Pages

Pages

Thursday, May 23, 2013

Mtwara yaendelea kuwa Uwanja wa vita, nyumba 10 zachomwa asubuhi hii, majonzi vuta nikuvute



Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Vita Mtwara yaendelea, mtaa wa Mkanarendi wageuka uwanja wa vita
HALI inazidi kuwa mbaya mkoani Mtwara, katika vuta nikuvute ya wananchi na askari polisi katika mvutano wa gesi, huku nyumba 10 asubuhi hii mtaa wa Mkanarendi zikichomwa moto na kuzua taharuki kubwa mjini hapa.
                             Hali ilivyokuwa mkoani Mtwara
Mtaa wa Mkanarendi ni ule unaoishi wananchi wa kawaida, hivyo jeshi la polisi limejazana katika mtaa huu kwa ajili ya kuendelea na harakati za kutuliza ghasia.

Handeni Kwetu Blog ilishuhudia nyumba hizo zikichomwa moto na kuendeleza mvutano wa wananchi, ikiwa ni mwendelezo wa tangu jana mchana baada ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kusoma hutuba ya Bajeti yake.

Kwa kawaida, mvutano huo ni mkubwa na ni hatari kubwa mjini hapa, huku vitu mbalimbali vya hatari vikitumiwa na kuwawafanya wananchi wengi waishi kwa hofu katika majumba yao.

Hata hivyo haitoshi, baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu nao wameingia kazini kuendeleza kufanya uhalifu wa aina mbalimbali, ikiwamo kuingia katika majumba ya watu na kuiba, hasa katika maduka na maeneo mengine.

Jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, aligeuka mbogo kwa kuwataka wote wanaondeleza kufanya ufedhuli huo wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kiini cha mgogoro huo ni wananchi wa mkoani Mtwara kutaka serikali isisafirishe gesi yao iliyogunduliwa mkoani kwao na kuipeleka jijini Dar es Salaam, badala yake shughuli zote zifanyike mjini hapa, ikiwa ni njia ya kuundeleza mji huo.

Jana mitaa mbalimbali iliwaka moto, ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto nyumba za serikali na baadhi ya madaraja ambayo ndio kiini cha maendeleo katika mji huo ambao baadhi ya wananchi wanadai umesahaulika.

No comments:

Post a Comment