Pages

Pages

Monday, October 14, 2013

Kigoda aahidi kulisaidia Tamasha la Utamaduni Handeni

Na Mashaka Mhando, Handeni
MBUNGE wa Handeni  Dkt Abdallah Kigoda, ameaahidi kushirikiana na kuwasaidia waandaaji wa Tamasha la Utamaduni na Michezo lililopewa jina la ‘Handeni Kwetu’ litakalofanyika Desemba 14 mwaka huu mjini Handeni, mkoani Tanga, ili kuunga mkono jitihada za wadau katika suala zima la utamaduni na maendeleo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, ambaye pia ni Mbunge wa Handeni.

Akizungumza wakati akizindua kisima cha maji katika soko la zamani lililopo katika mji wa Chanika, Dkt Kigoda, alisema anaunga mkono tamasha hilo ambalo litaibua fikra na mtizamo mpya wa utamaduni miongoni mwa wananchi wilayani hapa.

“Waandaji wa Tamasha la Utamaduni wamenipa taarifa za kufanyika tamasha hilo nami kama mbunge wa jimbo hili sina budi kuwaunga mkono kufanikisha tamasha hilo na nitashirikiana nao,” alisema Dkt Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.

Dkt Kigoda alisema suala la utamaduni ni suala mtambuka ambalo linagusa mioyo ya wananchi wengi hivyo unapoweka tamasha kwa ajili ya utamaduni wa ngomalicha ya kuwapa burudani wananchi hutoa hamasa kwa vijana kupenda mila na utamaduni hasa suala na ngoma za asili.

Mbunge huyo alitoa wito kwa wananchi wilayani humo na wale waliopo nje ya handeni kujitokeza kushiriki tamasha hilo ili kuibua mawazo mapya juu ya masuala ya utamaduni na michezo yaliyokosa msisiko kutokana na kutopewa kipaumbele.

Mbunge huyo, aliahidi kusaidia tamasha hilo baada ya kupewa taarifa na mwandaaji wake Kambi Mbwana.

Wadhamini waliothibitisha kushiriki katika tamasha hilo ni pamoja na Phed Trans inayomilikiwa na Yusuphed Mhandeni, Grace Products, Screen Masters, Dullah Tiles $ Construction Ltd, Katomu Solar Specialist na Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.

Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, SmartMind & Partners chini ya ANESA COMPANY LIMITED, ikidhamini kwa kupitia kitabu cha ‘NI WAKATI WAKO WA KUNG'AA, Screen Masters, Saluti5.com, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu Blog.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo alisema kuwa wataalamu wanafanya utafiti kwa ajili ya kuchimba kisima katika uwanja wa mpira wa Azimio ambao unakarabatiwa ili uweze kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu na klabu ya Mgambo JKT.

Alisema tayari ametoa kiasi cha shilingi milioni 250 kutoka katika mfuko wake wa maendeleo ya jimbo ili kuukarabati uwanja huo ambao tayari umeoteshwa nyasi mpya na kujengwa vyumba vya kubadilishia ngu wachezaji pamoja na jukwaa kuu.

No comments:

Post a Comment