Pages

Pages

Sunday, January 19, 2014

Wilaya 31 za Tanzania zakutwa na madini ikiwamo wilaya ya Handeni na Kilindi mkoaani Tanga

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo

Wilaya 31 nchini zimegundulika kuwa na madini ya aina mbalimbali kutokana na utafiti uliofanywa na Wakala wa Jiolojia nchini (GST) kwa kushirikiana na Wizara ya Madini.
 
Utafiti huo ulifanywa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama ndege kwa ajili ya kupima ramani kwenye maeneo yenye madini. 
 
Hayo yalibainishwa katika kongamano la uzinduzi wa taarifa za utafiti wa Fizikia ya Miamba (Jiofizikia) uliofanyika  katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, jana.
 
“Tunachokifanya hapa, ni kujua kiasi gani cha madini yaliyopo nchini. Huu ni mradi mkubwa sana, tulitumia teknolojia ya kisasa kwa kutumia ndege angani, tofauti na tafiti zilizokuwa zinafanywa miaka ya 70,” alisema  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akizindua taarifa hizo.
 
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, mradi huo ni wa mara ya kwanza kutumia vyombo vya kisasa kujua madini yaliyopo chini ya ardhi ya Tanzania, ulihusisha wilaya 31 ambazo ziligundulika kuwa na madini ya aina mbalimbali.
 
Alitaja wilaya hizo kuwa ni pamoja na Dodoma, Bahi, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa, Manyoni, Ikungi, Singida, Mkalama, Iramba, Igunga, Kiteto, Hanang na  Babati. 
 
Nyingine ni Simanjiro, Mbulu, Arumeru, Monduli, Moshi,  Handeni.Kilindi, Korogwe, Chemba, Mvomero, Kilosa, Gairo, Bagamoyo, Chunya, Mbozi na Mbarali.
 
Alisema ramani hizo zilizinduliwa jana zilikuwa zinaonyesha maeneo yenye madini nchini na ramani hizo si kwa ajili ya rasilimali hizo bali pia huweza kutumika kwa matumizi mengine kama vile uchorongaji wa ardhi na upangaji miji.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma, alisema, takribani Dola za Marekani bilioni 11, zilitumika katika mradi huo wa utafiti  na kutaja changamoto ni teknolojia.
 
Profesa Mruma, alisema baada ya kumaliza katika wilaya hizo 31, masuala ya kifedha yakikaa sawa, wanatarajia kuendelea kufanya utafiti na kupima ramani za jinsi hiyo  katika wilaya zingine za Nachingwea, Mpanda, Sumbawanga na Songea na kwamba maeneo ambayo yamegundulika kuwa na madini, yatatangazwa kwa wananchi kwa utaratibu maalumu uliowekwa na serikali na Watanzania wanapaswa kuwa na leseni kwa ajili ya kunufaika na rasilimali hizo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment