Pages

Pages

Tuesday, May 07, 2013

Soma tamko lote la Ruge Mutahaba dhidi ya Lady Jay Dee



KATIKA siku za hivi karibuni katika vyombo vya habari hasa hasa kwenye mitandao ya kijamii nchini kumekuwa na taarifa rasmi na zisizo rasmi kutoka kwa Mwanamuziki Lady Jaydee alilalamikia Kituo chetu cha Clouds FM na wakurugenzi wake Ruge Mutahaba na Joseph Kussaga.
Ruge Mutahaba akizungumzia mustakabali wa Made in Tanzania sambamba na sakata lao na Lady Jay Dee

Kwa mtazamo wangu, kila mwananchi ana haki ya kutoa maoni yake ingawa kwenye nchi yetu ya Tanzania, tumezoea maoni hayo kutolewa kwa lugha ya ustaraabu na staha.

Maoni kuhusu nani wa kuja kwenye msiba wako au nyimbo za kupigwa kwenye msiba wako ni haki ya kila mwananchi na hakuna atayeuingilia uamuzi huo. Maoni pia ya redio gani mtu anaipenda au tv gani pia nayo ni utashi wa mtu mwenyewe. 

Uongozi wa Clouds FM ulikuwa umefikia maamuzi ya kutojadili jambo hili kutokana na kuamini kuwa ni tatizo binafsi la mtu na sio jambo lenye maslahi ya Taifa hivyo kwa uhalali linahitaji majadiliano au mazungumzo binafsi.

Sura ambayo jambo hili limewekwa na kulifanya kama dharura ya kitaifa sio sahihi kabisa  kutokana na kukosekana na hoja za kina za kuhitaji majibu na pili kukosekana kwa ujumla wa tija kwa tatizo hili kitaifa.

Bado ninaamini linatakiwa kubaki kama tatizo la mtu binafsi ila inapofika taarifa zikapotoshwa kwa nia ya kuwapa mtazamo tofauti wasikilizaji wetu, Clouds FM inataka kuweka maslahi ya wasikilizaji, wabia wetu wa biashara na watanzania wote mbele kwa kuwapa taarifa sahihi za jambo hili.

Clouds Media Group inapata lawama kubwa sana kutoka kwa watu wengi ambao pamoja na kuunga mkono ukimya wetu wanajiuliza ni kwanini hatukufanya jitihada za kumaliza tatizo hili bila kufika hatua iliyofikia sasa ya matusi, kebehi na vitisho kutwa vinavyoelekezwa kwetu na pia vinaendelea kuichafua tasnia ya muziki hasa hasa Bongo flava; ambayo imefika mahali inaonekana kila changamoto inayomkabili msanii wa Bongo flava lazima itatuliwe kwa njia za mabavu (matusi, vitisho na kuchafuana).

Lawama hizo sio za kweli na naomba nirudi nyuma kidogo kwenye historia ya jambo hili. Tarehe 14 mwezi wa 12 mwaka 2012 kwenye tweeter account ya Jaydee, alipost kifuatacho:

Nilichofanya ni kumpigia simu na kuzungumza nae.  Akasema sijaandika kwenye blog chochote, nikamwambia Jide mi nakuheshimu sana. Nimekupigia kwasababu naamini kama kuna kitu chochote ni bora nisikie kwako, nategemea na wewe pia utanipigia iwapo kuna jambo lolote lile. 

Tulikotoka sisi hatutakiwi kuendeshwa na majungu na maneno ya mtaani.Hiyo ilikuwa tarehe 14 mwezi December mwaka jana. Baada ya kama dk 10 hivi akanitumia msg ( ambazo bahati nzuri nilizihifadhi) na kusema ni kweli alikuwa ananizungumzia mimi kwa sababu kuna vitu kadhaa vinamsumbua na aliambiwa mimi ndo nilihusika navyo.

La kwanza, ‘nililipa matangazo ya shs laki mbili na 40 ila hayajachezwa na wala sijarudishiwa hela yangu, nimeambiwa umekataza matangazo yangu ya Nyumbani lounge yasipigwe’. 

La pili, naruhusu watangazaji wangu wamtukane ikiwa ni pamoja na kupromote zaidi bendi ya Skylight.

Pamoja na kwamba yeye alinitumia message, mimi nilimpigia simu na kumpa ufafanuzi wa yote hayo niliyosema hapo juu.


