Pages

Pages

Wednesday, September 11, 2013

MGODI UNAOTEMBEA: Nashangaa malumbano na mnyukano huu wa CCM



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI wazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio chama kikongwe na chenye historia kubwa na Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Tangu Uhuru, wakati Tanzania ipo chini ya chama kimoja na sasa vyama vingi, CCM imefanikiwa kwa miaka kadhaa kuunda serikali kwa kutoa Rais wa Bara na Visiwani.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, akisalimiana na wanachama wa chama hicho katika moja ya matukio yake ya kisiasa.

Ni CCM ndio iliyoiweka nchi katika hatua hii nzuri ya kuungwa mkono ndani na nje ya mipaka yetu. Waswahili wamesema, mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni. CCM pamoja na mapungufu kadhaa yanayosemwa na baadhi yao, ila imefanya mengi mazuri.


Mbunge wa Monduli na Kada wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa, ni moja ya wanachama wanaotajwa sana katika mbio za urais mwaka 2015.

Ni kutokana na hilo, muasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kuelezea umuhimu wa serikali ya CCM kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, naye ni miongoni mwa makada wa CCM wenye nguvu kubwa na ushawishi wa aina yake.

Bila kuficha, Nyerere alisema wazi kuwa bila CCM imara, nchi itayumba. Ni kauli nzuri inayoendelea kukumbukwa hadi wakati huu. Mara kadhaa CCM imekuwa ikifanikiwa kutoa rais na kuunda serikali kwa ujumla wake.

Kwa wale wanaopingana na suala hili; wanapaswa kukaa na kuwaza haya machache kabla ya kutoa uamuzi wa kukichukia chama hiki kikongwe. Mosi; kwanini CCM imekuwa ikichanganya vichwa vya Watanzania kila inapofikia chaguzi zake za ndani?

Kwanini ni wagombea urais wa CCM pekee wamekuwa na mguso na kuangaliwa sana kiasi cha kuumiza watu wengine mtaani? Hawa wengine wa upinzani wapo wapi, wanafanya nini? Angalia, licha ya kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika tena mwaka 2015, lakini ni makada wa CCM na baadhi ya viongozi wanaotajwa zaidi kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Watu kama vile Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Samuel Sitta, Dkt Asha Rose Migiro na John Magufuli, hawa wanatajwa mno kuwa wana mipango ya kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa kwa sasa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Ukiacha hao, pia wapo vijana wachache akiwamo Naibu Waziri wa Sayansi na Technology, January Makamba anayetajwa katika nafasi hiyo, bila kuangalia kuwa umri wake bado haumruhu kuwania kiti hicho.

Sio kama hakuna wengine wanaotajwa katika nafasi hiyo, hasa kutoka vyama vya upinzani, akiwamo Dk Willbroad Slaa kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kutoka Chama Cha Wananchi (CUF), ambao pia waliwania nafasi hiyo Uchaguzi wa  mwaka 2010.

Ndio hao wanatajwa, ila si kama wanavyotajwa makada wa CCM. Kila mtu ndani na nje ya nchi amekuwa akitumia muda mwingi kuangalia majina hayo. Hii ni kwasababu wanatokea katika chama kikongwe na kinachokuwa na nafasi kubwa yaa kutoa rais wan chi kwa miaka kadhaa ijayo.

Ni chama kilichowafanyia mema Watanzania tangu Uhuru. CCM iliyozaliwa mwaka 1977, imeitoa Tanzania katika vipindi tofauti mno. Hata kama mabaya yake yapo na wachache wao wanayajadili, ila kwakuwa ndani yake kuna mazuri, basi ni vyema tukawa wepesi pia kuyaweka mbele.

Pamoja na hayo, ila ni wakati sasa wa kuangalia namna gani viongozi wa serikali kutoka CCM, viongozi wao wa chama na makada kwa ujumla kujaribu kutafakari hayo ili iwe njia yao ya kubakia madarakani.

