Pages

Pages

Tuesday, July 08, 2014

Aveva usisahau vipaumbele vyako Simba



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JUNI 29 mwaka huu, wanachama lukuki wa klabu ya soka ya Simba, walijitokeza katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oystarbay kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wapya. 

Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, pichani, akizungumza na waandishi wa habari, hawapo pichani, katika moja ya matukio ya kuelekea kwenye nafasi hiyo.

Hii ni baada ya uongozi wa mwenyekiti wao Ismail Aden Rage, kufikia tamati hiyo, ambapo wanachama hao kwa ridhaa yao wakaamua kumchagua kwa kishindo Evans Aveva kuwa Rais wa klabu ya Simba kwa kipindi cha miaka minne ijayo. 

Ulikuwa ni uchaguzi huru na wa haki, ijapokuwa kulikuwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ile ya kuwahimili wanachama wengi waliojitokeza katika uchaguzi huo. 

Katika uchaguzi huo, mbali na Aveva kuchaguliwa kuwa Rais wa Simba, pia alichaguliwa Geofrey Kaburu kuwa Makamu wa Rais, huku Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ikienda kwa Jasmin Costar, Collin Frish, Said Tully, Idd Kajuna Ally Suru, hivyo kuingia katika kapu la uongozi mpya wa klabu ya Simba. 

Hata hivyo si nia kuwataja nani ameshinda au yupi ameshindwa, ila ni kuangalia vipaumbele kadhaa ambavyo wagombea wengi walisikika wakivizungumzia, akiwamo Rais Aveva, Makamu wake Kaburu na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. 

Wagombea hao walisema hayo kwasababu walijua ndio karata yao ya kuwafanya wanachama wao wawaunge mkono kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa lengo ni kuona Simba inasonga mbele na kufikia ngazi za Kimataifa. 

SOKA LA VIJANA 

Hakuna hata mgombea mmoja aliyezungumza na wanachama bila kugusia soka la vijana. Wagombea hao akiwamo rais Aveva alitumia muda mwingi kusisitiza suala hilo.
Kila alikopita wakati wa kampeni zake alionyesha shauku ya kusimamia soka la vijana ili klabu iwe na wachezaji imara. 

Alisema hayo huku akiamini kuwa, hata vijana wanaowika kwa sasa ndani ya Simba, yeye ndio muanzilishi wa programu hizo za kuibua soka la vijana, baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, chini ya utawala wa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, wakati huo ni Hassan Dalali.

 Kamati hiyo ilifanya harakati nyingi na kufanikiwa kuweka mipango kamili, hivyo kuibukia vijana shupavu, akiwamo Jonas Mkude, Ramadhan Singano, ambao leo ni vinara wa kucheza soka la ushindani ndani ya uwanja. 

Hivyo alivyokuwa anazungumzia hili, hapana shaka Aveva alikuwa anajua anachozungumza kwasababu ndio eneo sahihi la kuwekeza ndani ya Simba. 

Klabu ikiwa na wachezaji vijana, itakuwa na eneo la kuwasajili hao badala ya kukimbilia nyota wa nje ambao si tu wana gharama kubwa, bali pia hawakidhi kiu ya kuitumikia Simba.
Wengi wao kiwango chao hakina tofauti na wa Tanzania, hasa kulingana na soka lenyewe la Afrika Mashariki. 

Hivyo ni wakati wa Aveva kukaa na kutafakari ahadi zake, vipaumbele vyake vya kuendeleza soka la vijana kwa vitendo na si kuacha kama ilivyo.
Akisahau hilo, kila mwanachama wa Simba amkumbushe kwa namna nzuri kwa ajili ya mafanikio ya klabu ya Simba. 

Kwa bahati nzuri, hata Wajumbe wa Kamati ya Utendaji nao walisikika sana wakikazia suala hilo la soka la vijana kwasababu ndio msingi wa klabu imara duniani kote. 

KUONGEZA WANACHAMA WAPYA

 Aveva pia katika kampeni zake alisikika mara kadhaa akipania kuwaunganisha wanachama wa klabu ya Simba na kuwaongeza wapya. 

Alisema katika kipindi cha uongozi wake, atajitahidi kuunda timu imara ya ushindi, ili iwe njia nzuri ya wadau na mashabiki kuchukua kadi za uanachama. 

Alisema hivyo huku akijua fika klabu ya simba imeegemea sana jijini Dar es Salaam. Hakuna mipango yoyote ya kuona walau wanachama wa mikoani nao wanatambulika na kuheshimika. 