Nikasema, Biashara yetu sisi ni matangazo…..kwanini tukataze matangazo yako yasipigwe?? Labda bahati mbaya tu, jamaa anayebook matangazo alipitiwa kuyabook kibinadamu ila Gadna si anakuja hapa kila wakati, kwann asimkumbushe tu?? Tutayasogeza tu mbele hadi wiki inayofuata, kwanini niyakataze wakati muda sio mrefu tumetoka kuleta biashara ya Repa bora wa bendi hapo hapo Nyumbani lounge.


Niliendelea kujibu kuwa sio kweli kabisa, siwezi kuruhusu jambo kama hilo na kama ni kweli mtangazaji anamtukana anifahamishe ni nani na kwenye kipindi gani, nitasikiliza kipindi na kama ni kweli nitamfukuza kazi ( Clouds ina mitambo ya kuhifadhi matangazo yake yote kwa takribani miezi 9).

Hili nilimjibu kwa kirefu kidogo ikiwemo kumwambia akaze buti maana Skylight Band wanakuja juu nk nk. (Skylight Band ni bendi inayofanya vizuri sana hapa mjini na ilipoanza ilichukua baadhi ya majina makubwa kutoka Machozi Band).

Baada ya kumaliza mazungumzo tuliagana vizuri tu kwa miadi ya kukutana nikirudi maana nilikuwa safarini.

Kwahiyo ukiniuliza Jaydee anacholalamika ni nini??? Jibu langu litakuwa ni hayo mambo mawili maana hata nyie watanzania wenzangu mnaosoma mitandao ya kijamii mtakubaliana na mimi kuwa amekuwa anashambulia personality zetu, mimi na Mkurugenzi mwenzangu bila kuweka wazi hoja za msingi kuhusu yale anayotutuhumu nayo. 

Nimejitahidi sana kuelewa tatizo lake hasa ni nini na imekuwa inanipa shida kidogo?? Nimejitahidi sana kufikiria ni mirija ipi ya biashara kwake imeingiliwa, nakosa majibu??? 

Clouds FM ni ya watu na watu wanaweza kufanya makosa kweli na hata kusababisha matangazo ya laki 2 na 40 yasirushwe, kwa hilo nilishazungumza na Jaydee na kuomba radhi toka tarehe 14 December 2012. Clouds FM haina ubia wowote ule na Skylight Band (ni bendi iliyoanzishwa na Mtanzania)hivyo kuipromote ni katika misingi ile ile ya biashara kama tunavyopromote bendi yeyote ile na vilevile Clouds FM pia haihusiki kabisa na kutetereka kwa biashara ya chakula, vinywaji na bendi inayofanyika Nyumbani lounge. Inashangaza hata kuhusishwa na biashara ya Nyumbani lounge…!!!

Sina ugomvi binafsi na Jaydee wala Gadna, na tarehe 12 February mwaka huu, nilienda kuazima stools kwa ajili ya shooting kutoka kwenye sehemu yao ya biashara ingawa yeye amekiri kuwa na ugomvi mkubwa na sisi binafsi na Clouds kama chombo.

Nyimbo yake iliyotoka ya Joto Hasira ilipokelewa vizuri sana kulinganisha na nyimbo mbili zilizopita ‘Yeye’ na ‘Mimi ni mimi’ ambazo hazikufanya vizuri pamoja na jitihada kubwa ya kuzipromote.

Joto Hasira iliacha kupigwa kutokana na shinikizo lake mwenyewe, ikiwa imeshachezwa mara 48 ndani ya wiki tatu toka imetoka wote tulipigwa na bumbuwazi na kujiuliza ni kitu gani tumefanya kuambiwa hatupigi nyimbo na lawama nyingine.

Kama ofisi tukaona tukae kimya na kusubiri hatua inayofuata ukizingatia tuliendea kupiga nyimbo na video hata baada ya maneno makali ya mwanzo. Kauli haikubadilika, mbaya zaidi kauli za kebehi na kuchafuana zikaongezeka hadi kufikia uamuzi wa sisi kama taasisi kuamua rasmi kutopiga nyimbo zake hadi atakapofuta kauli zake na kuomba msamaha.

Kupiga au kutopiga nyimbo kwa kituo cha redio ni jambo la kawaida na kwasababu ni chombo binafsi ni muhimu kwa watu kama Jaydee na wasanii wengine (na hata wananchi wa kawaida) kuelewa kuwa kila ofisi ina taratibu zake na iwapo utatokea ukiukaji wa taratibu hizo, policy ndo zinaongoza maamuzi. 

