Pages

Pages

Wednesday, June 11, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Nilikuwapo, Yusuf Manji ana kosa gani?

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Juni Mosi nilikuwapo kwenye Mkutano Mkuu maalum wa Yanga, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Ostarbay, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuingiza kipengele cha kuunda Kamati ya Maadili kwenye Katiba yao. Kila kitu kilikwenda vizuri, likiwapo agizo jipya la kumuomba Manji, agombee tena Uenyekiti wa Yanga, kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Juni mwakani.


Hii ni baada ya kusogeza mbele Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Juni mwaka huu, ambapo suala hilo liliungwa mkono na wanachama wote waliohudhuria. Hata hivyo, siku mbili baada ya Mkutano huo kupitisha mapendekezo hayo, wakaanza kujitokeza wanachama wengine wakipinga uamuzi wa Mkutano Mkuu, jambo linaloshangaza mno.

Sawa, inawezekana Manji na Kamati yake wamevunja Katiba kwa kusogeza mbele Uchaguzi wa Yanga. Katika kuliangalia hili; napata wasiwasi na kushuhudia unafiki wa baadhi ya wanachama wa Yanga.

Wanachama wanaotafuta nafasi ya kupata pesa kwa kuibua migogoro isiyokuwa na mwisho kwa klabu hii kongwe. Sina lengo la kumbeba Manji, maana si mwepesi wa kuchekea mabaya. Hili lifahamike, ndio maana hata uongozi wa Manji mara kwa mara nimekuwa nikiukosoa nionapo tofauti. Kwa hili la kusogeza mbele Uchaguzi au kuambiwa agombee tena, Manji hana makosa, maana ni matakwa ya wanachama waliojazana pale Osterbay.

Wao wenyewe waliomtoa Manji nje ili wamjadili kwa kina. Kila aliyesimama alimtaka Manji aendelee pamoja na kufanya kila analohitaji. Wakamuimbia kila aina ya wimbo mzuri kwa ajili ya kumburudisha. Ilibaki kidogo wambebe mgongoni, kama ishara ya kumuunga mkono. Hili lilikuwa kwa kila mtu, akiwamo Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanal Mstaafu Idd Kipingu, Bakari Malima na wengineo.

Inawezekana kweli kumefanyika ujanja ujanja wa kuwashawishi wanachama wakubaliane na madai yoyote ya Manji, lakini wote hao waliohudhuria walishindwa kusimama na kumpinga?


Kwani Manji ni nani? Aliwalazimisha wanachama hao wamuimbie wimbo mzuri wa upendo.Wengine walisikika wakisema, “Utakuwa mwenyekiti wa milele au walau miaka nane basi,”. Kauli hizi zilisikika kutoka kona zote za ukumbi ule.

Siwezi Kuvumilia. Siwezi kuvumilia kutokana na fitina, majungu na ubabaishaji wa wanachama hawa walioanza kuingiza chokochoko wakati wao wenyewe walipitisha maamuzi kwa ajili ya Yanga yao iliyoanzishwa mwaka 1935.

Najua Shirikisho la Soka nchini (TFF) ndio wanaosubiriwa kutoa ufafanuzi baada ya Yanga kusogeza mbele siku ya Uchaguzi wao. Kwa hawa wanachama waliopendekeza hilo kwa nguvu zote wanastahili kumlaumu Manji?

Hapa katu siwezi kuvumilia. Na ifikie wakati wanachama wa Yanga wajitambuwe kwa maendeleo ya klabu yao. Mkutano ule ulikuwa halali kutokana na wingi wa wahudhuriaji, huku wote wakiunga mkono kila jambo. Kama hivyo ndivyo, wanachama wote wa Yanga wanapaswa kuungana na maamuzi ya wenzao kwa maslahi ya klabu yao.

Huo ndio ukweli. Wanachama wa Yanga wasikubali kutunga uongo na kuanza kuzalisha mgogoro usiokuwa na mashiko kwa klabu yao.

Nilikuwapo kwenye mkutano ule, hivyo Manji asitolewe kafara maana ni uamuzi wa wanachama wote. Kinyume cha hapo, Yanga itabaki kwenye wasiwasi, mzozo, vurugu zisizokuwa na kichwa wala mguu kutoka kwa watu wanaoamini vurugu ndio njia ya wao kula na kusomesha watoto wao.

Tuonane wiki ijayo.

+255712 053949

No comments:

Post a Comment