Watanzania tunahitaji maendeleo. Na hapana shaka maendeleo hayo yataendelea kupatikana kutokana na uzalendo, ushirikiano kutoka kwa watu wote, wakiwamo viongozi wanaotoka CCM.

Huwezi kukwepa mazuri ya Tanzania yaliyopatikana ndani ya utawala wa serikali ya CCM, inayoongozwa na Kikwete. Sasa katika mikoa mbalimbali kumeunganishwa barabara za lami.

Sera nyingi zinazotekelezeka zimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa hili. Miaka ya 2005 kushuka chini ilikuwa kazi kupata shule ya kusoma elimu ya sekondari. Leo hii kila Kata kumejengwa shule.

Zamani mtu anayesoma Chuo Kikuu alionekana ni wa ajabu sana au pia kuonekana tajiri. Lakini hii Vyuo Vikuu na vinginevyo vimeendelea kujengwa katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya watoto wa Tanzania kuipata elimu ya juu.

Haya na mengine ni maatunda ya CCM. Ni vyema tukayatambua na kuyaheshimu ili iwe nafasi ya kutafuta mengine hata kwa vyama vya upinzani kama wanavyohitaji baadhi yao, ukizingatia kuwa hii ni nchi ya demokrasia.

Tunajua wapo wanaohitaji vyama vingi, ila si sababu ya kutufanya tuponde na kuchukia kila jema linalofanywa na CCM, ati kwasababu ni chama tawala. Kama hivyo ndivyo, hawa viongozi wa CCM wanafanya nini?

Kuanzia viongozi wa matawi hadi Taifa wanajua thamani yao? Wanafahamu ni namna gani wanapaswa kulitumikia Taifa na wananchi wao ili mazuri yao yawe mbeleko leo na hata kesho pia?

Wakati nasema haya, natambua kuwa katika sehemu nyingi za nchi yetu, Bara na Visiwani kumekuwa na msuguano wa aina yake kwa viongozi wa ndani ya CCM. Kila mara kumekuwa na msuguano unaotishia uhai wa CCM.

Utakuta Meya anasuguana na mbunge wa jimbo husika. Kama hivyo haitoshi, wakati mwingine diwani kumenyana na mwenyekiti au Katibu wa CCM na pengine msuguano huo kuingia hadi kwa Mkuu wa Wilaya na kuharibu kabisa ufanisi katika maeneo hayo, maana linapotokea huwakumbuka watu wengi.

Ni juzi tu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Taifa, Kikwete, alipowataka Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Khamis Kagasheki kumaliza mgogoro wake na Meya wa Kagera, Anatory Amani, ambaye naye anatoka kwenye chama hicho kikongwe Barani Afrika.

Mgogoro wa viongozi hao ulisababisha kuzaliwa kwa makundi yasiyokuwa na tija kwa serikali na chama kwa ujumla, hasa baada ya kuibua malumbano kutoka chini hadi juu, huku kila mmoja akiona yupo sahihi.

Akiwa mkoani Kagera, Kikwete aliwataka watu hao wamalize mzozo wao kwa sababu za kuijenga nchi inayoongozwa na CCM. Hata hivyo, hayo yalikolezwa pale madiwani nane wa CCM kuvuliwa uanachama mkoani humo.

Madiwani hao waliofukuzwa ambao baadaye walitetewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyepinga uamuzi wa viongozi wa chama Kagera ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).

Ingawa Kamati Kuu ya CCM iliwaita tena mahasimu hao, yani Kagasheki na Amani ili waangalie tatizo lililopokuwa, ila bado msuguano huo upo na umeenea katika maeneo mengi ya Tanzania.

Kwa bahati mbaya, matokeo hayo mara kadhaa yamekuwa machungu kwa CCM,  hasa pale vyama vya upinzani vinapogeuka kuwa fisi anayesubiri mifupa. Mara baada ya madiwani hao kufukuzwa kama ilivyotangazwa na CCM mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe aliibuka na kuwaita wajiunge na chama chao.

