Pages

Pages

Saturday, May 31, 2014

Kigoda Cup kuanza kutimua vumbi kesho wilayani Handeni



Na Mwandishi Wetu, Handeni
KIVUMBI cha michuano ya kuwania Kombe la Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda (Kigoda Cup) kinatarajiwa kuanza kesho kwenye Uwanja wa Azimio wilayani humo kikishirikisha timu 24 za soka na kumi za netiboli.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mashindano hayo, Ahamadi Salehe Chihumpu, timu za Chanika FC na Halmashauri FC zitafungua pazia la mashindano hayo upande wa soka, huku Mdoe na Alfa na Omega zikikata utepe kwa netiboli.

Chihumpu, alisema kuwa bingwa kwa upande wa soka atazawadiwa kombe na fedha taslimu sh milioni 1, huku mshindi wa pili ataondoka na sh laki 5 na wa tatu sh laki 3. Kwa upande wa netiboli, bingwa atabeba kombe na sh 300,000, wa pili sh 250,000 na wa tatu sh 200,000.

Mashindano hayo yaliayoanzishwa na Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, yanalenga kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wilayani humo, kuinua michezo na kupata nyota wa kuunda timu bora ya wilaya ya soka na netiboli.

Chihumpu alisema kuwa kabla Waziri Kigoda kuzindua rasmi mashindano hayo leo jioni, kutakuwa na shamrashamra za ngoma za asili, dansi na shoo kutoka kwa wasanii mbalimbali wa wilaya hiyo kuanzia saa 4 asubuhi.

Alisema kuwa pia Waziri Kigoda atazindua rasmi ukarabati wa Uwanja wa Azimio unaoendelea.

Friday, May 30, 2014

Wabunge wa upinzani wasusa tena vikao vya Bunge, watoka nje kuacha kuijadili bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wabunge wa Upinzani, leo wameendeleza mchezo wao wa kususa na kutoka nje ya vikao vya Bunge, kwa madai kuwa muda wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni mdogo.
Wabunge wa upinzani wakati wanatoka nje ya Bunge, wakati bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini inajadiliwa.

Kauli ya kuwataka wabunge wa upinzani watoke ilitoka kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, ambaye pia ndio mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kutoka kwa wabunge hao wa upinzani kumekuwa kawaida sasa, jambo ambalo huenda likapokewa vibaya na Watanzania.

Akizungumzia hilo mjini hapa mara baada ya kutoka nje ya Bunge, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kuwa muda wa kujadili vikao vya Bunge la bajeti linaloendelea ulishawekwa, ikiwa ni baada ya Bunge la Katiba kula muda wao mwingi.

Wakati wabunge hao wanatoka nje, kauli za kejeli na dharau dhidi yao zilisikika, ikiwa ni pamoja na waache watoke, warudishe posho na nyinginezo.

Tanzania yashika nafasi ya pili michezo ya Afrika ya vijana


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA imeshika nafasi ya pili kwenye Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya jana (Mei 29 mwaka huu) kuilaza Afrika Kusini mabao 2-0.



Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa SSKB jijini Gaborone ambapo kwa matokeo hayo Tanzania imetwaa medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili. Nigeria ndiyo ilishika nafasi ya kwanza na kutwaa medali ya dhahabu.



Tanzania imemaliza ikiwa na pointi kumi ambapo ilishinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja mbele ya Nigeria.



Katika mechi ya kwanza ilitoka sare ya bao 1-1, ikawafunga Botswana 2-0, Swaziland wakachapwa 3-0 na baadaye kuwafunga Afrika Kusini 2-0. Timu ya Tanzania inayofundishwa na kocha Abel Mtweve ilifungwa na Nigeria mabao 2-0.



Wachezaji 16 waliounda kikosi hicho cha Tanzania katika michezo hiyo inayomalizika leo (Mei 30 mwaka huu) ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.



Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland wakati Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) zilijitoa dakika za mwisho.


