Pages

Pages

Wednesday, February 11, 2015

MGODI UNAOTEMBEA:Vita ya urais, inawatoa akili wapambe

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania, inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu kwa nafasi mbalimbali. Ni katika Uchaguzi huo, Watanzania watapata fursa ya kuwachagua madiwani, wabunge na rais.
Bernard Membe, mmoja  wa makada wa CCM na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye anatajwa kuwa na ndoto ya kuwania urais baadaye mwaka huu.
Edward Lowassa, naye ni kada wa CCM ambaye pia Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, anayetajwa pia kuwa na ndoto ya kuwania urais baadaye mwaka huu.

Uchaguzi huo utafanyika Bara na Visiwani nao watachagua wawakilishi wao wanaoamini kuwa watakuwa na msaada nao kuhakikisha kwamba Zanzibar inapiga hatua.
Joto kali na msisimko wa aina yake umeshika kasi kutokana na uchaguzi huo. Mengi yanasemwa. Mengi yanasikika pia. Ieleweke kuwa, kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Yoyote anaweza kuwa mbunge au diwani kama sheria inavyosema katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, wale wenye sifa zilizotajwa kwenye urais, nao wana haki hiyo.

Hata hivyo lazima tufahamu urais si jambo dogo. Ni Mungu pekee anayebariki jambo hilo, ukizingatia kwamba ni nafasi moja inayoshikwa na mtu mmoja, iwe Tanzania au kwingineko kwenye utaratibu huo.

Tatizo si kugombea nafasi hiyo nyeti ya urais. Tatizo hawa wapambe wa urais wanaojitoa akili kwa kushabikia mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu, hususan kwa wakati huu.

Vita ya urais ipo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya wanachama wake wengi kutajwa au kuonyesha nia ya urais mwaka huu. Hadi sasa, wanachama zaidi ya nane wameonyesha nia ya kuwania urais badaye mwaka huu na kuibua joto na msigano wa hali ya juu.

Baadhi ya wanachama hao ni pamoja na Bernard Membe, Samuel Sitta, Dkt Asha-Rose Migiro, Steven Wassira, January Makamba, Khamis Kigwangwallah, Edward Lowassa, Lazaro Nyalandu na wengineo.

Si dhambi kuonyesha nia ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi, lakini ustaarabu unatakiwa ili kudhihirisha hekima yako, busara yako na namna gani ulivyojaliwa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti.

Sheria zifuatwe. Kwa mfano, wapo watu wanaotajwa kutumia fedha nyingi kushawishi  waungwe mkono katika vijiwe vya kahawa, pombe za kienyeji au katika nyumba za ibada.

Wale wanaotumia muda mwingi kufanya vikao vya kuungwa mkono bara na visiwani na kupewa majina ya ‘wapambe wa urais’. Jamii inajiuliza maswali mengi dhidi ya watu hao.

Ikulu kuna nini? Kwanini wahahe usiku na mchana sanjari na kutumia fedha nyingi bila kujua wanapozitoa ili tu watimize ndoto zao? Fedha hizo wamezipa majina mengi mazuri. Leo wanaziita sadaka, rambirambi, takrima au msaada katika mambo mbalimbali ili wasieleweke vibaya.

Ni fedha chafu kama fedha nyingine. Na zinatolewa na watu wachafu wenye nia chafu, ndio maana baadhi yao huona ni sahihi kusaka nafasi ya urais kwa kutumia fedha nyingi kuwanunua wapambe, wakitaka waimbiwe nyimbo nzuri ili waonekane umuhimu wao.

Watu hao hawana dhamira ya dhati ya kuwakomboa Watanzania. Wanataka waende Ikulu wakafanye biashara zao na kugawana vyeo wao na wapambe wao wanaotoka povu kuwasafisha mabwana wakubwa hawa wanaotaka Ikulu kwa udi na uvumba.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kulikemea suala hilo ma kusema Ikulu ni Mahala patakatifu. Utakatifu wa Ikulu ya Nyerere, unanajisiwa na hawa wasaka urais kwa fedha.

Tumeshuhudia kundi likijipambanua dhidi yaw engine, wakiona wao wana nafasi nzuri zaidi ya kupata nafasi ya kuingia Ikulu. Kujiamini huko kumetokana na kuamini wamefanikiwa kuwanunua watu  ambao pengine ndio wenye uwezo wa kuwapitisha katika vikao vya CCM.

Wanahangaika mchana na usiku kuwawekea mabwana wakubwa wao mazingira mazuri, bila kujua kwamba hawapo sahihi. Muda wa  uchaguzi bado, kampeni za mapema za nini.

Anapojitokeza mtu hadharani kuanza kumpigia kampeni mtu ni jambo linaloibua maswali mengi na kuhoji uhalali wao na shauku hiyo ya urais. Wiki iliyopita, tulishuhudia baadhi ya wabunge kusimama hadharani mjini Dodoma kwa ajili ya kumpigia debe Lowassa.

Wabunge kama vile Stephen Ngonyani Profesa (Maji Marefu), John Komba, Mary Chatanda na wengineo walijitoa akili kwa kumsafisha Lowassa na kumtaka agombee urais kwa madai Watanzania wana imani naye.

Wabunge hawa wana uhakika gani kama Watanzania wote wana imani na Lowassa? Na walitumwa waseme hilo hadharani ili waandishi waone na kuandika kwenye vyombo vyao?

Basi bora CCM iruhusu kampeni kuliko kuachia vitendo hivi hadharani vikiendelezwa na upande mmoja, maana unawanyima haki wengine katika mchakato huo wa urais.

Najiulizaa tu, kwani muda wa kampeni umefika? Kwani hawa wabunge na wapambe wote wa urais hawajui wakati bado? Hizi ni rafu na zinatakiwa ziangaliwe upya ili kulinda heshima ya chama.

