Pages

Pages

Friday, December 06, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Kwa Simba hii ya magazeti, basi kazi ipo


Na Kambi Mbwana, Handeni

NI jambo la kawaida mchezaji yoyote kuandikwa katika vyombo vya habari, hususan magazeti, ukaona kesho anasajiliwa na klabu ya Simba, tena bila hata kuridhishwa na kiwango chake ndani ya benchi la ufundi.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Ukitaka kulizungumzia jambo hili, utaona jinsi gani viongozi wa klabu za soka Tanzania, hasa za Simba na Yanga wanapoingia katika majaribu ya kuchukua mchezaji ili mradi ameng’aa kihabari.

Wakati mwingine mchezaji huyo amewekwa gazetini si kwa sababu ana kiwango kizuri, hivyo endapo viongozi wa soka wataendelea na mpango wao wa kusajili kwa kuangalia gazeti limeandika nini, hakika hatuwezi kuendelea.


Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Hatuwezi kuendelea, kama vyombo vya habari ndivyo vitakavyosajili. Hii ni kwasababu, mara kadhaa mchezaji anayeandikwa kupita kiasi, si kama ana kiwango cha juu.


Na kiwango hicho inastahili kuonekana mbele ya kocha wa timu husika na kwa viongozi wanaotumika kusajili, wakiamini wataonekana ni wachapakazi mbele ya wanachama na wadau wa soka.

Ukiangalia kwa sasa, vyombo vimegeukia kwa kipa Yaw Berko. Huyu aliwahi kucheza ndani ya Yanga kabla ya kuondoka akidaiwa kuwa kiwango chake kimeshuka.

Berko sasa anapigiwa chapuo na wadau akihusishwa na mipango yake ya kujiunga na Simba, timu pinzani na ile aliyoichezea hapa Tanzania.


Jumamosi iliyopita, Berko alitarajiwa kuwasili nchini, tayari kuingia makubaliano na Simba, katika michuano ijayo, ikiwamo Ligi ya Tanzania Bara, mzunguuko wa pili, utakaoanza Januari mwakani.

Inashangaza kama viongozi wetu wa soka watakuwa wakisajili kwenye magazeti, jambo ambalo haliwezi kuendeleza soka la Tanzania. Tunahitaji viwango vilivyothibitishwa na makocha wetu.


Wao ndio wanaofahamu wapi kwenye mapengo kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao, hivyo kuna kila sababu ya kubadilisha nyendo zetu kama kweli tunahitaji kusonga mbele.

Huo ndio ukweli wa mambo. Lakini kusajili wale walionekana kwenye magazeti wakati mwingine si dawa ya kukuza soka, isipokuwa njia mbaya ya kulidumaza soka letu linalokwenda mbele na kurudi nyuma.


Hakika siwezi kuvumilia. Siwezi kuvumilia hii haitokani na mtazamo wa kumsajili Berko, ila ni pale tutakapoendeleza maisha ya kusajili kwa kupitia vyombo vya habari, tena bila kuangalia mahitaji ya benchi la ufundi.


Tukifanyaa hivyo, miaka nenda rudi Tanzania itaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu maana si kila mmoja ana bahati ya kuandikwa katika vyomb hivyo, jambo linaloweza kuwafifisha wale wenye uwezo wa juu wa kucheza soka na wanaopata nafasi wakiwa wale wa kawaida.

Tukutane tena wiki ijayo.


+255 712053949

No comments:

Post a Comment