Makamu wa Rais Dkt Bilal afungua kituo cha tiba, uchunguzi na mafunzo kwa wagonjwa wa saratani

Maskamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi zawadi mmoja kati ya washiriki waliosaidia ujenzi wa jengo jipya la Kituo cha Tiba, Uchunguzi na Mafunzo ya Magonjwa na Saratani za Matumbo na Ini cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwakilishi wa Taasisi ya Else Kronner Fresenius Stiftung, Prof. Konrad Mebmer, baada ya ufunguzi huo. Picha na OMR

HOTUBA:- HOTUBA YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA KITUO CHA TIBA, UCHUNGUZI NA MAFUNZO YA MAGONJWA NA SARATANI ZA MATUMBO NA INI CHA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI,
TAREHE 30 MEI, 2014

Mhe. Dkt. Kebwe Steven Kebwe
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;

Dkt. Gabriel Upunda
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Hospitali ya Taifa Muhimbili;

Dkt. Rufaro Chatara
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO)

Prof. H.C. Konrad Meßmer (MESSMER);
 Mwakilishi wa Else Kroner – Fresenius Stiftung ya Ujerumani;

Prof. Meinhard Classen;
Mwenyekiti, Munich Society of Gastroenterology;

Waheshimiwa Mabalozi;
 
Dkt. Marina Njelekela
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili;

Prof. Ephata Kaaya
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha  Afya na Sayansi za Tiba Muhimbili;

Prof. Msemo Diwani
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Taasisi ya Saratani Ocean Road;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Wizara ya afya kwa kunialika kushirikiana nanyi katika tukio hili. Kwa namna ya pekee nikupongezeni kwa maandalizi mazuri na kwa kuwa na wazo la kuanzisha kituo hiki ambacho kinaongeza nguvu katika utoaji huduma za afya hapa Tanzania. Kituo hiki ni cha kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na kitatoa huduma za tiba, uchunguzi na mafunzo kwa kutumia Hadubini. Ni wazi kuwa kituo hiki kitasaidia wananchi wetu kupata huduma hapa nchini na kitawapunguzia gharama zilizotokana na wao kwenda nje kutafuta tiba ya magonjwa haya.

Mabibi na Mabwana;
Ninafahamu kuwa ujenzi wa Kituo hiki umewezekana kutokana na ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich. Serikali ya Tanzania imechangia shilingi Milioni Mia Nane na Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich kupitia msaada kutoka ELSE KRONER FRESENIUS STIFTUNG ya Ujerumani, imechangia zaidi ya shilingi za kitanzania Bilioni Moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Huu ni uwekezaji mkubwa sana na naomba kutumia nafasi hii kukuombeni wenzetu wa Hospitali ya Muhimbili kuhakikisha kuwa mnakitumia kituo hiki ipasavyo huku pia mkivitunza vifaa vilivyopo.

Mabibi na Mabwana;
Magonjwa ya mfumo wa chakula na ini ni  miongoni mwa  matatizo makubwa ya kiafya yanayoikabili dunia nzima kwa sasa. Kumbukumbu za magonjwa ya Saratani duniani zilizotolewa mwaka 2008 zinaonyesha kuwa, jumla ya wagonjwa wapya takribani milioni tatu na laki tano, waliugua saratani za mfumo wa chakula na ini.  Kati ya hao asilimia 65% walitoka katika nchi maskini, ikiwemo Tanzania.

Shindano la vipaji vya uigizaji, Tanzania Movie Talents lahamia jijini Dar es Salaam

 Msimamizi wa Mashindano ya Tanzania Movie Talents, Bw Tony Akwesa akitoa maelekezo kwa washiriki waliojitokeza kwaajili ya shindano la Tanzania Movie Talents kwa kanda ya Pwani unaoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar Es Salaam
 Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye mstari tayari kwa kuchukua fomu za ushiriki wa shindano la Tanzania Movie Talents lililoanza rasmi leo Kwa Kanda ya Pwani.
 Washiriki waliojitokeza kuchukua fomu za Shindano la Tanzania Movie Talents wakisoma fomu kwa umakini kabla ya Kujaza...

Nay wa Mitego: Nakula Ujana unanipa raha kupita kiasi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa Hip Hop, Emmanuel Elbariki maarufu kama Ney wa Mitego, amesema wimbo wake wa ‘Nakula Ujana’ unampa raha kutokana na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa kizazi kipya nchini.
Msanii Ney wa Mitego pichani.
Ney wa Mitego aliyasema hayo katika mazungumzo ya kuelezea namna gani amejiwekea mikakati ya kulinda hadhi na uwezo wake kisanaa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya uzinduzi wa huduma mpya ya Kampuni ya Simu za Mikononi ya Airtel Tanzania, inayojulikana kama switch on, katika Hoteli Kilimanjaro Kempisk, inayotoa urahisi wa wateja wao kupata huduma ya internet kwa urahisi.

Alisema kuwa wimbo wake huo wa Nakula Ujana umetokea kupendwa na wengi, hasa anapokuwa katika maonyesho mbalimbali, hivyo kuonyesha kuwa maendeleo yake kisanaa yamekuwa mazuri kupita kiasi.
“Nawashukuru wadau wangu wote kwakuwa wanapenda kazi zangu, hasa huu wimbo wa Nakula Ujana, ambao mimi mwenye unanipa raha.
“Naamini kila kitu kitakuwa kizuri zaidi kwa kuwapatia raha mashabiki wangu wakati wowote, kwakuwa bado nitaendelea kupambana ili kufanya vizuri zaidi katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini,” alisema.
Katika uzinduzi huo wa huduma ya Airtel, watu mbalimbali walialikwa, sambamba na msanii Barnabas na Vanessa Mdee nao kuwa miongoni mwa wasanii waliokutana kwa pamoja katika tukio la aina yake.

Njama za kumchafua Zitto Kabwe zaanikwa, mwenyewe atoa ufafanuzi baada ya kutuhumiwa na Mr Sugu

Maelezo yangu kuhusu kazi za Kigoma AllStars/LEKADUTIGITE kwa NSSF na TANAPA.
Leo tarehe 29 Mei, 2014 Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni amenituhumu kuhusika na kinachoitwa ufisadi katika Shirika la TANAPA na NSSF. 
Zitto Kabwe, pichani.
Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kwa sasa nitatoa maelezo kwa ufupi ili kuondoa upotoshaji.
Kampuni ya LekaDutigite inamilikiwa na wasanii 15 ambapo kila mmoja ana hisa 5% ambazo niliwalipia ili waweze kushirikiana katika kazi zao. Hisa 25% zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya Gombe Advisors ambayo ni kampuni isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara (not for profit company). Hivyo Mimi binafsi sina maslahi yeyote ya kifedha zaidi ya kuwasaidia wasanii hawa katika kazi zao mbalimbali. 

Wasanii wa Kigoma AllStars wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Kwa upande wa TANAPA wasanii hawa waliandaa kazi ya kuitangaza Hifadhi ya Saadani na walilipwa. Kwa upande wa NSSF wasanii hao walitunga wimbo na video yake ( http://m.youtube.com/watch?v=sMl8T-RkIdM ) na wimbo huo unatumika katika Shirika hilo. 

Vile vile walifanya matamasha mbalimbali ya kuhamasisha watu kujiunga na NSSF. Wasanii wa Kigoma All Stars wote ni wanachama wa Mfuko huo. Katika kazi zote hizi Mimi binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha. Kauli yeyote ya kujaribu kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa. 

Thursday, May 29, 2014

Uchaguzi Mkuu Simba moto wawaka, TAKUKURU waingia kwa fujo zote

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Uchaguzi Mkuu Simba umeanza kuibua hofu baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kuanza kuufuatilia kwa karibu uchaguzi huo utakaofanyika Juni 29 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, baada ya maofisa wa taasisi hiyo kuvamia bwalo la maofisa wa Polisi, jijini Dar es Salam, wakati wa usaili wa wagombea.


Kuingia kwa maofisa hao, kumekuja huku uchaguzi wa Simba unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu ukizidi kupamba moto na kila mmoja kuwa na imani na mgombea wake kuwa ataibuka na ushindi.


