Pages

Pages

Thursday, March 13, 2014

Wakulima wa chai Bumbuli waiangukia serikali


Na Mwandishi Wetu, Bumbuli

SERIKALI imetakiwa kufikia uamuzi wa haraka juu ya kumtafuta mwekezaji mwingine wa kiwanda cha Chai, cha Mponde,  kilichopo Halmashauri ya Bumbuli,  Wilayani  Lushoto, ili kuinusuru chai ya wakulima inayoendelea kuharibikia shambani kwa miezi minane sasa, tangu kifungwe.

Kiwanda hicho cha Mponde ambacho ni Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA), wanamiliki asilimia hamsini, huku mwekezaji asilimia iliyobaki, kilifungwa baada ya wakulima kugoma kupeleka  majani  mabichi  kwa madai kuwa mwekezaji huyo anawalangua.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani Bumbuli, wakulima hao walisema tangu kiwanda hicho kimefungwa jana chai yao inaharibikia mashambani na kuwapa ugumu wa maisha.

Hamis Jabiri mkulima wa Chai katika halimashauri hiyo, aliiomba serikali kuwafungulia kiwanda chao ili kunusuru maisha yao, maana wamekuwa wakiishi maisha magumu na kuongeza makali ya maisha na kuyumbisha uchumi wao.

Naye Robart Tembe, alisema baada ya kufikia uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho, serikali iliunda tume ili kupendekeza kuundwa kwa uongozi wa muda katika kiwanda hicho.

"Waandishi wa habari maamuzi ya kufungwa kwa kiwanda tuliyafanya sisi wakulima kwasababu hatumtaki mwekezaji, hivyo serikali ilete mwingine na kuanza kuendesha uzalishaji na sisi tuuze chai yetu kama ilivyokuwa mwanzo,” alisema Tembe.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatreace Msomisi, alisema tangu kiwanda hicho kilivyoacha kufanya kazi halmashauri hiyo imeathirika kiuchumi, kwasababu ya kiwanda hicho kuwa tegemezi la wakulima.

No comments:

Post a Comment