Pages

Pages

Wednesday, October 02, 2013

Mpira Pesa kukutana Oktoba 6 mwaka huu


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WANACHAMA wa klabu ya Simba wa tawi la Mpira Pesa, wanatarajia kufanya mkutano Mkuu Oktoba sita mwaka huu katika Ukumbi wa Anex Magomeni Mikumi, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Mkutano huo unafanyika kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu klabu yao wakiwa na lengo la kuhakikisha kuwa timu yao inafanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tawi hilo la Mpira Pesa, Ustadh Masoud, alisema kuwa maandalizi ya mkutano huo yanaendelea kwa ajili ya kuufanikisha kwa vitendo.

Alisema aidha pia watajaribu kuangalia namna gani tawi lao linaendelea kuwa na nguvu katika tasnia ya mpira wa miguu hapa nchini ili mambo yao yaende vizuri.

“Tawi la Mpira Pesa ni kati ya matawi yenye nguvu kwa klabu zote Tanzania, hususan Simba ambao tupo zaidi ya wanachama 500 na wenye mapenzi ya dhati na soka letu nchini.

“Tumeamua tufanye mkutano wetu ili tuangalie namna gani ya kuitumikia klabu yetu ya Simba kwa ajili ya kuendelea kufanya vyema katika soka na kuwa imara zaidi,” alisema.

Timu ya Simba ambayo ipo kileleni kwenye msimamo wa ligi, inaongozwa na mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, ambaye mara kadhaa amekuwa akiwarushia makombora wanachama wa Mpira Pesa kwa sababu mbalimbali na kuzua hofu kwa wanachama hao.

No comments:

Post a Comment