mada chokonozi ni kwa namna gani radio inaweza kutumika kama jukwaa la ushiriki kwa vijana katika mabadiliko ya kidemokrasia? Utafiti unaogusa Watanzania wakielekea katika uchaguzi mkuu.
DSC_0158
Mwandishi mkongwe na mkufunzi wa tasinia ya habari kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ayub Rioba akitoa mada Je uwekaji huru wa mawimbi ya radio kumesababisha mambo mabaya zaidi kuliko mazuri: Mitazamo na matarajio kuhusiana na ushiriki wa vijana wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani.
DSC_0147
Makamu Mwenyekiti wa mtandao wa redio za jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Meneja wa redio jamii Sengerema FM ya mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye, akiwasilisha mada inayohusu ushiriki wa vijana katika vipindi vya Redio, ambapo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Redio za jamii kuhakikisha zinawafikia watu wote kwenye jamii huku wakiwalenga vijana ambao ndio wana idadi kubwa ambayo inaweza kuchochea mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
DSC_0091
Meneja wa Redio Kahama FM, Marco Mipawa akichangia mada ya kuonesha nguvu za vijana na vyombo vya habari vya jamii pamoja na kujadili kanuni bora zilizojitokeza katika utekelezaji wakati sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.
DSC_0136
Mwandishi wa habari mkongwe, mzee Gervas Moshilo akitoa mada ya Uandishi wenye maadili na uwakilishi wa vijana kupitia vyombo vya habari wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani.
DSC_0054
Meza kuu ikifuatilia mada na michango mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na washiriki.
DSC_0183
Pichani juu na chini ni watangazaji wa redio za kijamii walioshiriki kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani wakichangia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye maadhimisho hayo.


No comments:

Post a Comment