Tuliona kwenye uchaguzi huu. Baadhi yao walijinyima ili waje kwenye uchaguzi huo. Wapo waliotoka mkoani Kigoma, Tabora, Lindi, Mtwara na maeneo mengine. 

Hivyo basi ni sahihi kwa kauli na mlengo wa Aveva kutaka kuwaunganisha hawa na kuwavuta wengine. Kuwa na wanachama wengi zaidi ni jambo la msingi. 

Wanachama hao wakiongezeka wengi klabu itazidi kuwa na nguvu ya kiuongozi na msaada mkubwa kwa timu husika. Timu inapokwenda mikoani itaamini inao walinzi na wapiganaji si wa kukaa getini, bali kusaidia baadhi ya mahitaji muhimu.

 Lengo la kuifikisha klabu ya Simba kuwa na wanachama wasiopungua elfu 50000 ni sahihi na hapana shaka Aveva lazima aweke mipango imara kufanikisha suala hilo maana ni sehemu ya mafanikio makubwa kwa klabu yao. 

UWANJA WAO BUNJU 

Kwa kipindi cha miaka 7 sasa kumekuwa na wimbo mtamu wa uwanja. Wimbo huu uliimbwa sana enzi za utawala wa Dalali. 

Hapana shaka Dalali alijitahidi, maana yeye aliweza kutafuta eneo kubwa na zuri la kujenga uwanja wao Bunju. Baada ya kupatikana eneo hilo, ndipo wimbo wa kujengwa ulipoanza.
Uliimbwa sana, kiasi kwamba baadhi yao walianza kuuchoka kuusikiliza masikioni mwao. Wakati wa kuelekea mwishoni mwa utawala wake, rage kama mwenyekiti wa Simba alitangaza siku 90 za operesheni ujenzi wa uwanja.

Sijui kinachoendelea kwa sasa, maana hata na mimi nikisema nitaendelea kuimba wimbo huo, wakati inajulikana waziwazi hakuna uwanja wa kisasa wa mpira unaojengwa kwa siku 90.

Kushikilia msimamo huo kunahitaji moyo wa chuma na pengine kujivunjia heshima mtaani pale unapomwambia mtu uwanja huo utajengwa kwa siku 90.
Kwa bahati mbaya siku hazigandi. Siku 90 zimekwisha na uongozi mpya umeingia madarakani. 

Wakati wa kampeni zake, Aveva aligusia suala la Uwanja wa kisasa wa Simba, Bunju. Ieleweke kwamba; suala la uwanja wa kisasa wa Simba ni muhimu kuliko kitu chochote.
Na inao uwezo wa kuujenga uwanja huo bila usumbufu wowote kulingana na rasilimali watu iliyokuwa nayo. Watu wengi wanaipenda Simba. Imeanzishwa mwaka 1936.
Kama hivyo ndivyo, ni aibu kubwa kuona hadi leo haina uwanja wa kisasa na kupitwa na timu ngeni ya Azam Fc. 

Nikisema hili, watu watashangaa! Wengine wanasema kuifananisha Simba na Azam inayomilikiwa na Bilionea Said Salim Bakheressa si sahihi. Hapana.
Wanaosema hivyo wanakosea. Maana hata Bakheressa mwenyewe anatamani kuwa na mashabiki na wanachama kama wa Simba au Yanga. 

Kuwa na wanachama wengi ni mtaji tosha. Hata ukiuza maji ya kunywa ukiyaandika Simba Sport Club, sidhani kama yale ya Bakheressa yatapata soko. Watu wana mapenzi na timu zao. 

Hivyo basi ni vyema Aveva akashikilia msimamo wake wa kutafakari namna ya kuujenga uwanja wa Simba kwa maendeleo ya klabu.
Kuwa na uwanja ni kuondoa gharama zinazoweza kuzuilika. Timu itafanya mazoezi kwenye uwanja wake na itacheza mechi zake za ndani kwenye uwanja wake nyumbani.
Gharama na makato mengi hayatakuwapo. Simba itaendelea na kupiga hatua kubwa. Itaonyesha kujitambua na kusaka njia ya mafanikio makubwa.

Hivyo suala la uwanja ni muhimu na linapaswa kushikiliwa kama alivyofanya Aveva kwenye kampeni zake wakati anaomba ridhaa ya kuongoza ndani ya klabu ya Simba. 

TIMU IMARA 

Katika kampeni za uchaguzi wa Simba, kuliibuka neno la eda. Kwamba enzi za utawala wa Rage wanachama na mashabiki wa Simba walikuwa wamewekwa eda.
Kwamba hawakuwa na furaha. Hii ni kwasababu timu yao haikuwa imara na ilikuwa inafungwa ovyo ovyo. 

