Pages

Pages

Wednesday, January 08, 2014

Julio: Makocha wazawa tumegeuzwa makatapila



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam



KOCHA wa zamani wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema kwamba mara kadhaa makocha wa Tanzania wanafanywa kama makatapila katika klabu kubwa, zikiwamo Simba na Yanga.




Kocha Jamhuri Kihwelo Julio
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati anapewa cheti cha kushiriki kozi ya makocha iliyofanyika mjini Zanzibar, Julio alisema hali hiyo hutokea na kutokana na kuhitajika katika timu kabla ya kutimuliwa atakapopatikana kocha mwingine.




Alisema ingawa makocha wanakutana na changamoto hizo, lakini wao wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakabiliana na matatizo yote katika timu hizo kwa ajili ya nafasi zao kuwanufaisha Watanzania wote.




“Mimi siangalii matatizo hayo, ingawa tunajua kuwa tunaitwa katika timu zetu kuwachongea  barabara wengine wanaokuja kurithi mikoba yetu katika timu nyingi.



"Sisi hatuna tofauti na makatapila, lakini hatuna wasiwasi katika hilo, maana kwa upande wangu nimekuwa na ndoto na uwezo wangu kuwanufaisha Watanzania, ndio maana najiendeleza kila mara,” alisema Julio.




Aidha, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Selestine Mwesigwa, aliwataka makocha wa Tanzania kuwa na moyo wa kujiendeleza ili wajiweke katika mazingira mazuri zaidi katika majukumu yao ya kila siku.



“Kwa makocha wa Tanzania wao ndio huimudu lugha mama ya Kiswahili, hivyo wanapojiendeleza kidogo kwa kuchukua kozi mbalimbali wanakuwa kwenye soko kubwa na huwa nafasi ya kukuza mpira wa miguu hapa nchini,” alisem Mwesigwa.

No comments:

Post a Comment