Pages

Pages

Saturday, April 05, 2014

Yanga: Hatuna presha na Simba



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema kwamba hawana presha na mechi yao ya Aprili 19 dhidi ya Simba SC, badala yake wanaelekeza nguvu kwa mechi nyingi kabla ya kuvaana na mtani wao wa jadi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga kwa sasa imeweka kambi yao mjini Bagamoyo, ambapo Jumapili wataingia uwanjani kumenyana na timu ya JKT Ruvu ya mkoani Pwani, huku wakiwa na mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi mnono.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa ingawa watu wamekuwa wakiangalia zaidi mechi ya Simba, lakini timu yao inakabiriwa na michezo migumu mno, hivyo hawaoni sababu ya kuwekeza katika mechi moja ya watani.

Alisema mipango yao ni kunyakua ubingwa wa Bara na sio kumfunga mtani wa jadi, huku wakishindwa kutetea taji lao ambalo kwa sasa linaelekea kuchukuliwa na timu ya Azam baada ya kufikisha pointi 53, huku Yanga wao wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 46.

“Hatuwezi kuwekeza zaidi mechi ya Simba wakati tuna mechi nyingine ngumu, ikiwamo ya JKT Ruvu, hivyo tunakwenda hatua kwa hatua kwa ajili ya kuiweka timu yetu katika mazingira mazuri ya kutetea taji letu la Ligi ya Tanzania Bara.

“Tusipokuwa makini tunaweza kuifunga Simba lakini tukapoteza mechi nyingine, hivyo kusababisha kuuweka rehani ubingwa wetu wakati ndio mipango tunayoiweka kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda vizuri kwa kufanya maandalizi ya kila mechi na si ile ya watani wa jadi tu,” alisema.

Ligi ya Tanzania Bara imezidi kukolea joto huku timu ya Yanga na Azam zikionekana kukabana koo kuwania taji hilo, ambapo kwa mtani wake wa jadi Simba, msimu huu ameonekana hana chake baada ya kupata matokeo mabaya kwenye mechi zake.

No comments:

Post a Comment