Pages

Pages

Thursday, July 25, 2013

Mlemavu Saada Khamis Hamad wa Visiwani Pemba apewa msaada wa baiskeli maalum ya walemavu


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa mashindano ya kuhifadhi Quran kitaifa Abdallah Said, Saada Khamis Hamad na Aisha Sururu.
TAASISI ya Aisha Sururu, imetoa msaada wa baiskeli maalum kwa mtoto
mlemavu, Saada Hamis Hamad (14), ambaye ni mshindi wa kwanza, kundi
maalum, katika mashindano ya kuhifadhi Quran Tukufu, kitaifa.

Saada ambaye mikono na miguu yake imelemaa, alikabidhiwa baiskeli hiyo
juzi jioni, na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aisha Sururu, ambapo alisema ina mahitaji muhimu kwa mtu mwenye ulemavu, ikiwemo sehemu ya kujisaidia.

Akizungumza mara baada ya kupokea baiskeli hiyo, aliishukuru taasisi
kwa kumsaidia kwa mambo mengi, ikiwemo kuibua kipaji chake cha
kuhifadhi Quran na kumsafirisha kwa mara ya kwanza.

Alisema tangu apate akili, amekuwa akijisaidia kwa tabu bila staha na
kwamba kupitia baiskeli hiyo, itamsaidia mambo mengi ikiwemo kuzunguka maeneo mbalimbali, ambapo hapo awali alishindwa kwani ili kutoka sehemu moja kwenda nyingine ilikuwa lazima abebwe.

"Kabla ya hapo nilikuwa nipo tu nyumbani, sikuwahi kupelekwa shule
wala kutoka nje ya mji wangu, lakini nashukuru nimejifunza mengi na
nimepata msaada huu,"aliongeza Saada.

Mtoto huyo, ambaye ni mkazi wa Mamoja, Pemba, alisema kuwa, ana ndugu zake wanne, ambao wawili kati yao ni walemavu kama yeye isipokuwa kaka yake wa kwanza ambaye alizaliwa akiwa mzima wa viungo.

Aisha, ambaye pia ni diwani wa viti maalum Ilala, aliwataka wahisani
wengine kujitokeza na kununua baiskeli mbili kwa ajili ya ndugu zake
Saada hasa mdogo wake ambaye anasoma chekechekea.

"Mdogo wake amekuwa akibebwa kwa ajili ya kupelekwa shule na
kuridishwa nyumbani, hivyo baiskeli hiyo itapunguza adha na kumsaidia
kuhudhuria masomo bila wasiwasi,"aliongeza.

No comments:

Post a Comment