Pages

Pages

Friday, July 19, 2013

DC Muhingo azindua mashine za EFD wilayani Handeni, mkoani Tanga


Na Kambi Mbwana, Handeni
MKUU wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, juzi alizindua sehemu ya pili ya matumizi ya ulipaji wa kodi kwa kutumia mashine ya Electronic Fiscal Device (EFD) wilayani hapa.

Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, akizungumza katika uzinduzi wa mashine za electronic za ukusanyaji wa kodi za bidhaa mbalimbali mjini Handeni juzi. Kulia kwake ni Meneja Msaidizi wa TRA Mkoani Tanga, Martenus Shirima na kushoto ni Meneja wa TRA Handeni, Charles Kamuhanda. Picha na Kambi Mbwana.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na wafanyabiashara mbalimbali pamoja na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Handeni, Charles Kamuhanda na Meneja Msaidizi wa Mkoa wa Tanga, Martenus Shirima.


Akizungumza katika uzinduzi huo, DC Muhingo alisema kuwa mashine hozo za kulipia ushuru kieletronic ni nzuri, huku zikiweza kuhamasisha pia matumizi ya kudai risiti.

Alisema mpango huo ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete na kuwataka wakuu wa wilaya kusimamia matumizi hayo, ni mpango pia unaoweza kukusanya kodi kwa wafanyabiashara.

“Sisi Handeni kwa pamoja tunazindua matumizi haya ya mashine za electronic za kulipa kodi ya bidhaa, huku nikiamini kuwa kila mwananchi atalifanyia kazi.

“Wafanyabiashara wote wanunuwe mashine hizi na kuzitumia kwa ufanisi, huku sisi wateja tunaponunua bidhaa lazima tudai tiketi ili kulifanya jambo hili liwe na tija,” alisema DC Muhingo.

Naye Meneja wa TRA Wilayani Handeni, Kamuhanda, alisema matumizi hayo ya mashine za electronic yana tija kwa watu wote, wakiwamo wafanyabiashara.

Alisema juu ya wizi unaoweza kutokea kwa wanaoachiwa biashara husika unaweza kukomeshwa kama mashine hizo zitatumiwa kikamilifu na kila mmoja kudai risiti.

“Tunapofanya uhakiki wa biashara zetu, basi mashine hizi zinaweza kutoa ukweli wote wa bidhaa zilizouzwa kwa siku, wiki, mwezi hata mwaka mzima, hivyo ni namna gani mpango huu ni mkombozi kwa wadau wote pamoja na Taifa kwa ujumla.

“Ni wakati wetu sasa kuingia kwenye matumizi haya ambayo kwa kiasi kikubwa pia yataongeza ulipaji wa kodi hasa kwa wale wafanyabiashara wasiopenda kulipa kodi,” alisema.

Katika uzinduzi huo, wafanyabiashara wa wilaya ya Handeni walipewa elimu ya matumizi hayo ya mashine kutoka kwa wafanyakazi wa TRA pamoja na Kampuni zinazosambaza mashine hizo.

No comments:

Post a Comment