Pages

Pages

Wednesday, May 29, 2013

Nafasi kibao za kazi zatangazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili



Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetangaza mamia ya nafasi za ajira kwa idara tofauti, wakiwamo madaktari bingwa na wauguzi wa vitengo, vikiwamo vya watoto na upasuaji wa moyo.

Miongoni mwa wanaohitajika ni madaktari bingwa daraja la pili 57 wa vitengo vya moyo, upasuaji, watoto, dawa za usingizi na mishipa.
Kati ya nafasi hizo zaidi ya 400, wanahitajika pia madaktari wa kawaida 85 ambao ni wa daraja la pili.

Kwa mujibu wa tangazo hilo la Mkurugenzi Mtendaji , madaktari bingwa wanatakiwa wawe wamesajiliwa katika Baraza la Madaktari la Tanganyika.
Wanahitajika pia maofisa wauguzi 22 ambao kati yao, nafasi moja ni kwa ajili ya Ofisa Mwandamizi, 11 ni maofisa wa daraja la kwanza na 10 ni wa daraja la pili.

Kwa upande wa maofisa wasaidizi, wanahitajika 10 wa daraja la kwanza na wengine 184 wa daraja la pili. Aidha, wanahitajika wataalamu saba kwa ajili ya kitengo cha mionzi.
Wataalamu wengine wanaohitajika ni wafamasia, wauguzi, maofisa afya na wataalamu wa maabara.

Kulingana na tangazo hilo, nafasi hizo zinatakiwa haraka kutokana na waombaji kuelekezwa kutuma maombi kabla ya Juni 21.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waombaji wanaofanya kazi katika taasisi za Serikali, maombi yao yanapaswa kupitia kwa waajiri na ajira zao zitahamishwa baada ya kuthibitishwa na Katibu Mkuu.
Ingawa wasemaji wa hospitali hiyo hawakupatikana jana kuelezea hali halisi ya rasilimaliwatu MNH, habari zilizowahi kuripotiwa na baadhi ya magazeti zilisema inakabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa wa upasuaji, hususan katika kitengo cha watoto.
Hata hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilipata kusema upungufu huo wa madaktari bingwa, hauathiri shughuli za tiba katika kitengo hicho cha magonjwa ya watoto.

No comments:

Post a Comment