Pages

Pages

Saturday, July 06, 2013

Vijiji 17 wilayani Handeni kuchimbiwa mabwawa kukabiliana na shida ya maji



Na Mwandishi Wetu, Handeni
NEEMA imeanza kuonekana katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, baada ya kupata ufadhili kutoka Benki ya Dunia (WB), kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa mabwawa ya maji katika vijiji 17 vilivyoko wilayani hiyo ili kupambana na tatizo la shida ya maji.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Hayo yameelezwa na Mkurungezi wa Halmashauri hiyo, Dk. Khalfany Haule wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2012/2013, kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika wilayani hapo, huku ukiwa ni mpango mzuri kwa wilaya hiyo.

Alisema pamoja na ujenzi huo, vijiji viwili vya Misima na Gendagenda vimepata ufadhili wa Sh milioni 360 kutoka Shirika la Chakula na Kazi la Japan kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili.  Ujenzi unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Haule aliongeza kuwa, Shirika la DANIDA limeweza kufadhili ujenzi wa visima virefu sita katika vijiji vya Manga, Mkata Mashariki, Mkata Magharibi, Kwamkonga, Kwedizinga na Michungwani.

“Licha ya ufadhili wote huo, halmashauri yetu bado inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa mitambo ya kusukuma maji na ukosefu wa umeme wa uhakika pamoja na wizi wa miundombinu hiyo unaofanywa na wananchi,” alisema Haule.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ramadhani Diliwa, aliwataka madiwani kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa miradi hiyo pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji ili wasiviharibu na kusababisha tatizo kuwa kubwa.

No comments:

Post a Comment