Pages

Pages

Monday, November 11, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Mashabiki tunang’oa viti uwanjani ili iweje?

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA hasira nyingine ukifikiria unaweza kucheka mwenyewe. Hii ni kwasababu baadhi yetu tunafanya vitu vya kijinga visivyokuwa vya kiungwana.

Mashabiki wanaodhaniwa ni Simba waking'oa viti uwanjani.
Hawa ndio wale wanagombana na wake zao ndani ya nyumba, lakini hasira inaingia kwa motto mchanga kitandani. Unabaki unajiuliza, huyu motto anajua kinachoendelea?


Zaidi ni kumuonea tu. Hastahili lawama hata kidogo. Nimetoa mfano huu baada ya mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Simba kung’oa viti ndani ya Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wakati timu hiyo inacheza na wageni wao Kagera Sugar na kutoka sare ya bao 1-1.


Mashabiki hao walifikia uamuzi huo baada ya Kagera kusawazisha bao dakika za lala salama kwa njia ya penati na kuwasononesha mashabiki hao wa wekundu wa Msimbazi.


Kitendo cha kung’oa viti uwanjani si cha kiungwana hata kidogo. Hakina faida zaidi ya hasara. Pia kinastahili kupingwa vikali na wote wanaopenda maendeleo ya kandanda.

Hakika siwezi kuvumilia. Kwanini hasira zetu za kufungwa au kutoka sare kuzimalizia katika uwanja? Viti vinakosea nini? Ndio vinachezesha mechi hiyo? Ndio mwamuzi? Huu ni ujinga.


Sisi mashabiki wa soka tunapaswa kujua kuwa mpira una matokeo matatu muhimu. Kwanza ni kufungwa, kutoka sare au kushinda. Hivyo moja wapo ya matokeo tunapopata ndani ya uwanja hakuna haja ya kukasirika.


Kama wachezaji hawajaonyesha kiwango kizuri basi tunapaswa kuwawajibisha wao na benchi la ufundi, lakini si kuvamia viti na kung’oa, maana ni uwendawazimu.


Imeniuma sana kuona kila siku tupo pale pale. Timu za Simba na Yanga zinashangaza sana. Hizi zinaamini wao ndio zenye sababu ya kushinda kwa kila mechi.


Huu si mtindo wenye matunda ya soka letu. Hatuwezi kusonga mbele hata kidogo. Mashabiki wa soka wanapaswa kufahamu hata wenzao nao wanastahili kushinda.


Kinachotakiwa ni mchezo mzuri wenye kujua mbinu muhimu za kukuza soka letu na sio kufanya uchafu ndani ya uwanja. Kung’oa viti na vitendo vingine si vya kiungwana.


Vinastahili kupingwa vikali. Kwanini kila siku Simba na Yanga ndio wanaongoza kwa uhuni? Kwani wao ndio nani hapa Tanzania? Kila timu imejipanga kucheza soka imara ili iweze kunyakua ubingwa wa Bara, hivyo mashabiki wanapaswa kufahamu hilo.


Hakuna haja ya kuumia kiasi cha kufikia kumaliza hasira zetu kwa viti ambavyo vimejengwa kwa kutumia gharama kubwa. Hivi kweli badala ya kuulinda uwanja wetu tunaubomoa?


Nani tunataka abebe hasara hizi? Na kama sababu ni mwamuzi, kung’oa viti ndani ya uwanja huo ndio aanachezesha vizuri? Hakika huu si mpango mzuri.


Unapaswa kupingwa vikali na kila anayependa maendeleo ya mpira wa miguu, hivyo kuna haja ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwa wakali zaidi katika hilo.


Mbali na TFF, hata sisi mashabiki wenyewe tulindane. Tunapomuona mmoja wetu anafanya uharibifu wa miundo mbinu ya viwanja vya michezo hatupaswi kumuangalia tu.


Tumzuie au kumfikisha sehemu husika ili wengine wasione haja ya kumaliza hasira zao za kufungwa au kutoka sare kwa kuipa hasara serikali juu ya viti ndani ya uwanja.


Kwani viti vinacheza namba gani? Viti ndio mwamuzi wa kati au kocha? Tuacheni ubabaishaji. Lazima tubadilishe mawazo yetu ili tuweze kusonga mbele, maana naona akili zetu zina matege.


Na ushabiki wa kuvunja viti umepitwa na wakati. Kule Ulaya timu inafungwa bao tatu na kuendelea, lakini mashabiki wanapiga makofi na kuimba muda wote.


Hapa kwetu timu ikifungwa au kutoka sare tunang’oa viti au kuwafungia safari wachezaji wetu na kuwashushia mvua ya matusi, ukichanganya na hasira za kung’oa viti ndio kabisa.

Hapana, hii siwezi kuvumilia.


+255712053949

No comments:

Post a Comment