Pages

Pages

Monday, December 09, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Tukitoka kwenye magazeti, tuhamieni ‘chandimu’

Na Kambi Mbwana, Handeni
KWA wiki kadhaa sasa, nipo katika mkoa wa Tanga, nikiwa kwenye majukumu mengine ya Kitaifa, ukizingatia kuwa ili Dunia isonge mbele lazima kuwe na pilika pilika za kimaisha. Nimetembelea wilaya kadhaa na kujionea mambo mengi ya kunifurahisha, hasa yanayohusu mchezo wa mpira wa miguu.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, moja ya viongozi wanaopaswa kuwa makini katika utendaji wao ili kuendeleza mpira wa miguu kwa vitendo.
 
Mchezo huo unaopendwa na watu wengi duniani, ni kati ya sekta ambazo tunashuhudia mwingiliano mkubwa sanjari na kuvutia vijana wetu wanaopenda kujiingiza katika kandanda.
 
Mpira wa miguu ndio michezo mizuri na rahisi kuchezwa na inayovutia wengi, maana hata watoto mtaani utakuta wameweka mawe yao manne, mawili huku na mawili kule kama goli zao.
 
Hii inavutia kusimama na kuangalia jasho linavyotoka kwa watoto hao. Utajisikia raha kuona chenga na nyodo zinavyoonyeshwa kwa watoto hao ndani ya uwanja, wenyewe wanaita ‘Chandimu’.
 
Hata hivyo, mawazo yakikujia kuwa watoto hao wachache unaoona kwa macho yako, ni kati ya mamia yanayoibukia uswahilini na kutokomea kusipojulikana kwa ajili ya uzembe wetu.
 
Ndio ni uzembe wetu, maana tuliokuwa wengi tumezoea kuangalia majina ya akina Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Kelvin Yondan, yakitawala kwenye vyombo vya habari na kushindwa kuweka sera nzuri kuhakikisha kuwa vijana wengi wanapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao.
Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu wengi wao wanaangalia walipokuwapo. Hatuna dhamira ya kweli.
Pamoja na kusema yote hayo, najikuta nikihema, nikiona kwa sasa sina kwa kuelekeza lawama zangu, hasa ukiangalia kuwa utawala mpya ndani ya Shirikisho la Soka nchini TFF umeingia. 
 
Alikuwa Leodgar Tenga kama Rais wa TFF na sasa ni Jamal Malinzi. Huyu Malinzi ameingia kwa mkwara mzito sana. Kila siku ya Mungu nasikia matamko kiasi cha kupasua kichwa change.
 
Sawa, nikisema sana nitaambiwa muda bado. Lakini je, Malinzi ameingia TFF na watu wote wapya? Bila shaka utagundua kuwa baadhi yao walikuwapo katika utawala wa Tenga.
 
Zaidi ya hapo utaona ni ubabaishaji tu. Hakika hatuwezi kusonga mbele kama hatugundua makosa yetu.  Ukweli ni kwamba sehemu za mikoani, katika vijiji mbalimbali vimejaa vipaji, lakini hatuna mipango zaidi ya kuona wale waliokuwa kileleni wanaendelea kubabaikiwa na kufifisha ndoto nyingine.
 
Si mara moja kupokea simu kutoka kwa watu wa mikoani wakililia mahali kwa kuonyesha uwezo wao. Viongozi wetu wa chama na serikali nao wamekalia siasa, kutoa sera zao kwenye kampeni na baada ya kupata wanachohitaji wanajifanya hawaoni wala kusikia.
 
Mechi za mchangani katika maeneo yao hufanyika wanapokwenda kuzindua kampeni zao sanjari na kuwanunua vijezi vya bei rahisi ili kuwarubuni katika mchakato wao wa kisiasa.
 
Huu si wakati wa kupiga porojo wakati maelfu ya vipaji yanatokomea katika vijiwe vya gongo na bange. Nani asiyependa kuona akina Ngassa wapya wanatokea katika maeneo yenye changamoto mbalimbali?
 
Je, tunaona thamani gani kushindwa kubuni walau ligi ndogo za mikoani, au kusaidiwa vifaa vya michezo kwa timu za mikoani kabla hata ya Uchaguzi Mkuu? Kila mtu atomize wajibu wake.
 
Kinyume cha hapo, siwezi kuvumilia kuona hatuna jipya katika kubuni mikakati yenye tija na soka letu. Sio siri, huku nilipokuwa katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Handeni, natamani nisihudhurie mechi za mchangani maana naona aibu kuwa vijana hawa wanaishia gizani miaka nenda rudi. Au kama kweli tuna dhamira ya kuendeleza soka letu, tukitoka kwenye soka la magazetini, tuhamieni chandimu.

Tukutane tena wiki ijayo.
+255712053949

No comments:

Post a Comment