Pages

Pages

Thursday, April 24, 2014

Serikali yapiga marufuku wnasiasa kwa timu ya Mbeya City



Na Pendo Fundisha, Mbeya.
SERIKALI Mkoani Mbeya imepiga marufuku itikadi za kisiasa katika uendeshaji wa timu ya soka ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ili kulinda uhai wa timu hiyo.

Uamuzi huo umefikiwa  kufuatia baadhi ya wanasiasa kuanza tabia ya kujinadi kuwa mafanikio ya timu ya Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya yametokana na juhudi zao na vyama vyao vya siasa.

 Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, aliyasema hayo kwenye hafla ya kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu ya Mbeya City iliyoambatana na kuivunja rasmi kambi ya timu hiyo baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara huku timu hiyo ikifanikiwa kushika nafasi ya tatu.

Mtunguja, alisema tayari baadhi ya wanasiasa mkoani hapa wameanza kuyahusisha mafanikio ya timu hiyo na harakati zao za kisiasa za vyama vyao hali ambayo ni hatari kwa uhai wa Mbeya City katika ulimwengu wa soka nchini.

Alisema, tabia hiyo inaweza kuwagawa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kwamba kila mmoja ana mapenzi na chama chake cha siasa hivyo kuingiza itikadi kwenye uendeshaji kutasababisha ubaguzi baina yao.

“Wanasiasa watuache, wasituvuruge baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana sasa wanataka kujiingiza katika timu, watatuulia timu yetu.” alisema Mtunguja.

Kufuatia mafanikio ya timu hiyo, Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, alisema Halmashauri ya jiji hilo imeamua kuboresha mishahara ya wachezaji ili kuzuia uwezekano wa kurubuniwa na timu kubwa kwa kigezo cha maslahi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mbeya City, Musa Mapunda, alisema baada ya kufanikiwa kushika nafasi ya tatu msimu huu, sasa wanaweka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inachukua ubingwa wa ligi Kuu ya Soka Tanzania bara msimu ujao.

Naye kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema katika usajili wao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi hiyo hawatachukua wachezaji wenye majina kutoka timu zinazoshiriki ligi hiyo bali bali ataangalia zaidi wachezaji chipukizi wasio na majina kutoka ndani ya mkoa wa Mbeya.

Mbeya City ilianzishwa Julai mwaka 2011 na huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki ligi hiyo na kupata mafanikio yak upigiwa mfano.

No comments:

Post a Comment