Katika uchaguzi huo, nafasi ya urais inawaniwa na Evans Aveva na Andrew Tupa,  huku Michael Wambura akitupwa nje hivyo kusubiri uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).


Mbali na urais, Swed Nkwabi na Godfrey Kaburu wanachuana vikali, ambapo makundi ya wagombea hao wanaendelea kuchuana, huku kambi ya Nkwabi, inaonekana kuwa na nguvu zaidi ya Kaburu.

Wednesday, May 28, 2014

Uchaguzi Simba moto, ofisi zake zafungwa, Wambura atangaza vita

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU, mashabiki na baadhi ya wanachama wa klabu ya Simba, wamejitokeza kwa wingi kufunga ofisi za klabu hiyo kwa madai kuwa mgombea wao Michael Wambura aneonewa na Kamati ya Uchaguzi inayoendesha mchakato wa Uchaguzi ndani ya Simba.
Michael Wambura, pichani.
Wambura alikutana na waandishi wa habari, sambamba na kutangaza nia yake kupinga uamuzi huo kwa Kamati ya Rufaa ndani ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa madai kuwa mchakato mzima wa uchaguzi huo hauna lengo zuri na upande wake.
Jengo la Makao Makuu ya Simba, likionekana kujaa watu waliokuwa wakisikiliza kinachoendelea baada ya mgombea Michael Wambura kuenguliwa katika mbio za kuwania urais wa klabu hiyo jana na Kamati ya Uchaguzi ya Simba.

Akizungumza kwa umakini mkubwa, Wambura alisema Kamati hiyo haijamtendea haki kiasi cha kumuengua katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi ndani ya klabu yao ya Simba, ingawa mwenye anajua fika anayo haki na hadhi ya kuwania nafasi ya urais ndani ya Simba.


Alisema hajakubaliana na uamuzi huo, hivyo kesho saa 5 asubuhi atawasilisha rufaa yake katika ofisi za TFF, jijini Dar es Salaam. “Kuhusu uanachama wangu, niligombea nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF na nilipofika pale walinikatalia kuwa sio mwanachama wa Simba kwani nilivuliwa uanchama tangu mwaka 2010 hivyo kutaka nipeleke barua ya utambulisho, jambo ambalo klabu yangu ilinisaidia katika hilo,” alisema.

Aidha aliyataja majina saba ambayo hajakuwapo katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Mei 5 mwaka 2010 kuwa hayajakuwapo kwenye kikao cha kumfukuza uanachama wake, ingawa sahihi zao zinaonekana, hivyo zimefojiwa.

Majina hayo yaliyoandikwa kinyume na Omari Gumbo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa kikao na wajumbe ni Idd Senkondo, Ayoub Semvua, Abdalah Mkopi, Ramesh Patel, Hassan Hassan, Sultan Ahmed Salimu, Said Rubeya na Yassin Mwete.

Taifa Stars kuifuata Zimbabwe kesho na watu 30



NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
MSAFARA wa watu 30 wa Taifa Stars unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi unaondoka leo kesho alfajiri ya Mei 29 mwaka huu kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.

Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, ambapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5 asubuhi na ndege ya Kenya Airways.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa msafara wa Taifa Stars utaongozwa na Rais wake Jamal Malinzi, ambapo utarejea nchini Juni 2 mwaka huu.

“Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo,” alisema Wambura.

Kwa mujibu wa Wambura, mgawo ulikuwa ni kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.


Tuesday, May 27, 2014

Malawi wachezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Taifa Stars



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Timu ya Taifa Stars, leo imeondoka na ushindi waa bao 1-0 dhidi ya Malawi, katika mechi ya Kimataifa ya kirafiki iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

 Bao hilo lilifungwa na Amri Kiemba, aliyetumia vyema krosi ya Shomari Kapombe, akilifunga dakika ya 37 kipindi cha kwanza, huku akizongwa na msitu wa watu.
 
Kuingia kwa bao hilo kuongeza joto kwenye mechi iliyokuwa na ushindani wa aina yake kwa timu zote mbili lakini bado bao hilo lilidumu hadi filimbi ya mwisho kwenye mchezo huo.