Pages

Pages

Saturday, May 31, 2014

Kigoda Cup kuanza kutimua vumbi kesho wilayani Handeni



Na Mwandishi Wetu, Handeni
KIVUMBI cha michuano ya kuwania Kombe la Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda (Kigoda Cup) kinatarajiwa kuanza kesho kwenye Uwanja wa Azimio wilayani humo kikishirikisha timu 24 za soka na kumi za netiboli.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mashindano hayo, Ahamadi Salehe Chihumpu, timu za Chanika FC na Halmashauri FC zitafungua pazia la mashindano hayo upande wa soka, huku Mdoe na Alfa na Omega zikikata utepe kwa netiboli.

Chihumpu, alisema kuwa bingwa kwa upande wa soka atazawadiwa kombe na fedha taslimu sh milioni 1, huku mshindi wa pili ataondoka na sh laki 5 na wa tatu sh laki 3. Kwa upande wa netiboli, bingwa atabeba kombe na sh 300,000, wa pili sh 250,000 na wa tatu sh 200,000.

Mashindano hayo yaliayoanzishwa na Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, yanalenga kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wilayani humo, kuinua michezo na kupata nyota wa kuunda timu bora ya wilaya ya soka na netiboli.

Chihumpu alisema kuwa kabla Waziri Kigoda kuzindua rasmi mashindano hayo leo jioni, kutakuwa na shamrashamra za ngoma za asili, dansi na shoo kutoka kwa wasanii mbalimbali wa wilaya hiyo kuanzia saa 4 asubuhi.

Alisema kuwa pia Waziri Kigoda atazindua rasmi ukarabati wa Uwanja wa Azimio unaoendelea.

No comments:

Post a Comment