Pages

Pages

Wednesday, October 30, 2013

MGODI UNAOTEMBEA: Sakata la Mwigamba na ishara mbaya Chadema



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BAADA ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali nchini (PAC), Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alipotoa hoja juu ya vyama vya siasa kutokaguliwa, mengi yalisikika.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pichani.
Hasa ni pale viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia muda mwingi katika vyombo vya habari kukanusha na wengine kufika mbali kusema kuwa Zitto anapenda kujenga matukio ili kuweka juu jina lake.


Mwenyekiti wa Chadema Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba, pichani.
Kwa wale tunaomfuatilia Zitto kwa karibu tukagundua kuwa kuna kitu ndani yake na kingetokea mapema iwezekanavyo. Ikumbukwe kuwa, Zitto mbali na kuwa mwenyekiti wa PAC, pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kama kweli vyama siasa havijakaguliwa hususan Chadema, yeye pia yupo ndani ya chama hicho. Je, hoja yake zaidi ilitokakana na kutaka kuinyuka Chadema?

Najikuta najiuliza maswali hayo baada ya Chadema kumsimamisha Mwenyekiti wa mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa madai kuwa ametoa siri za chama chao hadharani.
Siri? Ni siri gani hizo zinazofichwa kiasi cha kuwataka watu wengine wa nje wasijuwe? 

Inashangaza mno. Ukijaribu kufuatilia suala hilo na kauli ya Zitto juu ya mahesabu ya vyama vya siasa yanafanana.
Mwigamba amemtuhumu Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk Willbroad Slaa juu ya mahesabu na matumizi yote ndani ya chama hicho.

Anafika mbali zaidi kwa kusema kuwa kipengele cha ukomo katika Katiba yao kimeondolewa kwasababu za watu wachache, akiwamo Mbowe na kundi lake.
Aidha anasema pia fedha nyingi zinachotwa bila kufuata utaratibu, jambo linaloashilia uwapo wa ufisadi usioweza kuvumiliwa na wanaokitakia kheri chama chao.

Inawezekana kuwa ni uongo, lakini ni vyema pia viongozi walioguswa wasimame na kutoa tamko. Lakini kumsimamisha Mwigamba bila kuelezea juu ya sakata lake ni kumuonea.
Yote anayosema Mwigamba, ni kuonyesha mapenzi ya dhati kwa chama kinachovuna ruzuku ya Watanzania, hivyo lazima kiendeshwe bila ubabaishaji.

Kwa mfano, Chadema ndio chama kinachojipambanua kuupinga ufisadi, hivyo nao lazima wawe wasafi. Mbowe anatajwa pia kuchota Milioni 80 kwa ajili ya kutengenezea kadi za chama hicho, jambo ambalo halijafanikiwa hadi muda huu.

Hata kama lingefanikiwa kupatikana kwa kadi hizo, lakini haikuhitaji kauli ya mtu mmoja kutoa amri na kupewa fedha hizo. Kwani sheria za manunuzi katika chama hiki zikoje?
Kuyasema haya kwa kipindi hiki ambacho baadhi yao wanaona Chadema ndio mkombozi wao kunahitaji moyo wa chuma kupita kiasi, ukizingatia kuwa wanaweza wakakuona unakichukia.

Mara kadhaa watu hao hawataki ukweli. Wakielekezwa jambo wanaona wanasemwa na eti hawastahili kukosolewa hata kidogo. Hii sio haki kwa Chadema kinachoongozwa na binadamu.

Chadema hakiongozwi na malaika. Nao ni binadamu, hivyo kukosea kwao ni jambo la kawaida, hivyo inapotokea wanashauriwa basi hakuna haja ya kuchukia.
Ni kweli Chadema ni chama kilichopata umaarufu miongoni mwa Watanzania kiasi cha kuwa chama Kikuu cha upinzani kwa sasa, kikiipoka nafasi hiyo Chama Cha Wananchi (CUF).

Angalia, kama leo chama kama Chadema hakuna mtu anayejua hivi fedha za chama zinatumikaje zaidi ya watu wachache, yani Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha, unafikiri nini hatima yake?

Kama maamuzi ya vikao hayaheshimiki isipokuwa ya wale watu wachache, ni mwelekeo mzuri kwa chama hicho cha upinzani? Ifahamike kuwa Chadema wana vuna fedha nyingi za rukuzu, ndio maana tulishuhudia wanavyopiga kelele baada ya kuitwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali, PAC, chini ya Zitto.

