Pages

Pages

Tuesday, October 22, 2013

DRFA yaomboleza msiba wa Jimmy Mhango

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimetuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, Jimmy Mhango aliyefariki jana (Oktoba 21, 2013)  katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kutokana na presha.

Katibu Mkuu wa DRFA Msanifu Kondo amesema leo (Oktoba 22) kwamba wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mjumbe huyo, ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji mahiri katika timu ya Ushirika ya Moshi katika miaka ya tisini chini ya Kocha Dan Korosso.

Marehemu pia aliwahi kuzichezea timu za Pan Africans ya Dar es Salaa pamoja na timu ya Mkoa wa Kilimanjaro ‘Kilimanjaro Stars.

“DRFA imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Jimmy Mhango na inatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na wanafamilia wote wa mpira wa miguu, tunawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya DRFA ambayo marehemu alikuwa mjumbe, inaongozwa na Roman Masumbuko (Mwenyekiti), Fahadi Kayuga (Makamu Mwenyekiti), Mohamed Mpili (Mjumbe) na Peter Nkwera (Mjumbe).

Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Jumanne)katika makaburi ya Ilala Mchikichini, Dar es Salaam saa kumi jioni.


No comments:

Post a Comment