Pages

Pages

Monday, February 24, 2014

Yanga, Al Ahly haitafungwa kwa magazeti

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KIDOGO nimepata furaha kuona kocha msaidizi wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwassa, alielekea nchini Misri kwa ajili ya kusoma nyendo za wapinzani wao, timu ya Al Ahly, kabla ya kuvaana Jumamosi wiki hii.


Timu hiyo tishio katika ukanda wa Afrika Magharibi, inajiandaa kucheza na Yanga, timu kongwe hapa nchini, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kipa wa Yanga, Juma Kaseja, ni moja ya walinda mlango makini wanaopaswa kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya mechi ya Al Ahly hap0 Machi Mosi mwaka huu.

Yanga inaingia uwanjani huku Watanzania tukiwa na kumbukumbu mbaya ya timu zetu kushindwa kutamba mbele ya timu za Misri.


Ni timu ya Simba tu, walau inaweza kuwa na historia japo kwa uchache juu ya timu za kutoka Misri, walipokutana na mara chache iliweza kujivunia.


Mwaka 2003, Simba iliweza kuwaondosha Mabingwa wa nchi hiyo, timu ya Zamalek, baada ya kushinda bao 1-0 jijini Dar es Salaam, kabla ya kushinda 3-2 kwa njia ya penati katika Uwanja wa ugenini.


Ukiacha historia hiyo kwa Simba dhidi ya Zamalek, bado timu hiyo ina chakujivunia kwa timu ya Mafulira Wandarers ya Zambia, mwaka 1979 baada ya kuchapwa bao 4-0 kwenye uwanja wa Taifa, kabla ya kushinda bao 5-0 ugenini.

Ni ushindi mkubwa ambao bado unakumbukwa na wengi na ukishangaza pia. Nimejikuta nikianza hivi kwa kuangalia mechi ijayo ya Yanga dhidi ya timu ya Al Ahly ya Misri.


Yanga hawapaswi kubweteka wala kujiandaa kwa zima moto. Itaumbuka. Inapaswa kujua ina mechi ngumu kuliko hata ile ya Simba dhidi ya Zamalek ya nchi hiyo.


Nasema haya kwasababu kama ilivyokuwa kwa Simba, Yanga inakutana na Bingwa mtetezi wa michuno hiyo.


Pia inakutana na timu ambayo ambayo hapana shaka inafahamu namna gani Tanzania kuna timu nzuri zilizokusanya wachezaji mahiri.


Kama hivyo ndivyo; sidhani kama watacheza kwa kubahatisha. Wataingia uwanjani kutafuta ushindi katika mechi ya ugenini ili wapate nafasi nzuri watakaporudiana nyumbani kwao.

Wadau wa soka na mashabiki wataumia sana kama wachezaji na viongozi wao wataifananisha Al Ahly na Komorozine ya nchini Comoro.


Wataumbuka na kutoka vichwa chini. Nadhani ni wakati wao benchi laa ufundi kukaa chini na kuweka mipango kabambe.


Isiweke nguvu zao zote kwenye vichwa vya habari ili kuwavutia wadau wao juu ya mechi hiyo ngumu na inayoangaliwa kwa jicho makini sana.


Kwa bahati mbaya, timu zetu kongwe wakati mwingine hujikuta zinafungwa kabla ya mechi kumalizika.


Hii ni kwasababu wanajigamba tofauti na ufundi wao uwanjani. Angalia, wakati inashinda bao 7-0 dhidi ya Komorozine katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, maofisa kadhaa wa Al Ahly walikuwapo uwanjani.


Al Ahly walikuwa wa kwanza kuwasoma Yanga kabla ya kujibu mapigo, ilipomtuma Mkwassa kuelekea Misri.


Wasiwasi wangu ni kwamba; Al Ahly walivuna vitu vingi kutoka kwa Yanga kwasababu ujio wao haukupewa mkazo tofauti na wao kujua kuwa Yanga wapinzani wao nao wangekwenda kwao kuangalia wanachofanya kabla ya mechi yao.


Kila mtu ana mbinu zake. Kinachotakiwa ni ushindi ndani ya uwanja, hivyo ni wakati wa Yanga kufahamu kiu ya mashabiki wa soka wa Tanzania kuona wanafuzu mbele ya Al Ahly.


Hili linaweza kufanikiwa, lakini si kwa kutoa tambo bila mikakati kwenye vyombo vya habari. Yanga kwa kupitia mabosi wake wa ufundi, wanapaswa wajuwe uwezo na hira pia wapinzani wao wanapokuwa uwanjani.


Mara kadhaa timu za Misri zinapoona zimeshindwa ndani ya uwanja hutafuta ushindi kwa mbinu nyingi, hasa kuwavuruga wapinzani wao kisaikolojia.


Hii iliwahi kutokea mara kadhaa na inaweza kutokea pia kwa Yanga, maana pamoja na ubora wa soka la Misri, bado hawana dharau kwa timu wanazokutana nazo, hasa za Tanzania.


Wachezaji wa Yanga waingie uwanjani kwa kutafuta ushindi mnono katika mechi ya kwanza nyumbani, kabla ya kutafuta sare, kama watashindwa kushinda tena uwanja wa ugenini.


Yanga ina kila sababu ya kusonga mbele dhidi ya Al Ahly, licha ya kuwa wanakutana na timu ngumu yenye kiu ya kusonga mbele.


Huu ndio ukweli, hivyo litakuwa jambo zuri kama kila mwana Yanga atakuwa na kiu moja ya kuona timu yao inasonga mbele kwa kufanya bidii uwanjani, kuandaa kikosi imara na sio kuwa wajuzi wa kupamba kurasa za magazeti maana soka la ainaa hiyo daima haliwezi kuwasaidia.

Mungu ibariki Tanzania


+255712053949

No comments:

Post a Comment