Pages

Pages

Wednesday, August 14, 2013

Uchaguzi Mkuu wa TFF waiva, fomu kuanza kutolewa Agosti 16

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa tangazo la uchaguzi wa Kamati ya mpya ya Utendaji ambao utafanyika Oktoba 20 mwaka huu. Pia Kamati hiyo imetoa tangazo za uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPL Board) ambao utafanyika Oktoba 18 mwaka huu.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Akitangaza mchakato huo wa uchaguzi leo (Agosti 14 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hamidu Mbwezeleni amesema nafasi zitakazogombewa kwa upande wa TFF ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.

Fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia Agosti 16 mwaka huu kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 kamili jioni kwenye ofizi za TFF. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti 20 mwaka huu. Fomu kwa nafasi ya Rais ni sh. 500,000, Makamu wa Rais ni sh. 300,000 wakati wajumbe ni sh. 200,000.

Mbwezeleni amesema kwa wale ambao walilipia fomu katika mchakato uliofutwa na wanakusudia kugombea nafasi zilezile walizolipia, hawatalipia tena ada ya fomu husika bali watatakiwa kuambatanisha risiti za malipo wakati wa kurudisha fomu za maombi hayo ili kuthibitisha malipo yao.

Kwa upande wa uchaguzi wa TPL Board, fomu zitaanza kutolewa Agosti 16 hadi 20 mwaka huu, na nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambapo ada ni sh. 200,000 wakati wajumbe wa Bodi ada ni sh. 100,000.

Aidha, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokuwa ikutane jana (Agosti 13 mwaka huu) na leo (Agosti 14 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza sasa itakutana keshokutwa (Agosti 16 mwaka huu) saa 4 asubuhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Alex Mgongolwa amepanga tarehe hiyo mpya baada ya kikao cha jana kushindwa kupata akidi. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ina wajumbe saba, na ili kikao kiweze kufanyika ni lazima wapatikane wajumbe kuanzia wanne.

No comments:

Post a Comment