Pages

Pages

Thursday, April 03, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Ligi isha nisikie vibweka vya majina ya usajili

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KUNA wakati unaweza kupata uchizi unapoangalia vitu ambavyo kwa bahati mbaya havikufurahishi. Unachofanya ni kuviacha vipite ili visisumbuwe akili yako. Kwa bahati mbaya, unashindwa maana baadhi ya vitu hivyo vinakukereketa kupita kiasi. Hatua hiyo inakufanya uanze kuviwaza hali ya kuwa ulijiapiza kuacha kuvifikilia na kuviweka moyoni na akilini mwako.

Moja ya wachezaji mahiri wanaotoka nje ya nchi, Khamis Kiiza, akikipiga katika klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Katika soka la Tanzania, huwa nawaza kila kinapofika kipindi cha usajili. Kuanzia tetesi hadi dirisha hilo linapofunguliwa na kufungwa, utashangaa majina mengi kutajwa.

Wakati mwingine, wanaotajwa si wale wenye kiwango kizuri. Tena kuonyesha umbumbumbu wetu, majina hayo hupendekezwa na watu wasiojua lolote juu ya mambo ya kiufundi uwanjani. Mvutano huo baadaye unazalisha timu isiyokuwa na kiwango chochote katika mechi za ndani na nje ya nchi. Mbaya zaidi, timu nyepesi inapotokea, mashabiki nyanya nao huinuka na kuanza kumsema vibaya kocha wao.

Hapo ndipo nisipoweza kuvumilia. Kwa soka la Tanzania, hata aje mzee Alex Ferguson aliyestaafu akiwa na mafanikio lukuki ndani ya timu yake ya Manchester United, kamwe hawezi kudumu.

Zaidi atakimbizwa na wale wasiojua lolote. Na haya hutokea zaidi kutokana na sekeseke la usajili kwa timu za Tanzania, zisizoangalia mahitaji na maoni ya benchi la ufundi.

Angalia, kocha wa Simba Zdravko Logarusic, anaonekana kulia juu ya uwezo wa wachezaji wake. Loga ana haki ya kulaumu. Hii ni kwasababu hakushiriki kusajili wachezaji aliowakuta kwenye kikosi chake.

Na hata Simba ijayo huenda ikawa nyanya, maana kuna hatari ya Logarusic kuenguliwa katika timu hiyo. Kwa kuenguliwa kwake, hivyo klabu itasajili kwa kuangalia matakwa ya viongozi wa juu, akiwamo Mwenyekiti na wengineo.

Na ndio maana nasema, ligi bora imalizike ili tuanze kusikia vibwagizo vya majina ya usajili. Wengine wanaotajwa kusajiliwa utabaki kucheka. Sitaki kuwataja wachezaji wepesi wanaosajiliwa mara kwa mara, ila muhimu ni kuhakikisha kuwa mfumo mzuri unawekwa katika jukumu la usajili. Huo ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia, maana wadau wa soka kwa ujumla wetu tumeamua kufanya mambo mepesi na kuacha yale mazito yenye tija kwa sekta ya mpira wa miguu hapa nchini.

Hii sio sawa.


+255712053949

No comments:

Post a Comment