Hebu tujiulize, mbona sio mjadala wa Taifa msanii Diamond hapigwi karibu miezi sita sasa kwenye station ya Magic FM, Ray C na Ali Kiba kwa karibu mwaka mzima walikuwa nyimbo zao na video hazipigwi na East Africa hadi walipoomba msamaha, hadi Yanga kwa muda mrefu walikuwa hawatangazwi habari zao kwenye chombo kimoja cha habari. Hayo ni mambo ya ofisi binafsi na hakuna anayeweza kulaumu maamuzi hayo.

‘Management reserves the right of admission’……nani hajaona kibao hiki kwenye hoteli nyingi tu nchini, nani asiyefahamu kuwa kuna hoteli ambazo ukienda kama mwanamke peke yako unakataliwa? 

Hizi ni taratibu na kila mahali zipo…..hata nyumbani lounge ndo maana Sam Machozi ambaye yuko Skylight Band zamani alikuwa mwanamuziki wa Machozi Band amepigwa marufuku pale Nyumbani lounge na halalamiki maana ni sehemu binafsi na ina taratibu zake. Ni tofauti na sehemu za wazi za umma kama Mnazi mmoja au kituo cha basi cha Magomeni.

Clouds Media Group inafuata taratibu zote za nchi na za kimkoa ila na yenyewe pia inaweka taratibu zake za uendeshaji. Sasa isifike mahali Clouds inapoweka taratibu zake hizo na kuzitekeleza inaonekana inafanya makosa.  

Yaani hata tarehe za kufanya show nchi hii tunatakiwa kupeleka maombi sehemu ili watu zaidi ya mmoja wasifanye show kweli???  Kwanini tunachanganya ushindani na fitina.

Acha ziwepo bendi 10 zinazoshindana, kuanzishwa kwa bendi nyingine kusiangaliwe kama fitna.  Na hata mtu akianzisha bendi kwa kuchukua wanamuziki kutoka kwenye bendi nyingine, si ndio dhana ya ushindani???

Kama ni kulalamika kuanzishwa kwa bendi nyingine au kuchukuliwa wanamuziki, Dadaangu Asha Baraka si angeshafanya maandamano nchi nzima. Ila wote tunatambua kuwa ni jasiri ndo maana anatulia na kuanza upya.

Mbona watu hawalalamiki  baa zinapofunguliwa 10 mtaa mmoja, au saloon za nywele, moja jirani na nyingine. Ni lazima tukubali na tuzoea ushindani.

Pamoja na ushindani kingine ninachoomba  kuwasihi watanzania wenzangu hasa hasa wasanii wetu  zaidi ni kuwa kila mtu na kila kitu kina ‘shelf life’. Watu wa zamani naamini wanamkumbuka Power Mabula.

Alikuwa anatisha sana wakati ule. Au nani anaweza kusahau umaarufu wa Mzee Nobert Chenga na Kundi la Muungano cultural troupe au labda huko ni nyuma sana; nani anamkumbuka Kanda Bongo Man, alicharge laki moja enzi hizooo….au labda hapa katikati umaarufu wa Muumini, Mr Nice au mtu kama Saida Karoli (alijaza Stadium).

Wote hao walikuwa maarufu sana. Sasa wasanii hawa na wengine wanaokuja wasipojiandaa kuelewa kuwa kila kitu kina muda wake, tutakuwa na taifa la vijana ambao asubuhi mpaka jioni badala ya kuhangaikia fursa nyingi zilizopo wataishia kutafuta mtu wa kumlaumu.

Ni lazima Edibily Lunyamila atarithiwa sehemu yake na kina Mrisho Ngassa ambaye naye muda utapita ni lazima atawaachia kina Simon Msuva. Wapo watu kama kina Dully Sykes walioanza kujiandaa kwa kuwaachia kina Diamond na wao kufungua studio na kuwa maproducer. 

Suala la kupokezana vijiti halikwepeki kuanzia makazini, mpirani na hata kwenye sanaa. Cha kufanya ni kujiandaa kwa maisha yako baada ya kugawa kijiti chako.
 
Taarifa za kutaka kuua muziki wa Bongo flava kwa makusudi zinashangaza, ili iweje sasa? Clouds inategemea matangazo ya biashara kama asilimia 95 ya mrija wa mapato na muziki tunaopiga redioni ni sehemu ya maudhui kwahiyo hakuna namna yeyote ile tutataka muziki huo upotee. Tunafanya juhudi zote hizi kwasababu tunahitaji nyimbo bora na wasanii bora ili tuweze kuendelea kuwa kituo bora cha redio.


No comments:

Post a Comment