Pages

Pages

Friday, November 28, 2014

Migogoro ya ardhi, mipaka ni tishio wilayani Handeni

Na Mwandishi Wetu, Handeni 
SERIKALI Kuu kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni na Mkoa mzima wa Tanga, wameombwa kuingilia kati mgogoro mzito wa ardhi katika kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, ili kuepusha hatari inayoweza kutokea, ikiwamo vita ya wenyewe kwa wenyewe.


Hayo yamesemwa juzi na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano ulioandaliwa na taasisi ya Handeni Kwetu Foundation inayofanya ziara katika maeneo mbalimbali, hususan ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, baada ya kuzinduliwa Mei 8 mwaka huu.


Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, wananchi hao walisema kuwa hali ni mbaya, maana kijiji chao kimeendelea kutekwa na kubaki eneo dogo lililoanza kuibua chuki za wazi kwa wananchi.


Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Alhaj Ally Yasin Ling’ande, alisema kiuhalisia hakuna kijiji cha Komsala, kwakuwa hawana eneo la ardhi, hasa baada ya wilaya Korogwe kuingia kwenye eneo lao kwa kufikia hata kujenga mnada wa ng’ombe.


“Ukiaangalia usawa palipojengwa mnada, utaamini kuwa hata kwenye shule ya Msingi Komsala pia patakuwa ni eneo la Korogwe, ingawa si sahihi kulinganaa na ramani ya mwaka 1978, jambo linaloonyesha kuwa huu ni mzozo utakaoweza kumwaga damu,” alisema.


Naye William Seif alisema mbali na mipaka hiyo kuwa tata, pia kumekuwa na idadi kubwa ya wageni kumiliki heka zaidi ya 130 na bado wanaingia kwa wenye heka tatu wakiamini kuwa uwezo wao kifedha unawafanya wamudu kesi zinazoendeshwa kwenye mabaraza ya Kata na wao kupata haki.


“Masikini akionewa anakimbilia kwenye Bazara la Kata, lakini huko kumekuwa na danadana nyingi, ukizingatia kuwa siku zote mkono mtupu haulambwi, ndio maana tunaoimba serikali ya wilaya ya Handeni, mkoa na wadau wengine wa ardhi kuja kujionea bomu hili linalosubiriwa kuripuka hapa kwetu,” alisema.


Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bashiri Wabu, alisema kuwa ardhi katika kijiji chao imeuzwa kiholela kwa watu wenye nazo bila kufuata sheria za ardhi, ikiwamo ya kuandaa mkutano wa wananchi wote.


“Kuna watu hawana maeneo kabisa ya kulima, wakati watu wachache wanamiliki maeneo makubwa ambayo hata kuyalima yote hawana uwezo huo, jambo linalokera na kuudhi mno kila tunapoliangalia suala hili katika kijiji chetu,” alisema Wabu, akiungwa mkono pia na Hemed Ngona, Kombo Twaha, wakisisitiza kuwa sheria za ardhi na utawala bora hazifuatwi katika kijiji chao.


Katika mkutano huo ulioanza saa 9 alasiri na kumalizika saa 12 jioni, ulihudhuriwa na watu wengi, huku idadi kubwa ikiegemea katika kero ya ardhi na mipaka.


Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Komsala anayemaliza muda wake, Mwanaidi Said, alisema kero kubwa katika kijiji hicho ni mipaka iliyoshindwa kutatuliwa na viongozi wa juu, licha ya kupeleka malalamiko yao mara kadhaa.


“Kijiji cha Komsala sasa ni kama kitongoji tu, maana kimechotwa katika pembe zote na ndio maana hata wenzetu wa Korogwe wamekuja kujenga mnada wa ng’ombe kwa madai kuwa ni kwao, jambo ambalo hata mwenyekiti atakayefuata litamuumiza kichwa,” alisema na kuwafanya wananchi wapatwe na hofu.


Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo aliyetumia muda huo kuaga wananchi wake, sekeseke la mipaka limeshindwa kutatuliwa, huku akiwataka viongozi kulipa kipaumbele kabla ya matatizo hayajakikumba kijiji chao pale wananchi hao watakapotafuta haki yao.


Naye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, aliwashukuru viongozi wa serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa kuwapa ushirikiano, ikiwamo kuruhusu kutembelea katika vijiji mbalimbali kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha utawala bora.


“Naomba niwatoe hofu Watanzania wote kuwa mikutano hii ya hadhara hairatibiwi na chama chochote cha siasa, hivyo tunaomba tushirikiane kwa ajili ya kufanikisha maendeleo, hasa kama wananchi watahudhuria mikutano wanapoitwa na viongozi wao,” alisema.


Ziara ya Handeni Kwetu Foundation ilianzia Kata ya Misima, ambapo wananchi wengi wameiunga mkono taasisi hiyo yenye lengo la kuwakomboa wananchi kwa kutoa elimu na kuhamasisha maendeleo ya jamii.





No comments:

Post a Comment