Mwigamba anasema; “baada ya uchaguzi wa 2010 vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015, lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha.

“Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje, pamoja na maamuzi ya kikao cha Baraza kuu cha mwezi Januari kilichoamua kwamba kiasi cha fedha inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya na majimbo na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda, ingawa sasa ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa ipasavyo.” Ilisema taarifa hiyo ambayo hata hivyo ilikuwa ngumu baada ya kusimamishwa.

Nafikiria Chadema wanajidanganya katika suala hili kwakuona kuwa wakimsimamisha Mwigamba ndio njia ya kutuliza moto huu ulioanza kufukuta. Najua ndio hatua hii ni sababu ya mvutano wa nafasi za uongozi za Chadema.

Lakini njia ni kukaa chini na kuangalia lipi tatizo. Uwekwe mfumo mzuri wa kiutawala kwa chama hicho kinachojiona ni kisafi. Chama kinachoona kinastahili kushika dola na kuwaongoza Watanzania.

Inashangaza kuona mambo mabaya kama haya yakiendelea kutokea ndani ya Chadema. Hii inaweza kuchukukuliwa kama tahadhari kwa ajili ya kukijenga na kukiimarisha zaidi. Ni juzi tu wanachama wawili waliondoka, akiwamo Juliana Shonza na Mtela Mwampamba ambao wote kwa pamoja walikimbilia kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa wanaofuatilia mambo ya siasa wanakubaliana na mimi kuwa kuondoka kwa wanachama hao na maneno waliyokuwa wanayatoa yanajibu hoja juu ya Chadema kuendeshwa na kikundi cha watatu wasiozidi watatu.

Japo unaweza kuona ni masihala, lakini kwa chama kama Chadema, Chama Kikuu cha Upinzani, kuondoa kipengele cha kinachomzuia kiongozi kukaa madarakani kwenye nafasi moja zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Hii ni kwa mujibu wa tamko la Mwigamba, ambapo alisisitiza kuwa wakati wanafanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hawakugusa kipengele hicho, hivyo wakati Katiba hiyo inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela.

Nadhani hapa kuna haja ya kuliangalia kwa kina jambo hili. Halipaswi lipite hivi hivi. Kama Chadema wamekuwa wakipigia kelele ufisadi wa viongozi wengine hasa waliokuwa ndani ya serikali ya CCM, hata wao wanapaswa kunyooshewa vidole.

Na ndio maana wameona njia muafaka kwao ni kumsimamisha Mwigamba, wakisema ametoa siri, hali ya kuwa hawataki kilichopo ndani ya chama chao kionekane nje kwasababu za heshima ya chama chao.

Hiki si kitendo kidogo hata kidogo. Kinapaswa kuchunguzwa kwa kina, na endapo kitaonekana ni kweli, basi viongozi wa juu wa Chadema, akiwamo Mbowe, Slaa wanapaswa kujiuzuru kwa heshima ya kodi za Watanzania.

Pamoja na kujiuzuru huko, pia ni wakati wa Watanzania wote kukipiga jicho chama hiki kinachopigana usiku na mchana ili kishike dola. Huu ndio ukweli wa mambo. Unapaswa kuangaliwa kwa kina.

Bila kuangalia hisia juu ya chama hiki, ila ni dhahiri kuwa kuna siku viongozi hao hao wanaweza kufanya mambo mabaya zaidi, ukizingatia kuwa wanaonekana ndio wenye sauti na hawawezi kukoselewa na mtu yoyote.

Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya siasa, kadhia hii na mvutano huu unasababishwa na joto la wanaohitaji nafasi hizo, hasa ya uenyekiti ambapo Mbowe sasa amejihalalishia kuongoza hadi atakapotaka mwenyewe, ukizingatia kuwa kipengele hicho kwenye katiba yao hakipo baada ya kuchomolewa kienyeji.

Kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti na kama ni kweli basi sakata hili ni zaidi ya udikteta, hivyo wenye chama chao lazima wahoji.

Mimi ni miongoni mwa Watanzania wanaopenda kuhoji mambo mbalimbali ya vyama vya siasa, wakiwamo Chadema. Japo wakati mwingine napata wakati mgumu, lakini ukweli unaonekana wazi wazi juu ya mwenendo huu mbaya.

Ni vyema viongozi wa Chadema wakajibu hoja hizi ili kutuliza mawazo na mfadhaiko juu ya wanachama wao na wafuasi wao.
Mungu ibariki Tanzania.
+255712053949

No comments:

Post a Comment