Jambo hilo liliwafanya wapate hofu ya kufika uwanjani kushuhudia sare au kufungwa. Na ndio maana walishika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi.
Kwa mujibu wa Aveva na benchi lake la kampeni, chini ya Dalali ilikuwa ni aibu kubwa, hivyo jambo hilo linahitaji mkazo. Kuwa na timu imara iliyoandaliwa vyema. 

Kuwa na timu inayoweza kutafuta ushindi ndani ya uwanja. Kuwa na timu inayotoa furaha kwa mashabiki wake na si kuwatia simanzi na kuwarudisha tena kwenye eda ya miaka minne iliyopita. Inajulikana kama kufungwa, kushinda na kutoka sare ni sehemu ya mchezo.
Lakini kwa timu hizi kongwe zinaamini ushindi tu. Hivyo kwa kiongozi kama Aveva akaingia katika kasumba hiyo na kuitangaza vita dhidi ya timu nyingine.
Hata hivyo si dhambi. Malengo na mipango ya kuendeleza jambo zuri ndiyo inayotakiwa wakati wote. 

Ndio maana aliwaambia wanachama wake kuwa wajiandaye kupata shangwe za aina yake na klabu yake itafanya maajabu makubwa msimu ujao wa Ligi ya Tanzania Bara. 

USAJILI MZURI 

Suala la usajili mzuri pia lilizungumzwa sana na wagombea, akiwamo Aveva. Ifahamike kwamba kwa nyakati kadhaa Aveva amekuwa kwenye kitengo cha usajili ndani ya klabu ya Simba. 

Kwanza alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili enzi za Dalali, pia anajua kinachoendelea kwasababu mara nyingi usajili wa Simba unafanyika katika himaya ya marafiki wa Simba, Friends Of Simba, ambapo kwa sasa mwenyekiti wake ni Zacharia Hans Pope.
Hivyo mipango ya usajili makini itasababisha maendeleo ya Simba. Mara kadhaa Simba imekuwa ikifanya usajili wa presha.

Usajili usiokuwa na faida. Usajili unaogemea sana nyota wa kulipwa wakati uwezo wao mara kadhaa hauna tofauti na nyota wa Tanzania, kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Kelvin Yondan na wengineo. 

Si kila mchezaji wa Kimataifa anafaa kucheza soka Tanzania. Hii ikiangaliwa upya itasababisha matunda makubwa kwa Simba.
Lazima mkakati wa usajili ufanywe kwa kuangalia mahitaji husika. Kwa bahati nzuri Tanzania ina wachezaji wengi wazuri na wanaofaa kucheza soka la kimataifa. 

ANGA ZA KIMATAIFA 

Katika hatua nyingine, kipaumbele kingine kilichozungumzwa sana na Aveva ni kuona Simba inawika Kimataifa. Hili litafanikiwa kama sera na mipango imara itawekwa kuanzia chini hadi juu. Kwanza kuwe na timu imara ya ushindi.

Baada ya hapo watatwaa ubingwa wa ndani kisha waonyeshe maajabu walau kama ya mwaka 2002 ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa kurudi tena kwenye ligi hiyo, timu itawika Kimataifa. 

Kwa bahati nzuri Simba inajulikana na kuheshimika katika michuano ya Kimataifa. Timu ngumu za Misri, kama vile Ismailia, zamalek zina kumbukumbu nzuri dhidi ya Simba SC.
Simba ambayo kwa miaka minne hii ilionekana kuwa nyanya kiasi cha kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi, ikiachwa nyuma na Mbeya City, Yanga na Azam fc waliotwaa ubingwa wa Tanzania Bara. 

Hivyo ni jukumu la Aveva na watu wake kurekebisha baadhi ya mambo kwa maendeleo ya klabu ya Simba. Kila walichosema kwenye kampeni zao walau kionekane kinafanyiwa kazi kwa vitendo. 

Huu ni wakati wa kuwa timu imara. Huu ni wakati wa kuona nchi yetu inatangazwa kimataifa kwa kupitia mpira wa miguu ambao duniani kote hutumiwa kama kichocheo cha maendeleo.
Mwisho kabisa wadau wote wa Simba bila kusahau wanachama wao kuwaunga mkono viongozi wao ili wafikie malengo yao. Kusubiri mechi moja au mbili timu ifungwe kisha kuanza migogoro si kitendo cha kiungwana hata kidogo.
 +255712053949

No comments:

Post a Comment