Pages

Pages

Tuesday, March 11, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Tunakesha kuwatazama, ila hatujifunzi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

INASHANGAZA! Wadau wa michezo hususan mpira wa miguu tunakesha kwenye luninga zetu kuwatazama wenzetu, hali ya kuwa hatujifunzi kutoka kwao.

Sasa uwapi umuhimu wa kuwatazama? Ni bora hata tulale tu maana hakuna faida. Iwapi faida? Kumbe kila tunapoingia uwanjani tunafungwa, si bora tucheze karata?
Wengine ni wajuzi wa kuzungumza. Kwenye maneno hapo, utaona sisi wajuzi, wakati si lolote si chochote. Hapa Siwezi Kuvumilia.

Angalia, timu ya Manchester United yenye maskani yake nchini Uingereza, ipo katika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi kabla ya mechi za mwisho wa wiki.

Ni matokeo magumu, ambapo kocha wa timu hiyo, David Moyes anakutana nayo kila siku. Moyes alianza kuitumikia timu yake hiyo Julai Mosi mwaka jana, akitokea klabu ya Everton, akirithi mikoba ya Sir Alex Ferguson aliyestaafu baada ya kuitumikia Manchester kwa miaka 26.

Kwa mashabiki wa Tanzania wale wanaoshabikia Manchester ya Moyes, watashindwa kujizuia na kutoa maneno makali dhidi ya kocha huyo.

Waulize kitu gani kifanyike ndani ya timu hiyo, watakwambia Moyes aondoke. Mashabiki hawa Tanzania watakwambia hivyo kwasababu wameshazoea soka la Tanzania linalokwenda kwa kubahatisha.

Wameshazoea kocha anapewa mechi tatu, akifungwa basi anatimuliwa. Ndio hapo ninaposhindwa kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwasababu tunawaangalia wenzetu lakini tunashindwa kujifunza.


Mpira si maneno tu. Tujiulize, miaka 26 ambayo Ferguson amekuwa kocha wa Manchester, timu za Simba, Yanga zimebadilisha makocha wangapi?

Hata huyu Moyes, endapo angekuwa kocha wa Simba au Yanga na akakutana na matokeo kama anayopata sasa, sioni kama angeendelea kuwa kocha wa wakongwe hawa.

Sikatazi kocha kubadilishwa, ila mechi moja au mbili haziwezi kupima uwezo wa makocha. Huu ndio ukweli, hivyo timu za Tanzania lazima zijipime.

Viongozi wawe na mipango ya muda mrefu ili iwe na tija kwa soka lao. Naamini tukifanya hivi; tutakuwa tumepiga hatua kubwa kukuza soka la Tanzania.

Haina maana ya kuangalia wenzetu wanavyopiga hatua, lakini sisi ni mashabiki mandazi. Mashabiki wasiokuwa na nia ya dhati ya kukuza soka lao.

Bado najiuliza, kama Moyes angekuwa kocha wa Simba au Yanga, angekuwa hadi leo au angeshatolewa macho na wanaojiita wenye timu zao?

Kama Hassan Dalali licha ya kuwa mwenyekiti wa Simba mwenye mafanikio alifuatwa nyumbani kwake na kutukanwa na baadhi ya wanachama wake licha ya kuwa hachezi yeye uwanjani, itakuwa kocha anayejua masuala ya ufundi?

Na hata Moyes sidhani kama angekuwa na ujasiri wa kuvumilia matusi, kejeli pengine hata kurushiwa mawe kwa kuvumilia matokeo mabaya uwanjani, kiasi cha kushindwa kuvumiliwa na mashabiki wake.

Kama Ernest Brandit, kocha wa Yanga alitimuliwa licha ya kuipa ubingwa timu yake, huyu Hans Van Plujin, atadumu hata kama amefungwa mfululizo?

Ndio maana nasema, tunaangalia wenzetu, lakini tunashindwa kujifunza kutoka kwao, hivyo kuwa wahujumu wakubwa wa maendeleo ya mpira Tanzania, hivyo kamwe siwezi kuvumilia jambo hili.


+255712053949

No comments:

Post a Comment