Pages

Pages

Friday, October 18, 2013

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ahitaji mafunzo ya uongozi ili kuwa chachu kwa Tanzania na China

Na Mwandishi Wetu,  China
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kuwafaa makundi fulani ya viongozi ambazo zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji wao wa kazi hasa katika masuala yanayohusu sekta binafsi. 
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama vifaru na silaha nyingine za  kivita  wakati  alipotembelea   banda  la kunadi silaha mbalimbali  za kivita zinazotengenezwa na kampuni ya NORINCO  nje kidogo ya  Beijing akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 18, 2013.
Waziri Mkuu, Mizengo pinda akizungumza  baada ya  kutembelea kampuni ya  Aluminium Corporation of China , Beijing akiwa katika  ziara ya kikazi  nchini China Oktoba 18, 2013. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
Amesema taasisi hizo zinapaswa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP), zinapaswa kujua faida za ushirikiano huo na zinapaswa kubainisha ni sekta zipi zinapaswa kutekeleza mpango huo wa ushirikiano.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) wakati akifungua mafunzo ya siku 14 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali ya Tanzania yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
 
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji wa  Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) yameanza leo kwenye Chuo cha Uongozi cha China (China Governance Academy),  jijini Beijing, China.
Alisema Tanzania imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na ujenzi wa viwanda.
 
“Ni muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua jambo hili na kuchangia kwa juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa,” alisema.
 
Alisema kozi kama hizo zinapaswa kuwalenga watumishi kutoka taasisi za serikali pamoja na sekta binafsi na akazitaka taasisi hizo kuhakikisha zinaisaidia kuwepo kwa ufanisi wa hali ya juu kwenye ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma. 

“Muwasaidie  watu hawa waweze kutambua ni wakati gani ushirikiano wa aina hii unakuwa wa manufaa zaidi kwa wahusika, ni wakati gani wahusika wanafaidika na PPP, je wanakabiliwa na changamoto zipi, na wanafanyaje ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza,” aliongeza.
 
Alisema jambo lililo wazi kuwa ushirkiano baina ya wajasiriamali wa Kichina na wa Kitanzania utasaidia kuongeza fursa za kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na kuendeleza miundombinu. 

“Natambua kwamba kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa kutoka China ambao wako nchini Tanzania, hawa wanachangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania kwa kuingiza teknolojia mpya na kutoa fursa za ajira,” aliongeza.
 
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha aluminium cha China CHINALCO) na kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo.Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. 

Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.

Pia amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw.  Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na  Bw. Godfery Simbeye.

No comments:

Post a Comment