Pages

Pages

Tuesday, June 04, 2013

Sipati picha wabongo wataupokeaje mwili wa marehemu Mangwea utakapowasili leo Tanzania kwa ajili ya mazishi yake mkoani Morogoro

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWILI wa marehemu Albert Mangwea, unawasili leo ukitokea nchini Afrika Kusini, Shirikisho la Muziki Tanzania, likitangaza kuwa kila kitu kinakwenda vizuri kwa ajili ya kuuhifadhi kwenye nyumba ya milele.

Mwili wa Ngwea ukiwa tayari kwa kuagwa jana Afrika Kusini

Jeneza la NgweaNgwea alifariki nchini Afrika Kusini Jumanne ya wiki iliyopita na kalenda ya uletwaji wa mwili huo kuanza, hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa maziko yake.

                             Marehemu Ngwea enzi za uhai wake.
Mangwea akiletwa leo jioni, basi kesho Jumatano ataagwa katika viwanja vya Leaders Club, wakati saa sita mchana safari ya kuelekea mkoani Morogoro itaanza, huku mazishi yake yakipangwa kufanyika kesho au siku ya Alhamisi.


Akizungumza na Handeni Kwetu Blog leo asubuhi, jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo Novemba, alisema kuwa endapo mwili huo utafika leo Jumanne, basi maziko yake yatafanyika siku ya Alhamis, Kihonda, mkoani Morogoro.


Aliwataka Watanzania kuendelea kuwa wavumilivu katika msiba huo sambamba na kumuombea marehemu aletwe Tanzania kwa ajili ya kuzikwa katika ardhi ya nchi yao.


"Mara kadhaa ujio wake umekuwa ukivunjika kwasababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu, ila tumehakikishiwa kuwa kesho leo Jumanne mwili wa ndugu yetu utawasili hapa nchini.


"Akishaletwa leo, basi mwili wake utalala katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi asubuhi ya siku ya Jumatano ambapo utaagwa mpaka mchana safari itakapoanza kuelekea Kihonda, mkoani Morogoro, ambapo mazishi yake yatafanyika,” alisema Novemba.

Msiba wa Ngwea umepokewa kwa masikitiko makubwa, huku ripoti ya kifo chake ikishindwa kuweka bayana, hivyo kuzua hofu miongoni mwa wadau na mashabiki wa muziki Tanzania.
Aidha, jana mwili huo uliagwa na Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini, hivyo kuonyesha kuwa uhakika wa leo kuletwa kwa marehemu ni mkubwa mno.

No comments:

Post a Comment