Pages

Pages

Sunday, September 29, 2013

CCM Handeni wajipanga kuvunja ngome zote za Chadema wilayani humo



Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilayani Handeni mkoani Tanga, Athumani Malunda amesema kwamba wataendelea kujipanga ili wavunje ngome zote zinazotumiwa na vyama vya upinzani hasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Handeni, Athumani Malunda.
Malunda aliyasema hayo siku chache baada ya kufanikiwa kuvunja ngome za Chadema katika vijiji kadhaa kikiwamo Kwamatuku ambapo zaidi ya wanachama 380 walirudi CCM.

Akizungumza wilayani hapa juzi, Malunda alisema kuvunja kwa ngome za Chadema ni hatua ya kukiimalisha chama chao Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Alisema japo CCM haina wasiwasi na Handeni kutokana na kuheshimika kwa kiasi kikubwa, ila bado wanashawishika kuondoa dosari mbaya za kuzaliwa kwa upinzani wilayani humo.

“Juzi tulishuhudia mamia ya wafuasi wa Chadema wakirudi tena CCM kwa kasi ya ajabu, hivyo sisi kama viongozi tumejipanga kupokea wanachama wengine kwa ajili ya kurudi nyumbani.

“Tupo imara na tumejipanga imara kusimamia ilani ya Uchaguzi sanjari na kuleta maendeleo kwa Watanzania wote, jambo linaloweza kuwapa imani dhidi ya chama chao kinachopendwa na kukubalika,” alisema.

Matokeo ya kurudi CCM kwa wanachama na viongozi wa upinzani wilayani Handeni yanazidi kushika kasi siku hadi siku jambo linaloonyesha kuwa vyama vya upinzani vinazidi kupoteza dira.

No comments:

Post a Comment