Pages

Pages

Tuesday, April 15, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Siwezi kuwapongeza watoto wa mitaani kamwe

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
NASIKIA eti wale watoto wa mitaani waliokusanywa na kuelekea nchini Brazil wamepongezwa na serikali baada ya kunyakua Kombe la Dunia kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Baadhi ya wachezaji wa mitaani  waliopata taji nchini Brazil.
Kama hivyo ndivyo, basi sisi tuna moyo wa ujasiri sana. Kwa maana tumekubali kuwa suala la watoto wa  mitaani Tanzania limemea kiasi cha kukosa mbinu mbadala ya kupambana nalo.

Hii ni kazi kubwa. Tanzania nchi yenye wingi wa vipaji, tunahitaji kuwa na sera nzuri kwa ajili ya kuendeleza michezo, kama kweli tunataka kupiga hatua.

Huo ndio ukweli. Vinginevyo siwezi kuvumilia, kwasababu naona porojo, siasa, huku tukiwa wepesi kutafuta maeneo ya kupigia picha.

Kwanini nasema hivyo? Hata hawa watoto wa mitaani wanaopongezwa leo kwa kuchukua taji hilo, baada ya mwezi mmoja pengine wakawa wamerudi mtaani kuendelea na maisha yao magumu.

Mwakani watachukuliwa wengine, ukizingatia kuwa ni wengi kuliko wale wanaoishi maisha mazuri. Tukiendelea na mtindo huu, Watanzania hatutakuwa na  
mafanikio katika michezo zaidi ya kusubiria kuokoteza watoto na kuwasafirisha nchi za wenzetu na kuwatelekeza wakirudi.

Ndio maana nasema tunapaswa kubadilisha fikra zetu. Tuwe na mipango imara kama kweli tunahitaji kusonga mbele.

Huo ndio ukweli wa mambo. Hizi akili za kuwapigia makofi watoto wa mitaani waliokotezwa na kusafirishwa tumezipata wapi?

Basi wakisharudi wote wapelekwe shule au kuwekwa katika kituo kimoja cha michezo waendelezwe na sio kuwekwa kama pambo.

Au sisi tunaona sifa matatizo? Kumbe imekuwa kawaida sasa kujigamba kwa idadi kubwa ya watoto wa mitaani? Inawezekana ninachokiwaza si kizuri kwa upande wako, ila kiukweli siwezi kuvumilia.

Si ajabu baada ya watoto hao kurudi Tanzania, wamepata sehemu ya kusema na kutucheka kwa upumbavu wetu. Tunaelekea wapi Watanzania?

Makampuni yaliyojaa, lakini hakuna mipango imara ya kuendeleza michezo. Zaidi ya hapo tunasubiria kuokoteza watoto hao na baadaye kuwapongeza.

Hii si sawa. Tubadilisheni fikra zetu kama kweli tunahitaji kusonga mbele, maana juhudi za kupiga picha ni nyingi kuliko mikakati ya ufundi inayoweza kuinua soka la Tanzania.

+255712053949

No comments:

Post a Comment