Pages

Pages

Friday, December 20, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Karibu Logarusic, ila jiandaye kwa mengi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA hali ilivyokuwa ndani ya klabu za Tanzania, hususan zile kongwe za Simba na Yanga, utaamini kuwa hata aje kocha wa aina gani, bado mabadiliko yanaweza kuwa ya kubangaiza.
Siku kocha mpya wa Simba, Zdravko Logarusic alipowasili Tanzania.
Hii ni kwasababu mara kadhaa utaona jinsi baadhi ya viongozi wa soka na wadau wao wanavyojifanya hawanazo katika kubuni mikakati yenye kuleta maendeleo ya klabu zao.
 
Wakati nasema haya, nakumbuka jinsi kocha mpya wa Simba, Zdravko Logarusic alivyopokewa kwa mbwembwe na mashabiki wa timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi.
 
Hata hivyo, utagundua kuwa aina ya mapokezi ya Logarusic si kitendo kigeni, maana tayari walishawahi kupokewa kwa vishindo kiasi cha wao wenyewe kujishangaa.
 
Hakika siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia, maana najua kocha huyo hatakuwa   na maisha mazuri ndani ya Simba. Anapita njia tu. Labda amekuja kutalii au kujionea viongozi wa soka wasiokuwa na dhamira ya kweli ya kuokoa soka letu.
 
Ama amekuja kuangalia mashabiki na wanachama wenye mihemko ya aina yake. Ukifiria sana unaweza kulia. Ni pale makocha hao wa kigeni, mfano wa Logarusic wasivyokuwa na heshima mbele ya jamii yao pale matokeo yanapokuwa magumu.
Kwa wasiojua, chokochoko huanza tararibu mno. Kwanza utaona kocha anavyopangiwa wachezaji wa kucheza uwanjani na wale wanaotakiwa wawekwe benchi.
 
Kesho utaona anavyoingia kwenye mkwaluzo na viongozi wake na mwisho wake wanachama au mashabiki wanaingilia kati. Matusi na kejeli yanapamba moto.
 
Mwisho wa siku ni safari ya aibu. Matusi lukuki kuelekezwa kwa makocha ambao hapo kabla walipokewa kama wafalme. Kwa klabu za Simba na Yanga, naweza kusema kwa miaka hii hata kama aje Sir Alex Ferguson au Rafael Benitez, bado hakutakuwa na kipya.
 
Ndio, maana makocha hao watakapofanikiwa kuunda program zao hazitakuwa na mashiko na badala yake wataambiwa namna ya ufanyaji wa kazi wenye kutafuta sifa za kijinga.
 
Hakika siwezi kuvumilia hata kidogo. Hali hii inanifanya nione bado kuna kila sababu ya kujiangalia upya katika harakati za kukuza na kuendeleza soka letu.
Hii hali ya kuwashangalia makocha wa kigeni leo na kesho kuwatukana bila sababu za msingi zimepitwa na wakati. Huu ndio ukweli. Ifikie wakati kila mmoja ajitambue.
 
Ndio maana nasema, karibu kocha mpya wa Simba, ila pia ujiandaye kwa mengi maana Simba hii uliyoshangiliwa wewe siku zote haitabiriki na haina mipango ya kweli ya kimaendeleo.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949
 

No comments:

Post a Comment