Pages

Pages

Wednesday, December 25, 2013

Wananchi Misima waondolewa hofu kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji Handeni



Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni

WANANCHI na wakazi wa Kata ya Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga, wameombwa kutokuwa na wasiwasi na hatua ya kuingizwa kwenye Halmashauri ya mji kwakuwa mpango huo sio mbaya kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Thomas Mzinga, akiwa kwenye moja ya matukio ya kijamii wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alipozungumza na Mtandao wa Handeni Kwetu, juu ya hatua mbalimbali za kuunganisha eneo hilo na Handeni Mjini.

Alisema mchakato wote wa kuunganisha mji huo na Kata ya Misima ulifuata sheria zote, huku akisema woga wa wananchi unatokana na hoja dhaifu kuwa viwanja vyao vitauzwa na serikali.

“Sio kweli kama kuingia kwenye Halmashauri ya Mji basi viwanja vyote na mashamba yaliyokuwapo yatauzwa ovyo na watendaji wa serikali, maana hiyo si sababu ya kupanua mji wetu.

“Wananchi wameaminishwa uongo ili suala hilo lisiwe na mafanikio, hivyo tunaamini tutaendelea kuhamasisha wananchi wetu na Watanzania kwa ujumla ili kwenye mambo ya kimaendeleo tufanye kama inavyopangwa na viongozi wa serikali kwa ujumla wake,” alisema Mzinga.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hatua ya kuunganisha eneo la Misima katika Halmashauri ya Mji ni kuweka mikakati kabambe ya kuupanua mji wote wa Handeni na kusogeza pia maendeleo karibu na wananchi.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa, wananchi wa Misima wamekuwa wakivutana na viongozi wa serikali ya wilaya ya Handeni wakigoma kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji kwa madai kuwa bado mapema na kijiji hicho kipo mbali kabisa, huku wakiona kuwa huenda ni mipango ya waheshimiwa hao kusogea karibu ili kuteka mashamba yao.



No comments:

Post a Comment