Pages

Pages

Saturday, June 28, 2014

Timu ya Kurugenzi ya Mufindi yajipanga


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaaam

TIMU ya soka ya Kurugenzi Mufindi iliyopo Ligi Daraja la Kwanza, imejipanga vilivyo kuhakikisha inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2015/16.

Meneja wa timu hiyo, Athuman Kihamia ambaye ni Mweka Hazina wa Halmashauri wa Wilaya ya Mufundi, ameliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa wameunda uongozi mpya ili kufanikisha azma ya hiyo.

Alisema kuwa viongozi hao ni watumishi wa Halmashauri hiyo ya Wilaya Mufindi, wamiliki wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilipambana vilivyo, lakini ilishindwa kupanda daraja kutokana na sababu mbalimbali.

“Viongozi wote wametoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufundi kwa sababu ndiyo inayoigharamia timu kwa kila kitu, lakini tutaunganana viongozi wengine wawili, Mweka Hazina na Katibu Msaidizi watakaopendekezwa na Chama cha Soka Wilaya ya Mufundi,” 
alisema Kihamia ambaye ni mmoja wa wadau maarufu wa soka jijini Dar es Salaam, kwa sasa akiwa ni mtumishi wa halmashauri hiyo.

Kihamia alisema uamuzi huo wa kuunda uongozi mpya, ulifikiwa katika kikao chao cha Juni 17, mwaka huu ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Paul Ntinika, amepania kuifikisha mbali timu hiyo, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi-kuendeleza michezo kwa vijana kama sehemu ya kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini.

Aliwataja viongozi wapya wa timu hiyo na nafasi zao kwenye mabano kuwa ni Ofisa Utumishi na Utawala Monica Andrew (Mwenyekiti), Mhandisi Ujenzi Peter Mawere (Makamu Mwenyekiti), Ofisa Mipango Miji Bernard Kajembe (Katibu Mkuu) na Mweka Hazina Athuman Kihamia (Meneja).

“Mwenyekiti Monica amechaguliwa kutokana na uzoefu wake katika soka kwani ni mmoja wa waasisi wa timu ya Mbeya City inayotesa Ligi Kuu kwa sasa,” alisema Kihamia na kusisitiza kuwa watafanya usajili wa nguvu kufanikisha azma yao ya kuifanya Mufindi kuwa na timu Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment