Pages

Pages

Thursday, August 22, 2013

Maafisa wanne wa polisi wapoteza ajira zao baada ya kusimamishwa kwa kukiuka maadili ya Jeshi la Polisi

pic 2
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua  ya kuwavua madaraka Maafisa wanne wa Jeshi la polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja kutokana na kukiuka maadili na taratibu za Jeshi la Polisi.

Na Lydia Churi, MAELEZO

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka Maafisa wanne wa Jeshi la Polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja ambaye atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na taratibu za jeshi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Waziri Nchimbi amesema hatua hiyo ni katika kuendeleza vita ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na nidhamu, linatekeleza wajibu wake wa kutenda haki na kuwalinda raia na mali zao.

Alisema amewachukulia hatua Maafisa hao baada ya kuridhia maoni ya kamati aliyoiunda kufanya uchunguzi wa matukio yaliyolalamikiwa dhidi ya askari polisi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma kati ya Desemba 2012 na Mei, 2013.

Waziri Nchimbi aliwataja waliovuliwa madaraka kuwa ni Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani Arusha Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Dumila Inspekta Juma Mpamba na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kasulu ASP Daniel Bendarugaho na kumsimamisha kazi Inspekta Isaack Manoni.

Alifafanua kuwa  Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro alivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maafisa walio chini yake ambao walikamatwa wakisafirisha bangi yenye uzito wa kilogramu 540 kwa kutumia gari la polisi.

Alisema askari hao wawili waliokamatwa wakisafirisha bangi, walikuwa wakifanya kazi kwenye kituo cha Ngarananyuki na baada ya kukiri kosa walifukuzwa kazi mwezi Mei mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Inspekta Jamal Ramadhan amevuliwa madaraka yake kwa kutochukua hatua stahiki baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara wa Mvomero Samson Mwita kubambikiwa fuvu la kichwa cha binadamu na askari polisi watatu wakishirikiana na matapeli wawili.
“Katika tukio hilo Inspekta Isaack Manoni amesimamishwa kazi na atashtakiwa kijeshi kutokana na tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa, Cpl. Edward aliyekuwa dereva wa gari la Polisi lililokamatwa na bangi kitendo ambacho kimelifedhehesha jeshi la polisi” alisema Waziri Nchimbi.

Alibainisha kuwa Inspekta Juma Mpamba amevuliwa madaraka hayo kwa kuonesha udhaifu katika utendaji wake wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari walio chini yake kitendo kilichosababisha askari kujipangia kazi nje ya utaratibu na kumbambikiza mfanyabiasha huyo kesi kwa lengo la kujinufaisha kinyume na maadili ya kazi. Aliongeza kuwa askari waliohusika na tukio hilo wamefukuzwa kazi na kushtakiwa.

Waziri Nchimbi alisema ASP Daniel Bendarugaho amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini katika kufanya na kusimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ya marehemu Gasper Mussa Sigwavumba aliyeuawa baada ya kupigwa na askari polisi wawili Desemba mwaka jana.

Alisema upelelezi mbovu uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu huyo wa upelelezi ulisababisha kesi hiyo kuondolewa mahakamani. Aliongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo utaanza upya ili haki itendeke.

No comments:

Post a Comment