Wana CCM wote, wabunge, madiwani na viongozi wa serikali wanapaswa kuisimamia ilani ya  Uchaguzi wa chama chao kuwapatia maendeleo Watanzania, kuliko kuelemea kwenye kampeni za mapema za urais.

Majimbo yao yamekuwa na changamoto nyingi na pengine wapiga kura wao wamekata tamaa na maisha. Badala ya kubuni, kusimamia miradi ya maendeeleo, wapo ‘busy’ kuwanadi wasaka urais kinyume cha sheria na maadili ya CCM.

Hivi wabunge hawa na wapambe wengine wa Lowassa hawajui kama ni makosa kufanya kampeni mapema? Wasubiri muda ufike ili wajinafasi. Ikumbukwe Lowassa ni kati ya makada wa CCM walioadhibiwa kwa rafu za mbio za kumrithi Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Pamoja na kuadhibiwa huko, bado wapambe wanajitoa akili. Wanaona wanayo haki kuliko wengine. Najiuliza tu, hivi kila mmoja akisimama kumpigia debe mgombea wake wakati huu serikali itafanya kazi?

Lowassa asimame, Membe ashangiliwe na Makamba hali kazalka. Basi hii itakuwa nchi ya vituko isiyoheshimu taratibu zake ilizojiwekea ili kuepusha mikanganyiko kwa mambo nyeti kama urais.

Wakati nasema haya, nakumbuka namna gani nchi iliyumba kabla ya makada hao wa CCM kuadhibiwa. Walipishana makanisani, misikitini na katika vijiwe vya bodaboda, wakijificha kwenye kivuli cha kusaidia jamii. Fedha nyingi zilitolewa na baadhi yao kwa kivuli cha misaada.

Viongozi wa CCM wakawatia hatiani na kuwapunguza makali yao. Je, wangapi wamepunguza kasi baada ya adhabu hiyo? Na wanaoendelea ndio kusema wapo juu ya sheria kuliko wote?

Ni wakati wa wapambe hao wa urais kujitathimini upya. Wajiangalie mara mbilimbili juu ya mambo wafanyayo? Si kweli kama Watanzania wote wanaamini wanachotaka wapambe hao.

Wapunguze joto na haraka. Wasubiri muda wa kutangaza nia ufike na kupitishwa pia na chama chao ili wawanadi vizuri.

Hata wakitaka kuwabeba mgongoni ruhusa. Wakitaka kuwafuta viatu au kuwabebea mikoba yao pia hawatakatazwa. Si wakati huu.

Haraka hizi ndio zinazosababisha baadhi ya vitendo viovu, matusi, kejeli na chuki kwa baaadhi ya makundi hayo ya urais. Baadhi yao wamekosa busara na uvumilivu katika suala hilo.

Fuatilia vyombo vya habari bila kusahau mitandao ya kijamii. Hali ni mbaya na yapo makundi yanayofanya kampeni za wazi kabisa. Nyimbo za wagombea zinatungwa na kusambazwa kwa nguvu zote.

Hizo si kampeni, zinaitwaje. Hizo si rushwa nguvu hizi zinatoka wapi na faida yake ni nini? Wasanii wanaokwenda studio kurekodi nyimbo za mapambio kabla ya muda wanapata wapi pesa? Na kama wanatoa wenyewe kwa mapenzi yao, mara ngapi wamekemewa?

Ifikie wakati tuwe na subira na uvumilivu. Hili litajenga heshima ya CCM na Taifa kwa ujumla katika kutafutwa mrithi wa JK, rais anayemaliza muda wake baadaye mwaka huu.

Purukushani hizo zinaangaliwa na watu wote, wakiwamo wapinzani wanaosubiri kuona nani anasimamishwa na CCM katika urais mwaka huu. Wanataka kuona na kujipanga pia. Huenda wanatumia muda huo kujiridhisha juu ya wanaotajwa na mapungufu yao ili wawabane kirahisi, hususan atakapoteuliwa mtu mchafu na asiyekuwa na mvuto.

Sina shaka na wanaotaka urais Tanzania. Shaka yangu ni vitendo viovu vilivyoshika kasi vya kufanya kampeni mapema. Ni mwanzo wa kuingiza choko choko endapo baadhi watamwagwa kwa kufanya kampeni mapema.

Hawa hawa wapambe waliojitoa akili watasimama hadharani kupinga uamuzi huo na kuibua migogoro,  wakati wanajua sheria na miiko yote, wakiwamo viongozi wa chama wanaotumika pia katika harakati hizi.

Ya nini haraka? Tusubiri muda ukifike na kuamua hatma ya nchi yetu, huku tukiomba apatikane mtu bora na mwenye maadili, bila kusahau ndoto za kuliletea maendeleo Taifa letu.

Mungu atamuinua Mtanzania mmoja kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo kwa CCM na kuungana na wengine wa upinzani ili kumpata rais wetu mpya.

Atakuwa ni chaguo la Watanzania wote. Si kama hivi inavyoaminishwa na wapambe kila uchao. Wayafanyayo yapo kwa maslahi yao si ya Watanzania wote. Katika harakati hizo, wajisemee wao na si Watanzania wote.

Mwisho natoa rai kwa CCM juu ya kuwamulika wapambe au wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi za udiwani, ubunge na urais kuhakikisha wanafuata sheria za chama chao.

Wasubiri mchakato huo ufunguliwe rasmi. Wasijitoe akili kwa kufanya kampeni kabla ya muda. Watakaobainika, majina yao yatupwe bila kuangalia wangapi watalia au watacheka. Hili litakiletea chama heshima na kudhihirisha ukongwe wake na kisima cha kupika viongozi wenye maadili.
+255712053949

No comments:

Post a Comment