Mbowe alizungumza mengi, hasa madai ya ufisadi unaofanywa na Amani, hivyo kuwakera madiwani hao wa CCM. Hii ni nzuri, ila nathubutu kusema kuwa maneno ya Mbowe yamekuja huku yakionyesha kuwa inategemea zaidi mnyukano huo ili iwe tija kwao.

Sio mbaya pia, ila lazima viongozi wa CCM wenyewe wafahamu kuwa wao ndio kila kitu kwa chama chao. Msemo wa vita vya panzi faida ya kunguru unaweza kuchukua nafasi kubwa katika kadhia hii.

Bado vyama vya upinzani haviwezi kufanya vizuri bila kuhitaji Baraka kutoka kwa makada au viongozi wa CCM. Hivyo sitaona ajabu hata leo Mbowe akamuita Lowassa, Membe, Sitta na wengineo akiamini kuja kwao hao ni faida kwa Chadema, ukizingatia kuwa miamba hiyo itakuja na watu wao.

Katika mchezo wa siasa, hakuna mwanasiasa mdogo. Diwani mmoja tu alitepita kwa haki na ambaye ni chaguo la wananchi wake, basi ni wazi kuwa akihamia upinzani, bado anaweza kutetea nafasi yake hiyo.

Kama hivyo ndivyo, diwani aliyefukuzwa ndani ya CCM akahamia Chadema au CUF, nafasi ya kutetea nafasi yake ni kubwa, hivyo Kata hiyo itapotea. Je, CCM matawi, Kata, Wilaya na Taifa wanafahamu hili?

Naheshimu mno busara za Kikwete katika kukiendesha chama cha CCM, akiamini kuwa yeye ndio dreva wa kuliongoza jahazi hili. Ni CCM tu yenye mamlaka ya kuunda serikali ya kuwaongoza Watanzania.

Kwa bahati mbaya, CCM hii imekuwa na mnyukano wa kila wakati, hivyo ni wakati wao sasa kukaa chini kwa ajili ya kukijenga chama chao. Mwaka 2014, ikiwa ni miezi michache kutoka sasa itaingia kwenye Uchaguzi wa serikali za mitaa.

Uachaguzi huo ni muhimu kuliko hata ule wa ndani ya chama. Ni kipimo kikubwa kuonyesha CCM ya miaka mitano ijayo itakuwaje. Kama CCM itaanguka kwenye mitaa mingi, basi matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 yatashangaza wengi.

Lakini kama ikifanikiwa kushika serikali za mitaa kama kawaida yake, basi viongozi hao watakaochaguliwa na wananchi, wakawa ni machaguo yao halisi, wakawatumikia kama inavyotakiwa, kwanini wasiwaunge mkono kwenye Uchaguzi Mkuu?

Hatuhitaji uchakachuaji wala mihemko ya kisiasa. Tunahitaji busara, unyenyekevu na moyo wa uzalendo kwa ajili ya Watanzania wote. Hayo yakifanyika kwa mikono miwili, hata hayo maisha bora kwa kila Mtanzania yapatikana.

Na kama yakipatikana kwa vitendo na sio maneno ya kisiasa, sasa kwanini watu waichukie serikali ya CCM wakati inawapatia kila wanachohitaji? Haya ni mambo yanayotakiwa yawekwe vichwani mwa viongozi wote wa CCM.

Viongozi hawa wanaowezo mkubwa wa kuwasimamia watendaji wengine wa serikali kwa ajili ya kusimamia sera na utekelezaji wote uliokusudiwa kwa ajili ya kuwaongoza vyema wananchi wanaounda serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huu ndio ukweli na kuna kila sababu ya kuangalia nyendo zote zenye tija, maana CCM wasipokuwa makini, suala hili la mnyukano litawaathiri.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment