Pages

Pages

Wednesday, February 04, 2015

Makala:Unafuu wa ada Twayyibat Sekondari wamkuna DC Temeke

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ILI elimu ya Tanzania izidi kukua kunahitajika kuwa na shule nyingi za serikali na zile za binafsi zinazomilikiwa pia na taasisi za kidini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Mkuu wa wilaya Temeke, Sofia Mjema, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Kiislamu, Twayyibat, iliyopo Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Kuwapo kwa shule hizo kutazidi kuongeza idadi kubwa ya watoto wanaopata elimu ya msingi, sekondari na vyuo Vikuu kwa ajili ya kujikomboa katika maisha yao.

Ukiacha mikoani ambako hakuna shule nyingi hususan maeneo ya vijijini, jijini Dar es Salaam kumefanikiwa kuwa na shule nyingi mno, zikiwamo za serikali na mashirika.

Zipo shule za kidini ambazo wakati wote zimekuwa zikifundisha watoto elimu ya Dunia na ile ya kufahamu Mungu ni nani, nazumgumzia pale watoto wanapofundishwa kisawa sawa na kukolea kiimani kama njia ya kumjua Mungu na kutenda matendo ya kiungwana.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, alitembelea katika shule ya Twayyibat Islamic Seminary, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.

DC Sofia alitumia muda huo kuikagua shule hiyo pamoja na kuzungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi wa shule hiyo kwa ajili ya kuona inakuwa kati ya shule bora wilayani Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo yaliyomkosha DC Sofia ni pale alipoambiwa kuwa ada ya shule hiyo kwa mwaka mmoja ni Sh 200,000 tu, jambo ambalo ni agharabu kuliona wala kulikisia katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Akizungumza shuleni hapo, Mkuu huyo wa wilaya ya Temeke, Sofia, anasema kwamba ameshangazwa na kuwapo kwa ada nafuu katika shule ya Twayyibat.

“Hili bado linanifanya nijiulize urahisi wa ada hizi wakati najua fika siku hizi elimu ni ghari na kuna mambo mengi yanayohitajika ili shule ziweze kujiendesha, ikiwamo mishahara ya walimu.

“Katika hili linanifanya nione serikali hususan Halmashauri ya wilaya ya Temeke inakaa na viongozi wa shule hii kutatua changamoto zinazowezekana kwakuwa kwa ada hizi shule haiwezi kujiendeshaa vizuri na kusonga mbele,” alisema.

DC huyo anasema urahisi wa ada hizo katika shule ya Twayyibat sit u utawafanya wazazi na walezi wamudu kusomesha watoto wao, bali pia kukuza kiwango cha elimu cha Temeke na Tanzania kwa ujumla.

Anasema amefurahishwa na mazingira ya shule hiyo, ingawa hajaona maabara, jambo alilojibiwa na uongozi wa shule kuwa tayari wameshatenga eneo la kujenga maabara kwa ajili ya shule hiyo ya sekondari ya Kiislamu.

“Maabara ni muhimu mno, fanyeni kila liwezekanalo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inakuwapo, maana kama tungewasiliana kwa karibu na Halmashauri yetu ni wazi tungeangalia namna ya kusaidia katika hilo ukizingatia kuwa shule inatoa huduma na ada zake ni nafuu.

“Tukitoka hapa tutafute namna bora ya kuhakikisha kuwa shule hii inakuwa bora, kwakuwa nimeshaona misingi na dhamira ya kweli kutoka kwa walimu, wadau, viongozi na wanafunzi kwa ujumla ili kuwapa mwanga zaidi, alisema.

DC Sofia aliwasili shuleni hapo saa 7 mchana, huku akipokewa kwa shangwe na wanafunzi wa shule hiyo, wadau wa elimu na wahisani wa shule hiyo, bila kusahau walimu waliokuwa na shauku ya kumpokea mgeni huyo tangu asubuhi.

Baada ya kuingia na kusaini kitabu cha wageni, alianza kutembezwa katika eneo lote la shule hiyo na kujionea hali ya kielimu inavyoendelea na namna wanavyofanya kazi zao.

Akizungumzia hali yaa utendaji kazi na uwajibikaji kwa walimu hao, DC Sofia aliwataka walimu kuongeza bidii ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanafanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne.

Anasema shule ina matokeo ya kuridhisha kutokana na wanafunzi wao kujisomea vizuri, wakiamini kuwa ni elimu pekee ndiyo inayoweza kuwakomboa katika maisha yao.

“Nashauri wanafunzi waelimishwe zaidi umuhimu wa kujisomea ili waachane na mambo ya Kidunia wakiwa bado wadogo kwakuwa wataharibu maisha yao.

“Mambo ya anasa na starehe zisizokuwa na tija zimepitwa na wakati kwakuwa wanaweza kuharibu kabisa mfumo wao wa maisha na kujiweka katika kundi la majuto,” alisema.
Aidha DC huyo alitumia muda huo kuwapongeza wahisani na wadau mbalimbali wanaoiwezesha hiyo yenye maskani yake wilayani Temeke, karibu na Msikiti wa Tungi.

Pia aliwakabidhi wahisani hao vyeti vya kutambua mchango wao kutokana na mara kwa mara kujitolea misaada mbalimbali inayochangia maendeleo ya kielimu kwa shule hiyo.

Baadhi ya wahisani waliokabidhiwa vyeti hivyo ni pamoja na Adam Malima, Skywards Construction, Shaimar Kweigir, Zainabu Vullu, Yakubu Chamber&Associate, Alosco, Home Shooping Centre, ambapo baadhi yao waliwakilishwa kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kiserikali.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Juma Omari, anasema shule yao imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kutoa ufaulu wa kufurahisha, huku akiihakikishia serikali kuwa watajitahidi kuwapa mwanga wa kielimu watoto wanaosoma Twayyibat.

“Tangu shule hii ilipoanzishwa mwaka 1996 imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na matokeo yake ya Taifa, hili linatufanya tuongeze bidii katika kufundisha wanafunzi wetu tukiamini ndio mpango sahihi.

“Sisi kama walimu tumekuwa tukiongeza bidii katika ufundishaji kwa ajili ya kuhakikisha kuwa shule yetu inakuwa bora kati ya nyingine, huku tukiamini kuwa kwa pamoja tutakuwa tunazifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazotukabili,” alisema.

Mkuu huyo wa shule aliwataka wazazi na walezi kuacha sababu, maanaa shule yao inafikika kiurahisi na imeamua kutoza ada nafuu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata haki ya kupata elimu.

No comments:

Post a Comment